Waziri Kombo afungua mkutano wa 27 wa MCO ya SADC
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Thabit Mhamoud Kombo, amefungua Mkutano wa 27 wa Kamati ya Mawaziri wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) ya Masuala ya Siasa, Ulinzi na Usalama (MCO), katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere, jijini Dar Es Salaam.
Mhe. Kombo ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati hiyo amesema mkutano huo unajadili na kutathmini hali ya usalama, mafanikio na maendeleo ya kisiasa na kijamii, utekelezaji wa maamuzi ya vikao vilivyopita, pamoja na mikakati ya kuimarisha taasisi na mifumo ya usalama wa kikanda.
“Tunapotathmini mafanikio yaliyopatikana, tuendelee kuongozwa na misingi ya mshikamano, ushirikiano wa pamoja, na tukubali kuwajibika kwa dhati kwa mujibu wa Mkataba wa SADC na Dira ya 2050. Nina imani kuwa kupitia majadiliano yetu, tutajizatiti upya na kuthibitisha nafasi ya SADC kama kinara wa amani, umoja, na mchakato wa kuunganisha bara la Afrika” alifafanua Mhe. Kombo.
Amesema dhamira ya SADC ni kuendelea kudumisha amani na utulivu kupitia usuluhishi wa migogoro, kuimarisha mifumo ya tahadhari za mapema, pamoja na kushirikisha makundi maalum kama wanawake na vijana katika juhudi za upatanishi.
Mwenyekiti huyo wa MCO pia amezisihi nchi wanachama wa SADC kudumisha mshikamano, ushirikiano na uwajibikaji ili kuendelea kuleta mafanikio makubwa ya kanda, huku akiwataka Mawaziri kuendeleza maono ya waasisi wa jumuiya hiyo, kwa kulifanya eneo la kusini mwa Afrika kuwa Kitovu cha Amani, Maendeleo na Umoja Barani Afrika.
Mhe. Kombo pia alisema Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inatarajia kufanya uchaguzi wake mkuu mwezi Oktoba 2025, na kuukaribisha Ujumbe wa Waangalizi wa SADC -SEOM kuja kushuhudia uchaguzi huo na ametoa salam za kheri kwa Jamhuri za Malawi na Seychelles, ambazo zinatarajia kufanya uchaguzi mkuu mwezi Septemba 2025.
Kuhusu mapambano dhidi ya Rushwa, Mhe Kombo amesema SADC imeanza kutekeleza mkakati wa kupambana na rushwa kwa kuanzisha Kielelezo cha Juhudi za Kupambana na Rushwa, ambacho tayari kimejaribiwa katika nchi mbili wanachama ambazo ni Jamhuri ya Mauritius na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, na kuonesha mafanikio makubwa.
Naye Katibu Mtendaji wa SADC Mhe. Elias Magosi amezisihi nchi wanachama kutekeleza majukumu yao sambamba na utekelezaji wa sera na mipango muhimu inayolenga kuimarisha amani, utulivu, na utawala bora katika ukanda wa SADC.
“Katika dira yetu ya kuleta mshikamano wa kanda na maendeleo endelevu, dhamira yetu kuu ni kuhakikisha amani na usalama vinadumu,” alisema Mhe. Magosi