WAZIRI KOMBO ASISITIZA USHIRIKIANO KATIKA KUTEKELEZA MIKAKATI YA KIKANDA – SADC
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo (Mb.) ameahidi kushirikiana na Baraza la Mawaziri wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) katika kukuza uchumi wa kanda.
Hayo yamejiri wakati akichangia mada katika Mkutano wa Mawaziri wa SADC unaofanyika nchini Zimbabwe kuanzia tarehe 13 hadi 16 Agosti, 2024 ambapo, Mhe. Kombo anashiriki mkutano huo kwa mara ya kwanza tangu aapishwe na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kushika wadhifa wa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.
‘’Naahidi kushirikiana nanyi katika kutekeleza mikakati ya kikanda kama ilivyoainishwa katika Mkataba wa Uanzishwaji wa SADC na Mpango Mkakati wa Maendeleo wa Kanda (RISDP) wa mwaka 2020-2030’’ alisema Waziri Kombo.
Aidha, Waziri Kombo ameeleza kwamba Tanzania itaendelea kushiriki kikamilifu katika shughuli za Jumuiya ikiwa ni pamoja na ulipaji wa michango yake ili kuyafikia malengo ya kanda hiyo.
Mkutano wa Mawaziri wa SADC pia umefanya makabidhiano ya nafasi ya mwenyekiti wa Baraza hilo ambapo mwenyekiti wa sasa wa Baraza la Mawaziri wa SADC na Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Angola, Mhe. Balozi Tete António amekabidhi nafasi hiyo kwa Waziri wa Mambo ya Nje na Biashara ya Kimataifa wa Jamhuri ya Zimbabwe, Mhe. Balozi Dkt. Fredrick Shava.
Wakati wa makabidhiano hayo Mhe, Tete António amempongeza Mhe. Shava kwa kupokea majukumu hayo na pia amesisitiza juu ya umuhimu wa kuondolewa vikwazo vya kiuchumi ilivyowekewa Zimbabwe, ushirikishwaji wa wanawake katika maamuzi mbalimbali ya kijamii, kiuchumi na kisiasa na ushirikishwaji wa vijana katika shughuli za maendeleo.