TAARIFA YA MAFANIKIO YA MIAKA 60 YA UHURU WA TANZANIA BARA
JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA YA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI
TAARIFA YA MHESHIMIWA BALOZI LIBERATA MULAMULA (MB), WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI KWA VYOMBO VYA HABARI KUHUSU MAFANIKIO YA MIAKA 60 YA UHURU WA TANZANIA BARA
TAREHE 20 NOVEMBA, 2021, DODOMA
Ndugu wanahabari na wananchi mnaofuatilia matangazo haya mubashara, ninawasalimu kwa jina la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania …... Kazi iendelee!!!
Awali ya yote, nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema kwa kutuwezesha kukutana hapa siku ya leo tukiwa na afya njema. Pia nitumie fursa hii kuwashukuru kwa namna ya pekee kwa kufika kwenu kwa wingi. Ni matarajio yangu kuwa kupitia vyombo vya habari mnavyoviwakilisha, watanzania na dunia kwa ujumla itaweza kufahamu kuhusu mafanikio ya Serikali kupitia Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, wakati huu Taifa likielekea kuadhimisha miaka 60 ya Uhuru wa Tanzania Bara.
Pili, nawapongeza kwa kuendelea kutekeleza majukumu yenu kwa weledi na uzalendo ambao umeiwezesha nchi yetu kuendelea kuwa Taifa lenye amani, umoja na mshikamano, na sasa tunaelekea kuadhimisha miaka 60 ya uhuru tukiwa imara na wamoja kama Taifa.
Ndugu wanahabari, kama mnavyofahamu, kila ifikapo tarehe 9 Desemba nchi yetu huadhimisha uhuru wa Tanzania Bara, na kipekee kwa mwaka huu Serikali imetoa kipaumbele katika kuuhabarisha umma wa Watanzania na dunia kwa ujumla kuhusu mafanikio yaliyopatikana katika kipindi cha miongo sita iliyopita. Na kwa muktadha huo nitaeleza kwenu, kwa uchache, mafanikio ambayo Tanzania imeyapata kupitia mahusiano ya kimataifa kwa kutekeleza Sera ya Mambo ya Nje katika kipindi cha miaka 60 iliyopita. Maelezo yangu yataainisha utekelezaji wa majukumu, malengo na mikakati ya Wizara ninayoiongoza katika kipindi husika.
Ndugu wanahabari, kabla sijaendelea, napenda kuwafahamisha kuwa, dhamana ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki ni kusimamia uhusiano kati ya Tanzania na mataifa mengine duniani, jumuiya za kikanda na mashirika ya kimataifa kwa lengo la kulinda na kutetea maslahi ya Tanzania kimataifa. Utekelezaji wa majukumu ya Wizara unaongozwa na Sera ya Mambo ya Nje ya Mwaka 2001 pamoja na miongozo mingine ya Serikali.
HISTORIA YA WIZARA
Ndugu wanahabari, kama ilivyo kwa Wizara nyingine, historia ya Wizara hii inaanzia pale Tanzania Bara (wakati huo Tanganyika) ilipopata uhuru kutoka kwa Uingereza tarehe 09 Desemba 1961. Wizara ilianza ikiwa ni Idara ya Mambo ya Nje na Ulinzi chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu, ambaye kwa wakati huo alikuwa ni Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere. Mwaka 1963, Idara ya Mambo ya Nje na Ulinzi ilibadilishwa na kuwa Wizara ya Mambo ya Nje na Ulinzi. Mwaka 1965, majukumu ya ulinzi yaliondolewa kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na tangu hapo jina la Wizara hii limekuwa likibadilika kutokana na dhamana na majukumu ya wakati husika. Mwaka 2016, majukumu ya zilizokuwa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa na Wizara ya Ushirikiano wa Afrika Mashariki yaliunganishwa na kuundwa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki. 3
Ndugu wanahabari, mara tu baada ya kupata uhuru, kipaumbele cha Serikali kilikuwa ni kuongeza ushirikiano na uhusiano na mataifa mengine duniani na taasisi za kimataifa ambapo ilitulazimu kufungua ofisi za uwakilishi na kupeleka watumishi nje ya nchi ili kuongeza ufanisi wetu katika kushiriki masuala ya kimataifa. Mnamo mwaka 1962 Serikali iliteua mabalozi wa kuiwakilisha Tanzania katika nchi ya Uingereza na Umoja wa Mataifa - New York, Marekani. Aidha, Serikali ilifungua milango kwa nchi nyingine na mashirika ya kimataifa kufungua ofisi za uwakilishi hapa nchini, ambapo Serikali za Uingereza na Ujerumani zilikuwa ni nchi za kwanza kufungua Balozi zao hapa nchini.
Ndugu Wanahabari, kwa sasa tunapoelekea kuadhimisha miaka 60 ya Uhuru wa Tanzania Bara, Nchi yetu ina Balozi 44 na Konseli Kuu 6 katika nchi mbalimbali duniani ambapo katika kipindi hiki cha Serikali ya Awamu ya Sita (6) Ubalozi mmoja (1) umefunguliwa Vienna, Austria. Pia, Tanzania ni mwenyeji wa Balozi 62 na Mashirika ya Kimataifa 30.
Ndugu wanahabari, ili kuwezesha watumishi katika balozi zetu nje kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi na weledi, Serikali imekuwa ikinunua, kujenga au kupanga majengo ya ofisi na makazi ya watumishi balozini, ambapo hadi hivi sasa Serikali inamiliki viwanja 12 na majengo 106 nje ya nchi. Serikali imeendelea kukarabati majengo hayo na kuendeleza kwa awamu viwanja hivyo, ambapo kwa sasa inatekeleza miradi minne (4) ya ujenzi wa majengo ya ofisi na makazi ya watumishi kwenye Balozi za Tanzania Nairobi - Kenya, Kinshasa – Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Moroni - Comoro na Muscat - Oman.
Ndugu wanahabari, Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imedhamiria kuendelea kuimarisha ushirikiano na uhusiano baina ya nchi yetu na mataifa mengine, jumuiya za kikanda na kimataifa, ambapo katika kipindi kifupi cha kuwepo madarakani tayari imepeleka watumishi wengi zaidi kuhudumu katika balozi zetu.
Ndugu wanahabari, tangu uhuru hadi sasa, Serikali kupitia Wizara hii imetekeleza kwa mafanikio ya kujivunia sera ya mambo ya nje ambayo mwanzo ilijikita katika kutetea haki za wanyonge na kupiga vita ukoloni na ukoloni mamboleo; kupinga siasa za ubaguzi na ukandamizaji wa aina zote; kuendeleza Umoja wa Afrika; na kuunga mkono sera ya kutofungamana na upande wowote. Mafanikio yaliyopatikana kupitia utekelezaji wa sera hiyo ni pamoja na kulinda, kutetea na kudumisha uhuru wetu; na mchango wa Tanzania katika ukombozi wa nchi za kusini mwa Afrika, kutokomeza siasa za ubaguzi wa rangi Afrika Kusini na kujenga umoja na mtangamano wa kikanda na Bara la Afrika.
Ndugu wanahabari, ilipofika miaka ya 1990, msisitizo wa Sera ya Mambo ya Nje ulihuishwa na kujumuisha masuala ya kiuchumi na kijamii baada ya nchi nyingi barani Afrika hususani zilizopo kusini mwa Afrika kupata uhuru na kukomeshwa kwa siasa za kibaguzi nchini Afrika Kusini. Sababu nyingine za kuhuisha sera yetu ya mambo ya nje ni pamoja na kumalizika kwa vita baridi duniani na kuibuka kwa utandawazi na mageuzi ya kisiasa, kiuchumi na kijamii.
Kwa kuzingatia mabadiliko hayo, mwaka 2001 Serikali ilitunga sera mahsusi kwa ajili ya kusimamia mambo ya nje ambayo iliendelea kubeba misingi ya kulinda uhuru wa kujiamulia mambo yetu wenyewe; kuheshimu mipaka ya nchi na uhuru wa kisiasa; kulinda uhuru, haki za binadamu, usawa na demokrasia; kukuza ujirani mwema; kuendeleza Umoja wa Afrika; kukuza ushirikiano wa kiuchumi na wabia wa maendeleo; kuunga mkono utekelezaji wa sera ya kutofungamana na upande wowote; kuimarisha ushirikiano wa nchi zinazoendelea; na kuunga mkono Umoja wa Mataifa na jitihada zake za kuimarisha maendeleo ya uchumi wa kimataifa, amani na usalama.
Ndugu wanahabari, Sera ya Mambo ya Nje ya mwaka 2001 iliweka bayana azma ya Serikali kukuza uchumi na maendeleo ya Taifa kupitia mahusiano ya kimataifa, ambapo msisitizo mkubwa ulielekezwa katika kutekeleza diplomasia ya uchumi. Jitihada za Serikali zilielekezwa katika kuongeza wigo wa biashara ya kimataifa kupitia utafutaji wa masoko ya bidhaa mbalimbali za Tanzania nje ya nchi, kuvutia uwekezaji wa mitaji na teknolojia kutoka nje katika sekta za kijamii na kiuchumi, kutangaza vivutio vya utalii, kuongeza fursa za ajira na masomo kwa watanzania nje ya nchi na kushawishi upatikanaji wa misaada na mikopo ya masharti nafuu kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo nchini.
MAFANIKIO YA TANZANIA KATIKA HARAKATI ZA UKOMBOZI BARANI AFRIKA 5
Ndugu wanahabari, tangu kupata uhuru hadi miaka ya 1990, Tanzania ilikuwa mstari wa mbele kupigania ukombozi wa nchi za Afrika hususan zile za Kusini mwa Afrika kutoka katika utawala wa kikoloni sanjari na kupinga ubaguzi dhidi ya mwafrika. Katika kipindi hicho, Tanzania ilichangia rasilimali fedha, askari pamoja na ardhi yake kusaidia wapigania uhuru kutoka nchi nyingine za Afrika ikiwemo Angola, Namibia, Zimbabwe, Afrika Kusini na Msumbiji. Imani ya waasisi wa nchi yetu wakati huo ilikuwa ni kwamba uhuru wa Tanzania hautakuwa kamili endapo nchi zinazotuzunguka zitakuwa hazijapata uhuru wa kujitawala zenyewe.
Ndugu wanahabari, ili kufanikisha azma hiyo, Tanzania ilishirikiana pia na nchi nyingine za Afrika zilizokuwa zimepata uhuru kipindi hicho na ambazo viongozi wake walikuwa na dhamira sawa ya kuchangia katika harakati za ukombozi wa Bara la Afrika. Mnamo mwaka 1970 Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere aliungana na Hayati Kenneth Kaunda, Rais wa Jamhuri ya Zambia na Hayati Seretse Khama, Rais wa Botswana na kuanzisha umoja wa Nchi zilizo Mstari wa Mbele (Frontline States) katika kupigania ukombozi wa nchi zilizo kusini mwa Afrika kutoka katika utawala wa kikoloni na kupinga ubaguzi uliokuwa ukifanywa na Makaburu katika nchi ya Afrika Kusini pamoja na utawala wa wachache katika nchi ya Rhodesia.
Ndugu wanahabari, pamoja na harakati za ukombozi wa kisiasa na vita dhidi ya ubaguzi, majadiliano kati ya Nchi Zilizo Mstari wa Mbele kuhusu ushirikiano wa kiuchumi yalianza kupewa msukumo katika miaka 1970, na hatimaye nchi hizo (Frontline States) na nchi zilizopata uhuru baadaye ziliungana na kuanzisha mtangamano wa kiuchumi ambao awali ulijulikana kama Jukwaa la Uratibu wa Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADCC) mwaka 1980 kabla ya kuwa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) mwaka 1992. Kupitia SADC Tanzania imeendeleza harakati zake za kulinda amani na usalama katika ukanda wa kusini mwa Afrika ambapo tumechangia kutafuta ufumbuzi wa migogoro katika nchi za Lesotho, Madagascar, Comoro, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) na Msumbiji. 6
Ndugu wanahabari, mchango wa Tanzania katika harakati za ukombozi na kupigania uhuru katika nchi za kusini mwa Afrika umehifadhiwa katika juzuu maalum kupitia Mradi wa Hashim Mbitta ulioanzishwa na SADC kuenzi harakati hizo. Hii ni heshima ya kipekee kwa Tanzania, kwani kumbukumbu hizo zitadumu na kuifanya historia ya mchango wa nchi yetu katika ukombozi wa nchi za kusini mwa Afrika kuishi vizazi na vizazi.
Ndugu wanahabari, mbali na nchi za Kusini mwa Afrika, Tanzania ilifanikiwa kuiondoa madarakani Serikali ya Hayati Iddi Amin, iliyokuwa ikitawala kimabavu nchini Uganda kupitia vita inayojulikana na wengi kama Vita ya Kagera mwaka 1977-1978. Uamuzi wa Serikali ya Tanzania kipindi hicho ulikuwa ni muhimu kwa lengo la kulinda usalama wa mipaka ya nchi yetu. Aidha, hatua hiyo ilirejesha utawala wa sheria nchini Uganda na utulivu wa kisiasa ambao umedumu hadi hivi sasa.
Ndugu wanahabari, jitihada hizo pamoja na utulivu wa kisiasa na uwepo wa amani nchini uliodumu kwa kipindi chote tangu Uhuru, imeifanya Tanzania kujijengea heshima na kutambulika na jumuiya ya kimataifa kama kisiwa cha amani na mshirika katika masuala ya ukombozi, ulinzi na usalama katika Bara letu la Afrika na duniani kwa ujumla, jambo ambalo Tanzania inajivunia hata sasa tunapoadhimisha miaka 60 ya Uhuru wetu.
MAFANIKIO YA TANZANIA KATIKA ULINZI WA AMANI NA USALAMA BARANI AFRIKA NA DUNIANI
Ndugu wanahabari, Tanzania inajivunia mchango wake katika juhudi za kuhakikisha uwepo wa amani, ulinzi na usalama Barani Afrika na duniani kwa ujumla, katika kipindi cha miaka 60 iliyopita. Masuala hayo (amani, ulinzi na usalama) pia ni miongoni mwa tunu na urithi wa Taifa letu.
Ndugu wanahabari, katika kipindi hicho, Tanzania imeshiriki katika utatuzi wa migogoro kwa njia ya mazungumzo kwenye nchi mbalimbali duniani. Ushiriki wa Tanzania katika harakati hizo umekuwa wa moja kwa moja au kupitia jumuiya za kikanda. Kwa mfano, mwaka 1999 Tanzania ilishiriki katika kuzipatanisha pande mbili zilizokuwa zikihasimiana nchini Burundi. Mpatanishi Mkuu katika mgogoro huo alikuwa Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere kabla ya kifo chake na baadaye juhudi hizo ziliendelezwa na Hayati Benjamini Mkapa, Rais wa Awamu ya Tatu. Usuluhishi wa mgogoro huo ulitamatishwa kwa pande zinazohasimiana kusaini Makubaliano ya Amani na Maridhiano ya Arusha mwaka 2000 na Makubaliano ya Kusitisha Mapigano mwaka 2005, ambayo yamedumisha amani nchini Burundi hadi hivi sasa.
Halikadhalika, mwaka 2015 Jumuiya ya Afrika Mashariki ilimteua Hayati Benjamin Mkapa kuongoza Majadiliano ya Amani ya Burundi baina ya pande zilizokuwa zikihasimiana nchini humo kufuatia mgogoro wa kikatiba uliombatana na machafuko yaliyotokana na tofauti za kisiasa.
Ndugu wanahabari, Vilevile, mwaka 2008 na 2013, Tanzania ilishiriki katika upatanishi wa pande zilizokuwa zikihasimiana nchini Kenya kutokana na tofauti za kisiasa zilizoambatana na vurugu za uchaguzi mkuu. Mwaka 2008, Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Awamu ya Nne alialikwa kuzipatanisha pande zilizokuwa zikihasimiana nchini Kenya. Mwaka 2013, Hayati Benjamin Mkapa, Rais wa Awamu ya Tatu alishiriki kwenye upatanishi wa pande zilizokuwa zikihasimiana nchini Kenya akiwa kama mjumbe wa jopo la watu mashuhuri chini ya uangalizi wa Umoja wa Afrika. Jopo hilo lilikuwa likiongozwa na Hayati Koffi Annan, aliyewahi kuwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa.
Ndugu wanahabari, pamoja na kushiriki katika usuluhishi wa migogoro na upatanishi, katika kipindi cha miaka 60 Tanzania pia imetoa hifadhi kwa raia wanaozikimbia nchi zao kutokana na changamoto za kiusalama hususani nchi za Ukanda wa Maziwa Makuu. Baadhi ya wakimbizi hao, hususani walioishi nchini kwa muda mrefu au kuzaliwa na wazazi wao wakiwa ukimbizini hapa nchini, wamepatiwa uraia na wanaendelea na shughuli za kijamii na kiuchumi kama walivyo raia wengine wa Tanzania.
Ndugu wanahabari, mifano hiyo michache inaonesha jinsi gani nchi yetu ilivyo kuwa katika mstari wa mbele kulinda, kutetea na kudumisha amani katika nchi nyingine majirani na duniani. Aidha ushiriki wa Tanzania katika usuluhishi na upatanishi wa migogoro ni kielelezo cha kuaminiwa kwa nchi yetu katika kudumisha amani kimataifa.
Ndugu wanahabari, Tanzania pia imechangia walinda amani kwenye misheni tano za kulinda amani za Umoja wa Mataifa, ambapo hadi kufikia mwezi Septemba 2021, ilikuwa na jumla ya walinda amani 1,483 katika Misheni za MINUSCA (Afrika ya Kati), MONUSCO (Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo), UNIFIL (Lebanon), UNISFA (Abyei, Sudan) na UNIMISS (Sudan Kusini). Idadi hiyo ya walinda amani inaifanya Tanzania kuwa nchi ya 13 kati ya nchi 122 zinazochangia kwa wingi walinda amani katika misheni za kulinda amani duniani.
Ndugu wanahabari, tunapoelekea kuadhimisha miaka 60 ya Uhuru wa Tanzania Bara, mipaka ya nchi yetu imeendelea kubaki salama ikichagizwa na utulivu na amani iliyopo nchini. Aidha, hali ya ujirani mwema pamoja na uhusiano wa kidugu uliopo baina yetu na nchi zinazotuzunguka, imesaidia nchi yetu kuendelea kuwa na amani katika ukanda wetu ambao una baadhi ya nchi zinazokabiliwa na migogoro ya wenyewe kwa wenyewe pamoja na changamoto za kiusalama.
Ndugu wanahabari, kama kielelezo cha sifa adhimu ya utulivu na amani iliyopo nchini, Taarifa ya Global Peace Index ya mwaka 2020 imeitaja Tanzania kuwa ni nchi ya kwanza (1) kwa amani na utulivu kwenye Ukanda wa Afrika Mashariki na ya saba (7) katika nchi zilizopo Kusini mwa Jangwa la Sahara.
Ndugu wanahabari, ninatoa rai kwenu na kwa Watanzania wote kuendeleza amani, umoja na mshikamano uliodumu kwa kipindi cha miaka 60 iliyopita. Aidha Serikali ya awamu ya Sita chini ya Uongozi wa Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania itaendelea kudumisha amani, umoja na mshikamano huo sambamba na kuendelea kutetea, kulinda na kudumisha usalama na amani duniani kwa kushirikiana na jumuiya ya kimataifa.
MAFANIKIO YA TANZANIA KATIKA USHAWISHI NA UONGOZI NDANI YA JUMUIYA NA TAASISI ZA KIMATAIFA 9
Ndugu wanahabari, ushiriki wa nchi yetu ndani ya jumuiya na taasisi za kimataifa katika miongo sita (6) iliyopita umekuwa wa mafanikio ambapo Tanzania imekuwa mstari wa mbele kupaza sauti na kuishawishi jumuiya ya kimataifa katika masuala mbalimbali yenye maslahi kwa Taifa letu na dunia kwa ujumla. Mathalan, mwaka 1972 Tanzania iliungana na baadhi ya nchi zinazoendelea kuzishawishi nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa kuirejeshea nafasi ya kudumu Jamhuri ya Watu wa China katika Baraza la Usalama la Umoja huo iliyokuwa imetwaliwa na Jamhuri ya China (Taiwan). Vilevile, Tanzania kupitia Ushirikiano wa Nchi za Kusini (South South Cooperation) imekuwa ikikemea mifumo kandamizi ya kiuchumi na kisiasa na kutetea haki na usawa kwa nchi zote. Aidha, kupitia ushirikiano huo, Tanzania imeendelea kuzitaka nchi zilizoendelea kuheshimu ahadi zao za kutoa asilimia moja ya utajiri wao kuzisaidia nchi zinazoendelea kujikwamua na umaskini.
Katika kuendeleza msimamo huo wa kutetea haki na usawa kwa nchi zote ulimwenguni, katika miaka ya hivi karibuni Tanzania imekuwa mstari wa mbele kuitaka jumuiya ya kimataifa, hususani nchi za magharibi, kuiondolea Zimbabwe vikwazo vya kisiasa na kiuchumi. Sambamba na hilo, Tanzania imeweka bayana msimamo wake wa kupinga ukandamizaji unaofanywa kwa nchi mbalimbali duniani ikiwemo Cuba na mataifa ya Saharawi ya Magharibi na Palestina.
Ndugu wanahabari, katika kipindi hiki ambacho dunia inakabiliwa na athari za kiafya na kiuchumi kutokana na mlipuko wa UVIKO-19, Tanzania kupitia majukwaa mbalimbali ya kikanda na kimataifa imeeleza waziwazi msimamo wake wa kuzitaka nchi zilizoendelea kuyawezesha mataifa yanayoendelea kujijengea uwezo wa kuzalisha chanjo, dawa na vifaa tiba ili kukabiliana na magonjwa mbalimbali ya mlipuko ikiwemo UVIKO-19.
Ndugu wanahabari, kutokana na msimamo huo thabiti pamoja na ushawishi wa nchi yetu katika jumuiya ya kimataifa, Tanzania kwa nyakati tofauti imeaminiwa na kupewa dhamana za uongozi katika ngazi mbalimbali ndani ya jumuiya za kikanda na kimataifa. Mfano, Tanzania imewahi kuwa mwanachama asiye wa kudumu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwa vipindi viwili, mwaka 1975 hadi 1976 na mwaka 2005 hadi 2006.
Aidha, Tanzania imechaguliwa kuwa Makamu wa Rais wa Kikao cha 76 cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa (UNGA 76) kinachoendelea hivi sasa New York, Marekani.
Tanzania pia imekuwa mwenyekiti wa Umoja wa Nchi Huru za Afrika (OAU) ambao kwa sasa unajulikana kwa jina la Umoja wa Afrika (AU) mara mbili, mwaka 1984 hadi 1985 na mwaka 2008. Tanzania imekuwa mwenyekiti wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) kwa vipindi viwili, mwaka 2004 na 2019. Kipekee, pia Tanzania imekuwa mwenyekiti wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa miaka miwili (2) mfululizo mwaka 2015 na 2016.
Kadhalika, Watanzania mbalimbali wamechaguliwa kushika nyadhifa za juu na za maamuzi katika jumuiya za kikanda na kimataifa. Mfano, Mhe. Balozi Salim Ahmed Salim, Waziri Mkuu Mstaafu, alikuwa Katibu Mkuu wa OAU kwa vipindi viwili mfululizo kuanzia mwaka 1989 hadi 2001; Mhe. Balozi Mstaafu Getrude Mongela alikuwa Spika wa kwanza wa Bunge la Umoja wa Afrika kuanzia mwaka 2004 hadi 2009; Mhe Balozi Dkt. Asha – Rose Migiro, ambaye kwa sasa ni Balozi wa Tanzania nchini Uingereza alikuwa Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kwa kipindi cha miaka sita kuanzia 2007 hadi 2012; Balozi Liberata Mulamula (Mb), ambaye kwa sasa ni Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki alikuwa Katibu Mtendaji wa kwanza wa Jumuiya ya Nchi za Ukanda wa Maziwa Makuu (ICGLR) kuanzia 2006 hadi 2011; na Mhe. Dkt. Stergomena Tax (Mb), ambaye kwa sasa ni Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa alikuwa Katibu Mtendaji wa kwanza mwanamke wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) kwa vipindi viwili mfululizo kuanzia mwaka 2013 hadi 2021.
Ndugu wanahabari, watanzania wengine waliowahi kushika nyadhifa za uongozi katika jumuiya za kimataifa ni pamoja na Mhe.Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aliyewahi kuwa Mjumbe wa Jopo la Ngazi ya Juu la Wataalam wa Umoja wa Mataifa Kuhusu Masuala ya Uwezeshaji Wanawake Kiuchumi; Prof. Anna Tibaijuka, aliyewahi kuwa Katibu Mtendaji wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Makazi; Dkt. Winnie Mapunju Shumbusho, aliyewahi kuwa Mkurugenzi Msaidizi wa Shirika la Afya Duniani ; na Hayati Balozi Augustine Mahiga, aliyewahi kuwa Mjumbe Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu mgogoro wa Somalia.
Ndugu wanahabari, wapo pia watanzania ambao hivi sasa wanaongoza jumuiya za kikanda na mashirika ya kimataifa. Kwa kuwataja wachache ni pamoja na Balozi Ali Mchumo, ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la International Bamboo and Rattan Organisation kwa kipindi cha miaka mitatu kuanzia mwaka 2019 hadi 2022; Mhe Jaji Imani Aboud ambaye ni Rais wa Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu kwa kipindi cha miaka sita kuanzia 2021; na Mhe Balozi Maimuna Tarishi, Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania ndani ya Umoja wa Mataifa – Geneva na Vienna ambaye ni Rais wa Bodi ya Biashara na Maendeleo ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Biashara na Maendeleo kwa kipindi cha mwaka mmoja kuanzia 2021 hadi 2022.
Ndugu wanahabari, wingi wa wanawake katika orodha ya watanzania walioshika nyadhifa za uongozi na maamuzi katika jumuiya za kimataifa ni kielelezo cha Serikali yetu kuthamini mchango wa mwanamke katika masuala ya uongozi na uhusiano wa kimataifa.
Ndugu wanahabari, Serikali ya Awamu ya Sita imelipa kipaumbele suala la kuongeza ajira kwa Watanzania nje ya nchi na katika taasisi za kimataifa, ambapo katika kipindi cha muda mfupi tangu kuingia madarakani, fursa za ajira nje ya nchi zipatazo 70 zilitangazwa kwa umma kwa watanzania wenye sifa kuzichangamkia. Fursa hizo zinajumuisha nafasi nne (4) za ajira katika Shirika la Afya Duniani; Umoja wa Afrika (22); Umoja wa Mataifa (1); Benki ya Maendeleo ya Afrika (26); Jumuiya ya Nchi za Ukanda wa Maziwa Makuu (1); Shirika la Jumuiya ya Nchi za Afrika, Caribbean na Pacific (5); na Shirika la Kuzuia Matumizi ya Silaha za Kemikali (6). Ninatoa wito kwa watanzania kuendelea kufuatilia fursa za ajira za kimataifa zinazotangazwa na Serikali mara kwa mara na kuomba nafasi hizo ili kuongeza wigo wa watanzania kwenye ajira kimataifa.
UENYEJI WA TAASISI NA MASHIRIKA YA KIKANDA NA KIMATAIFA PAMOJA NA MIKUTANO YA KIMATAIFA
Ndugu wanahabari, ishara mojawapo ya kuaminika na kukubalika kwa nchi yoyote kimataifa ni nchi husika kupewa uenyeji wa taasisi na mashirika ya kikanda na kimataifa pamoja na kuandaa mikutano ya kimataifa. Tanzania katika miaka 60 inajivunia kuwa mwenyeji wa taasisi na mashirika ya kimataifa. Miongoni mwa taasisi na mashirika ya kimataifa yenye makao makuu au ofisi za uwakilishi hapa nchini ni pamoja na Jumuiya ya Afrika Mashariki, Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu, Kamisheni ya Kiswahili ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, Bodi ya Ushauri ya Masuala ya Rushwa ya Umoja wa Afrika, Umoja wa Mataifa na Mashirika yake, Taasisi ya Afrika ya Sheria za Kimataifa, Chuo cha Upasuaji cha Afrika Mashariki, Kati na Kusini, Umoja wa Posta Afrika na Chuo cha Afrika Mashariki cha Takwimu.
Ndugu wanahabari, pamoja na mashirika na taasisi hizi kuitangaza nchi yetu kimataifa, uwepo wake una faida za kiuchumi pia. Miongoni mwa faida za kiuchumi tunazopata kwa kuwa mwenyeji ni pamoja na ajira kwa watanzania, upatikanaji wa fedha za kigeni na uhawilishaji wa ujuzi na utaalam.
Ndugu wanahabari, katika kuonesha dhamira yake ya kuendelea kuvutia mashirika na taasisi za kimataifa kuwa na makao makuu au ofisi za uwakilishi nchini, Serikali imetenga eneo lenye ukubwa wa ekari 431 la Lakilaki, jijini Arusha kwa ajili ya ujenzi wa taasisi za kimataifa. Hadi sasa Mahakama ya Kimataifa ya Masalia ya Kesi za Mauaji ya Kimbari ya Rwanda imeanzisha ofisi zake katika eneo hilo.
Ndugu wanahabari, Tanzania pia inajivunia kuwa mwenyeji wa mikutano ya kimataifa katika kipindi cha miaka 60 ya uhuru. Baadhi ya mikutano ya kimataifa ambayo tumekuwa nchi mwenyeji ni pamoja na Mikutano ya Wakuu wa Nchi na Serikali ya SADC iliyofanyika mwaka 2004 na 2019; Mkutano wa Sullivan uliofanyika mwaka 2008; Mkutano wa Smart Partnership uliofanyika mwaka 2013; Mikutano mbalimbali ya Wakuu wa Nchi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki; na Mkutano wa Nordic-Africa uliofanyika mwaka 2019.
Ndugu wanahabari, tunapoelekea kuadhimisha miaka 60 ya uhuru na kuanza safari ya miaka mingine 60 ijayo, Tanzania itaendelea kuwa mwenyeji wa mikutano ya kimataifa ikiwemo, Mkutano wa 65 wa Kamisheni ya Afrika na Jukwaa la Pili la Uwekezaji kwenye
Utalii uliopangwa kufanyika mwaka 2022. Mikutano hiyo pamoja na kuitangaza nchi kimataifa, ni kichocheo cha ukuaji wa sekta mbalimbali za uchumi kama vile utalii, biashara, uchukuzi, malazi na hoteli.
Ndugu wanahabari, kiashiria kingine cha uimara wa uhusiano kati ya Tanzania na jumuiya ya kimataifa ni uwepo wa miadi na ziara za viongozi wakuu wa kitaifa na mashirika ya kimataifa. Katika kipindi cha miaka 60 iliyopita, viongozi wakuu wa kitaifa kwa nyakati tofauti wamekuwa wakifanya ziara nje ya nchi na viongozi wakuu kutoka mataifa mengine pamoja na mashirika ya kimataifa wamekuwa wakiitembelea Tanzania.
Kupitia ziara hizo Tanzania imenufaika na uwekaji saini makubaliano na mikataba ya ushirikiano katika nyanja za kiuchumi, kijamii na kisiasa. Mfano, kufuatia ziara ya Mhe. Barack Obama, Rais Mstaafu wa Marekani hapa nchini mwaka 2013, nchi yetu ilijumuishwa katika Mpango wa Kukabiliana na Changamoto za Milenia (Millenium Challenge Compact-MCC), ambapo kupitia Awamu ya Kwanza ya Mpango huo tulipata fedha kiasi cha Dola za Marekani milioni 698 kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo. Baadhi ya maeneo yaliyonufaika na miradi ya MCC-I ni Dodoma, Tanga, Morogoro, Iringa, Mbeya, Kigoma, Mwanza, Manyara, Njombe, Geita na Zanzibar.
Ndugu wanahabari, orodha ya ziara za viongozi wakuu wa kitaifa na mashirika ya kimataifa wa ndani na nje katika kipindi cha miaka 60 ni ndefu na manufaa yake kwa nchi yetu ni makubwa. Kwa kutambua hilo, Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Mhe, Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imezipa msukumo ziara za kimataifa ambapo, tangu kuingia madarakani nchi yetu imepokea viongozi mbalimbali wa kitaifa na mashirika ya kimataifa.
Aidha, Mhe. Rais amefanya ziara katika nchi mbalimbali zenye manufaa ya kisiasa, kiuchumi na kijamii. Mfano, kufuatia ziara ya Mhe. Rais Samia nchini Kenya mwezi Mei 2021, Tanzania na Kenya zilikubaliana kuondoleana vikwazo vya muda mrefu visivyo vya kiforodha 46 kati ya 64. Hatua hiyo imechochea ukuaji wa biashara na uwekezaji baina ya nchi hizi mbili, ikiwemo Tanzania kuwa na urari chanya wa biashara baina yake na Kenya. Taratibu za kuondoa vikwazo 18 vilivyosalia ambavyo ni vya kiutawala zinaendelea.
Ndugu wanahabari, ninatoa rai kwenu kuendelea kuuhabarisha na kuuelimisha umma wa watanzania na dunia kwa ujumla kuhusu manufaa ya ziara zinazofanywa na viongozi wetu wa kitaifa nje ya nchi pamoja na zara za viongozi kutoka mataifa mengine nchini.
MAFANIKIO YA TANZANIA KATIKA KUKUZA MATUMIZI YA LUGHA YA KISWAHILI DUNIANI
Ndugu wanahabari, historia inaonesha kuwa, lugha ya Kiswahili imetumika katika harakati za ukombozi na kupigania uhuru katika nchi za ukanda wa Mashariki, Kati na Kusini mwa Afrika ikiwemo Tanzania. Kiswahili pia kinazungumzwa kwa wingi katika nchi zenye uhusiano wa karibu wa kihistoria na nchi za mashariki mwa Afrika kama vile nchi ya Oman, kutokana na lugha hiyo kutumika kurahisisha ufanyaji wa biashara kabla na wakati wa ukoloni. Hata hivyo, nchi yetu imekuwa kinara katika matumizi ya lugha hiyo kiasi cha kutambulika kimataifa kama nchi waasisi wa lugha hiyo. Kwa kutambua manufaa ya lugha ya Kiswahili, Tanzania imeendelea kukuza na kueneza matumizi ya lugha hiyo Barani Afrika na duniani kwa ujumla. Kufuatia jitihada hizo, lugha ya Kiswahili sasa inakadiriwa kuwa ya tatu kwa kuwa na watumiaji wengi barani Afrika baada ya Kiingereza na Kiarabu, na ya kumi (10) duniani.
Ndugu wanahabari, katika kipindi cha miaka 60 ya uhuru, Tanzania inajivunia lugha ya Kiswahili kuwa lugha rasmi inayotumika katika mikutano ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) na Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC). Aidha, Serikali inaendelea na jitihada za kuhakikisha kuwa lugha ya Kiswahili inakuwa lugha rasmi katika Umoja wa Afrika (AU) na Umoja wa Mataifa, ambapo hadi sasa Kiswahili kinatumika kutafsiri mijadala katika mikutano ya wakuu wa nchi na serikali wa Umoja wa Afrika. Pia, Idhaa ya Kiswahili imeanzishwa katika Radio na Televisheni ya Umoja wa Mataifa. Vilevile, Shirika 15 la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) limeitangaza tarehe 7 Julai ya kila mwaka kuwa siku maalum ya kuadhimisha lugha ya Kiswahili duniani.
Halikadhalika, Serikali kupitia baadhi ya Balozi za Tanzania nje, imeanzisha madarasa ya kufundisha lugha ya Kiswahili katika ngazi za awali, kati na juu. Mfano Ubalozi wa Tanzania Seoul, Jamhuri ya Korea umefanikiwa kufundisha jumla ya wanafunzi 150 ambao ni raia wa nchi hiyo. Serikali pia imesaini makubaliano ya ushirikiano katika matumizi ya Kiswahili na Serikali za Afrika Kusini, Namibia, Ethiopia na Misri.
Ndugu wanahabari, kukua kwa matumizi ya lugha ya Kiswahili katika nchi nyingine, jumuiya za kikanda na kimataifa ni fursa ya ajira kwa watanzania katika kada mbalimbali zikiwemo ualimu na ukalimani. Vilevile, matumizi ya lugha hiyo kimataifa yanatoa fursa ya kukuza na kuimarisha uhusiano wa kijamii na kiuchumi baina yetu na nchi nyingine.
Ndugu wanahabari, tunaposherekea maadhimisho ya miaka 60 ya uhuru, ninatoa rai kwenu kutumia taaluma yenu kukuza na kueneza matumizi ya lugha adhimu ya Kiswahili, ambayo pia ni urithi wetu, katika mataifa mengine duniani.
MAFANIKIO YA TANZANIA KIUCHUMI KUPITIA UHUSIANO WA KIMATAIFA
Ndugu wanahabari, Tanzania imepata mafanikio ya kiuchumi kupitia uhusiano baina yake na nchi nyingine, jumuiya za kikanda na mashirika ya kimataifa. Uhusiano wa kiuchumi kati ya Tanzania na nchi nyingine unatokana na uwepo wa mikataba na makubaliano ya ushirikiano katika sekta mbalimbali za kijamii na kiuchumi. Mathalan, kupitia makubaliano ya ushirikiano katika biashara baina ya Tanzania na nchi za Oman, Qatar, Kuwait na Saudi Arabia, nchi yetu inauza mbogamboga, nyama na bidhaa za nyama katika masoko ya nchi hizo. Kadhalika, kupitia makubaliano ya hivi karibuni ya biashara kati ya Tanzania na China, kampuni 72 za kitanzania zimepata ithibati kutoka katika mamlaka za China kuuza maharage ya soya katika soko la nchi hiyo ambapo zaidi ya tani 120 za bidhaa hiyo tayari zimeuzwa nchini humo. 16
Ndugu wanahabari, kupitia ushirikiano wa kiuchumi kati ya Tanzania na washirika wa maendeleo wanaojumuisha nchi na taasisi, Serikali imepokea misaada na mikopo yenye masharti nafuu kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo. Mfano, Serikali ya India ilitoa mkopo wa masharti nafuu wenye thamani ya Dola za Marekani milioni 500 kwa ajili ya kutekeleza miradi ya kusambaza maji katika miji mbalimbali hapa nchini. Vilevile, Serikali ya Kuwait kupitia Mfuko wa Maendeleo wa Kuwait (Kuwait Fund) ilitoa mkopo wa masharti nafuu wenye thamani ya Shilingi bilioni 117 kwa ajili ya ujenzi wa barabara ya Chaya-Nyahua yenye urefu wa kilometa 85.4 mkoani Tabora, ambayo ujenzi wake umekamilika mwezi Machi 2021. Mfuko huo pia umefadhili mradi wa kilimo cha umwagiliaji katika Bonde la Mto Luiche lenye ukubwa wa ekari 3,000 mkoani Kigoma.
Kadhalika, Tanzania na Umoja wa Ulaya (EU) zilisaini mikataba 6 ya msaada yenye thamani ya Shilingi bilioni 307.9 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika sekta za nishati, kilimo na uhifadhi wa mazingira.
Ndugu wanahabari, ni wazi kuwa, mifano niliyotaja ni michache ikilinganishwa na historia ndefu iliyopo ya ushirikiano kati ya Tanzania na washirika wa maendeleo, ambao umeisaidia Serikali kutekeleza miradi na program za maendeleo kwa lengo la kupunguza umaskini na kuongeza ustawi wa wananchi. Serikali inazishukuru nchi na taasisi washirika wa maendeleo kwa michango yao ya kifedha na utaalam. Aidha, Serikali ya Awamu ya Sita inaahidi kuendeleza na kukuza ushirikiano huo.
Ndugu wanahabari, vilevile, Tanzania ni mwanachama katika jumuiya za mtangamano wa kikanda, ambapo kupitia uanachama wake imenufaika na makubaliano ya kuondoleana vikwazo vya kiforodha na visivyo vya kiforodha katika biashara ya bidhaa na huduma. Mathalan, kupitia utekelezaji wa Itifaki ya Umoja wa Forodha ya Afrika Mashariki (EAC) na Eneo Huru la Biashara la SADC, bidhaa za Tanzania zinauzwa katika nchi wanachama wa EAC na SADC bila kutozwa ushuru wa forodha. Serikali imeendelea kuwawezesha wafanyabiashara kunufaika na fursa za biashara katika mtangamano wa kikanda kwa kutoa vyeti vya uasili wa bidhaa ambavyo vinawasaidia kupata unafuu wa 17
kodi kwa kutolipa ushuru wa forodha kwa bidhaa zinazozalishwa nchini na zinazokidhi vigezo vya uasili wa bidhaa vya jumuiya hizo.
Kutokana na fursa hiyo, mauzo ya Tanzania katika jumuiya za EAC na SADC yamekuwa yakiongezeka na kuinufaisha nchi yetu kwa fedha za kigeni pamoja na ajira. Pia, kupitia utekelezaji wa Itifaki ya Soko la Pamoja la Afrika Mashariki, Tanzania imenufaika na mitaji, ujuzi na uhawilishaji wa teknolojia baina yake na nchi nyingine wanachama wa EAC. Kupitia utekelezaji wa itifaki hiyo, Watanzania wanaweza kupata ajira au kuanzisha biashara katika mojawapo ya nchi za EAC bila kubaguliwa na vivyo hivyo raia kutoka nchi nyingine za jumuiya wanaweza kupata ajira na kuwekeza nchini.
Ndugu wanahabari, Tanzania pia inanufaika na utekelezaji wa miradi ya maendeleo ya kikanda katika sekta mbalimbali kama vile miundombinu ya usafirishaji, nishati, maji, afya na elimu. Miongoni mwa miradi iliyotekelezwa nchini kupitia ushirikiano wa kikanda ni Mradi wa Maji na Usafi wa Mazingira katika Ziwa Victoria unaotekelezwa kupitia EAC katika Wilaya za Geita na Sengerema; Mradi wa Ujenzi wa Kituo cha Kufua Umeme cha Rusumo (MW 80), unaotekelezwa kwa ubia baina ya Tanzania, Rwanda na Burundi; Mradi wa Ujenzi wa Barabara ya Bagamoyo-Tanga-Horohoro/Lungalunga-Malindi (Km 425) kati ya Tanzania na Kenya. Utekelezaji wa miradi hiyo, pamoja na kuimarisha mtangamano wa kiuchumi, pia inasaidia kuboresha ustawi wa wananchi na kufungua fursa za kiuchumi na kijamii.
Ndugu wanahabari, katika kipindi cha miaka 60 ya uhuru wa Tanzania Bara, nchi yetu imekuwa mstari wa mbele katika kupigania haki na usawa wa kiuchumi duniani kupitia majukwaa ya kimataifa kwa kupaza sauti na kushawishi mageuzi katika taasisi na mashirika ya kimataifa kama vile Shirika la Biashara Duniani. Dhamira ya Tanzania ni kutaka kuwepo kwa mazingira sawa ya kiuchumi duniani yatakayoziwezesha nchi zinazoendelea kustawi kiuchumi kupunguza pengo lililopo kati yao na nchi zilizoendelea. Vilevile, Tanzania imeshiriki kikamilifu katika kutekeleza program za maendeleo chini ya Umoja wa Mataifa ambazo zimekuwa na manufaa ya kiuchumi na kijamii. 18
MCHANGO WA WATANZANIA WANAOISHI NJE YA NCHI (DIASPORA)
Ndugu Wanahabari, kwa kutambua mchango wa Watanzania wanaoishi nje ya nchi (Diaspora), mnamo mwaka 2010 Serikali ilianzisha Kitengo cha Diaspora chini ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwa ajili ya kuratibu masuala yote yanayohusu Diaspora. Vilevile, Serikali imeendelea kuweka mazingira wezeshi yatakayochochea ushiriki wa Diaspora katika shughuli za maendeleo kwa kuchangia rasilimali fedha (mitaji), elimu, ujuzi na teknolojia. Vilevile, Diaspora ni kiungo muhimu cha kuitangaza nchi yetu kimataifa na kuhamasisha uwekezaji kutoka nje.
Ndugu Wanahabari, mchango wa Diaspora katika Taifa letu umeendelea kukua ambapo kwa mujibu wa takwimu za Benki Kuu ya Tanzania, fedha zinazoingizwa nchini na Diaspora (remittances) zimeongezeka kutoka Dola za Marekani milioni 465.7 mwaka 2016 hadi Dola za Marekani milioni 497.9 mwaka 2019. Vilevile, Diaspora wamekuwa wakichangia katika sekta za afya, elimu na huduma nyingine za kijamii. Mathalani, kati ya mwaka 2015 na 2019 Watanzania wanaoishi Marekani na Uingereza wamefanikisha ziara takribani tano za kitabibu zilizofanyika Tanzania Bara na Zanzibar. Aidha, Diaspora wamekuwa mstari wa mbele katika kuitangaza lugha adhimu ya Kiswahili ulimwenguni kupitia ufundishaji wa lugha hiyo katika nchi mbalimbali. Mathalani, takwimu zinaonesha kuwa kuna vituo takribani 30 vya ufundishaji wa lugha ya Kiswahili na Utamaduni wa Mtanzania vinavyomilikiwa na kuendeshwa na Diaspora katika nchi za Afrika Kusini, Misri, Malawi, Uingereza, Zimbabwe, Ubelgiji, Comoro, Jamhuri ya Korea, Ufaransa na China.
MAFANIKIO YA TANZANIA KATIKA MASUALA MENGINE MTAMBUKA YA KIMATAIFA
Ndugu wanahabari, Tanzania inajivunia miaka 60 ya kushiriki kikamilifu katika kutekeleza masuala mengine mtambuka ya kimataifa yakiwemo jinsia; uhifadhi wa mazingira na mapambano dhidi ya mabadiliko ya tabianchi; haki za binadamu na utawala bora; na mapambano dhidi ya rushwa, makosa yanayovuka mipaka (mfano biashara 19
haramu ya usafirishaji wa binadamu na dawa za kulevya). Katika miongo sita ya uhuru, nchi yetu imesaini na kuridhia mikataba ya kimataifa inayohusu utekelezaji wa masuala hayo mtambuka, hivyo kujijengea heshima na kutambulika na jumuiya ya kimataifa kwa mchango wake.
Ndugu wanahabari, Serikali imetenga eneo lenye ukubwa wa kilometa za mraba 400,000 kama eneo tengefu sawa na asilimia 37 ya eneo lote la nchi kavu. Vilevile, Tanzania ni mshirika wa Itifaki ya Kyoto kuhusu Mapambano Dhidi ya Mabadiliko ya Tabianchi ya mwaka 1997, ambapo kwa kudhihirisha uthabiti wake na dhamira yake katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ilishiriki kikamilifu katika Mkutano wa 26 wa Nchi Wanachama wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi (COP26) uliofanyika mwezi Oktoba 2021 jijini Glasgow, Scotland. Kupitia mkutano huo, nchi yetu iliungana na nchi nyingine duniani kuzitaka nchi vinara wa uchafuzi wa mazingira kutekeleza kwa vitendo makubaliano ya kupunguza kiwango cha hewa ukaa wanachozalisha. Vilevile, Tanzania kwa kinywa kipana ilizitaka nchi zilizoendelea kutimiza ahadi zao za kuzisaidia nchi zinazoendelea kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
Ndugu wanahabari, Tanzania imepiga hatua katika utekelezaji wa masuala ya jinsia ambapo Serikali za awamu zote zimekuwa zikitoa kipaumbele kwa watu wa jinsia zote kushika nyadhifa za uongozi na maamuzi bila kujali kigezo cha jinsia. Hilo linajidhihirisha hivi sasa ambapo nafasi ya juu ya uongozi katika Serikali inashikiliwa na mwanamke, hatua ambayo imeifanya Tanzania kuwa miongoni mwa nchi chache barani Afrika na nchi pekee katika Ukanda wa Mashariki mwa Afrika kuwa na kiongozi mkuu wa Serikali mwanamke. Aidha, kama nilivyoeleza awali wanawake wameshika nyadhifa za juu za uongozi na maamuzi katika mashirika ya kimataifa ambapo utumishi wao ni wa kutukuka, wenye tija na sifa kwa nchi yetu kimataifa.
Ndugu Wanahabari, Tanzania ni mwanachama wa Mpango wa Hiari wa Kujitathmini Kiutawala Bora wa Umoja wa Afrika (APRM). Vilevile, kupitia majukwaa ya kikanda na kimataifa Tanzania imeshiriki kikamilifu kushawishi na kusisitiza masuala ya utawala 20
bora. Serikali ya Tanzania pia imeendelea kuaminika kimataifa kwa kuheshimu haki za binadamu, utawala wa sheria na demokrasia kutokana na kutekeleza sera, sheria, mipango, mikakati, program na miradi inayolenga kuongeza ustawi wa wananchi na kupunguza umaskini pamoja na kutoa uhuru wa kushiriki katika shughuli za kijamii na kiuchumi.
Ndugu wanahabari, kadhalika, nchi yetu imekuwa mstari wa mbele katika mapambano dhidi ya rushwa na aina nyingine za uhalifu zikiwemo uharamia, utakasishaji wa fedha, ugaidi, usafirishaji haramu wa binadamu na dawa za kulevya, kupitia utekelezaji wa makubaliano baina yake na nchi nyingine, jumuiya za kikanda na kimataifa. Kama kielelezo cha ushiriki thabiti wa Tanzania katika mapambano dhidi ya uhalifu wa kimataifa, nchi yetu ni mwenyeji wa Kituo cha Kupambana na Ugaidi cha SADC. Jitihada hizo zimeipatia nchi yetu sifa nzuri na kutambulika kimataifa kama mshirika thabiti katika kupiga vita aina zote za uhalifu.
Ndugu wanahabari, Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, itaendelea kuheshimu makubaliano ya kimataifa kwa kutekeleza sera, mipango, mikakati, program na miradi inayohusu masuala hayo mtambuka.
HITIMISHO
Ndugu wanahabari, Serikali kupitia Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, itaendelea kutekeleza sera, mipango na mikakati yenye lengo la kudumisha na kuendeleza mafanikio yaliyopatikana katika kipindi cha miaka 60 ya Uhuru wa Tanzania Bara katika uhusiano wa kimataifa. Baadhi ya malengo ya Serikali katika kipindi kijacho ni kukuza sauti ya Tanzania katika jumuiya za kikanda na kimataifa; kushiriki kikamilifu katika mikutano ya kikanda na kimataifa na kulipa michango yake ya uanachama; na kuendelea kuchangia juhudi za kulinda amani na usalama duniani na kutetea haki na usawa kwa kupinga mifumo kandamizi ya kiuchumi na kisiasa duniani.
Vilevile, Serikali itaendelea kuweka mazingira wezeshi kwa sekta binafsi nchini kuongeza ushiriki wake katika masuala ya kimataifa; kuweka mazingira wezeshi kwa Diaspora kuendelea kutoa mchango wao katika maendeleo ya Taifa; na kuendelea kuziwezesha Balozi zetu nje kutekeleza kikamilifu majukumu yake hususani diplomasia ya uchumi.
Ndugu Wanahabari, baada ya kusema hayo, ninawashukuru sana kwa mwitikio wenu, na ni matarajio yangu kuwa mtatumia vyombo vyenu vya habari kueneza taarifa ya mafanikio ya Serikali kupitia Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki katika kipindi cha miaka 60 ya uhuru kwa Wananchi na dunia kwa ujumla.
Ndugu Wanahabari, nimalizie kwa kuwasilimu tena kwa Jina la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania……Kazi iendelee!!!
Asanteni kwa kunisikiliza.