Skip to main content
News and Events

YAJUE MANUFAA YA MAKUBALIANO YALIYOSAINIWA KATI YA TANZANIA NA KOREA

Tanzania na Jamhuri ya Korea zimesaini Mkataba, Tamko na Hati za Makubaliano (MoUs) zenye manufaa makubwa kwa maendeleo ya kiuchumi kwa wananchi wa pande zote mbili.

Hati hizo zimesainiwa Juni 02,2024 mbele ya Marais, Mhe. Samia Suluhu Hassan na Mhe. Yoon Suk Yeol baada ya kukamilika mazungumzo rasmi ya viongozi hao yaliyofanyika Ikulu jijini Seoul.

Rais Samia yupo nchini Korea ikiwa ni mwendelezo wa ziara zake za kimkakati za kutafuta fursa za uwekezaji, biashara, utalii na teknolojia, na utiaji saini wa makubaliano hayo ni ishara njema za kutimiza malengo ya Serikali yake ya kukuza na kuboresha hali ya maisha ya wananchi.

Makubaliano hayo yametiwa saini na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba (Mb) na Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb) kwa niaba ya Serikali ya Tanzania. Kwa upande wa Korea yamewekwa saini na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Uchumi na Fedha, Mhe. Choi Sang Mok; Waziri wa Uvuvi na masuala ya Bahari, Mhe. KANG, Do-Hyung na Waziri wa Biashara, Mhe. Inkyo Cheong.

Maukubaliano yaliyosainiwa yanahusu mkopo wa hadi Dola za Marekani bilioni 2.5 unaotolewa kwa Tanzania na Mfuko wa Ushirikiano wa Maendeleo ya Uchumi wa Serikali ya Korea (Economic Development Cooperation Fund-EDCF) kwa ajili ya miradi ya maendeleo kwa kipindi cha kuanzia mwaka 2024 hadi 2028; ushirikiano katika kuendeleza Uchumi wa Buluu; Tamko la Pamoja kuhusu Uanzishwaji wa Majadiliano juu ya Mkataba wa Ushirikiano wa Kiuchumi (EPA); na ushirikiano katika kuendeleza madini ya kimkakati.

Manufaa ambayo Tanzania inatarajia kuyapata kupitia makubaliano hayo ni pamoja na kupokea mkopo nafuu wa Dola za Marekani bilioni 2.5 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika sekta ya miundombinu, elimu na afya. Mkopo huo una riba ya aasilimia 0.01 na unalipwa kwa miaka 40 na utaanza kulipwa baada ya miaka 15 (15 years grace period).

Aidha, Tanzania kupitia ushirikino wa Uchumi wa Buluu itajengewa uwezo na kupewa teknolojia ya kufanya utafiti wa Rasilimali zake zinazopatikana majini ikiwa ni pamoja na msaada katika ujenzi wa bandari za uvuvi.