Wakuu wa Nchi EAC- SADC wajadili hali ya Usalama Nchini DRC
Wakuu wa Nchi na Serikali wa Nchi Wanachama wa Jamuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) wamefanya mkutano wa dharura wa pamoja (EAC-SADC Joint Extra-Ordinary Summit) kwa njia ya mtandao tarehe 13 Agosti 2025.
Kwa upande wa Tanzania Makamu wa Rais Mhe. Dkt. Philip Mpango aliongoza ujumbe wa Tanzania akimwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan katika mkutano huo uliofanyika kwenye ukumbi wa Benki Kuu ya Tanzania jijini Arusha.
Mkutano huo ulioongozwa na Wenyeviti Wenza Rais wa Jamhuri ya Kenya na Mwenyekiti wa EAC Mheshimiwa Dkt. William Ruto na Rais wa Jamhuri ya Zimbabwe Mheshimiwa Dkt. Emmerson Mnangagwa umeangazia hali ya utelekezaji wa masuala mbalimbali yaliyokubaliwa kwenye mikutano ya awali ya pamoja, yaliyolenga kurejesha hali ya amani na usalama katika eneo la Mashariki mwa DRC.
Masuala hayo ni pamoja na kujadili namna ya kuunganisha michakato ya kutafuta amani mashariki mwa DRC chini ya EAC na SADC kuwa mchakato mmoja utakao ratibiwa na kusimamiwa na Umoja wa Afrika.
Pia, mkutano huo umeridhia na kupongeza uteuzi wa Rais Mstaafu wa Botswana Mhe. Mokgweetsi Masisi wa kujiunga katika Jopo la Wanachama Wawezeshaji wa juhudi za kutafuta amani Mashariki mwa DRC, uliofanywa na mkutano wa pamoja wa EAC na SADC uliofanyika terehe 1 Agosti 2025 jijini Nairobi.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti wakati wa ufunguzi wa mkutano huo Wenyeviti Wenza Mheshimiwa Dkt. William Ruto na Mheshimiwa Dkt. Emmerson Mnangagwa na Katibu Mtendaji wa SADC Mhe. Elias Magosi wameeleza kuguswa na kutambua juhudi zinazoendelea kufanywa na wadau mbalimbali katika kutafuta suluhu ya kudumu Mashariki mwa DRC. Hata hivyo, viongozi hao wameazimia kuendeleza juhudi za uratibu na kuwezesha mikakati ya upatikanaji wa misaada ya kibinadamu kwa ajili ya kuwasaidia raia walioathiriwa na mgogoro unaoendelea Mashariki mwa DRC.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango katika mkutano huo aliambatana na Manaibu Wiziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Cosato Chumi na Mhe. Dennis Londo (anayesimamia masuala ya Afrika Mashariki), Katibu Mkuu, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki anayesimamia masuala ya Afrika Mashariki Balozi Stephen P. Mbundi, Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Said Shaib Mussa na Watendaji wengine Serikali.