Skip to main content
News and Events

Mkutano wa 27 wa Kamati ya Mawaziri ya SADC ya Masuala ya Siasa, Ulinzi na Usalama Waanza

Mkutano wa 27 wa Kamati ya Mawaziri wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) ya Masuala ya Siasa, Ulinzi na Usalama (MCO) unaofanyika nchini tarehe 21-25 Julai,2025 umeanza katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam.

Akifungua mkutano huo kwa Ngazi ya Maafisa Waandamizi, Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt. Samwel Shelukindo, amesema nchi wanachama wa SADC hazina budi kuzingatia umoja, mshikamano, na uratibu wa kimkakati katika kukabiliana na changamoto za kiusalama na mabadiliko ya kijiografia ya kisiasa, ili kuimarisha amani, usalama, na uthabiti wa muda mrefu wa kanda.

“Ni muhimu tuimarishe uratibu na ushirikiano katika ngazi ya kikanda, bara, na kimataifa ili juhudi zetu ziwe na ufanisi, zisigharimu sana, ziratibiwe vizuri, na ziwe za kimkakati; kwani njia zisizoratibiwa zinaweza kudhoofisha mafanikio yaliyopatikana chini ya mipango kama Mpango Elekezi wa Maendeleo ya Kanda (RISDP) na Dira ya Maendeleo ya SADC ya mwaka 2050” Alifafanua Balozi Shelukindo.

Balozi Shelukindo amepongeza mafanikio yaliyopatikana katika Mkutano wa Kwanza wa Pamoja wa Wakuu wa Nchi wa SADC na EAC uliofanyika Dar es Salaam, kwa lengo la kuunganisha juhudi za amani Mashariki mwa DRC kupitia michakato ya Luanda na Nairobi.

Amesema hatua hiyo ni dalili ya matumaini ya kupatikana kwa suluhisho la pamoja la kisiasa na kidiplomasia, huku akisisitiza umuhimu wa mshikamano wa kikanda katika kukabiliana na changamoto kama uhalifu wa kimataifa uliopangwa, uhalifu wa mtandaoni, usafirishaji haramu wa binadamu na biashara ya dawa za kulevya, ambazo alisema zinaweza kudhoofisha juhudi za maendeleo na kutishia dira ya pamoja ya SADC endapo hazitashughulikiwa ipasavyo.

Mkutano wa MCO unafanyika nchini kwa kuwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni Mwenyekiti wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya SADC kwa kipindi cha mwaka mmoja kuanzia Agosti 2024 hadi Agosti 2025 baada ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, kuteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Asasi hiyo katika Mkutano uliofanyika mwaka 2024 nchini Zimbabwe.

Mkutano wa 27 wa MCO utaongozwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo ambaye ni Mwenyekiti wa Mkutano huo utakaofanyika tarehe 24 na 25 Julai 2025.