Skip to main content
News and Events

WADAU WA UTALII WATAKIWA KUTUMIA TEKNOLOJIA KUTANGAZA UTALII

Wadau wa Utalii watakiwa kutumia ubunifu zaidi katika kutangaza vivutio vya utalii wa ndani ili kukuza sekta ya utalii na kuongezea pato la taifa.

Wito huo umetolewa na Mkurugenzi wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mindi Kasiga alipotoa salamu za Wizara katika Kongamano la Wiki ya Ubunifu Tanzania 2022 lililofanyika leo Jijini Dar es Salaam.

“Kuna mambo yanayojitokeza katika mazingira ya sasa kwenye sekta ya utalii ambayo ni muhimu sana kuhusisha ubunifu wa teknolojia katika kutangaza vivutio vya utalii,” alisema Balozi Kasiga .

Balozi Kasiga ameeleza kuwa haiwezekani kuendelea kutangaza utalii kwa njia tulizokuwa tunatumia zamani, ndiyo maana wabunifu wa teknolojia wametuonesha mchango wa teknolojia katika kutangaza vivutio vya utalii na sasa tunaona Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan amejadiliwa sana kutokana na kutangaza uzinduzi wa filamu ya ‘Royal Tour’ ambayo imeelezea kwa undani vivutio vya utalii nchini kwa teknolojia ya juu zaidi.

Pamoja na mambo mengine, Balozi Mindi amewasihi wabunifu kuendelea kutumia teknolojia kutangaza vivutio mbalimbali vya utalii vilivyopo nchini. 

Kupitia kongamano hilo washiriki wamejadili namna  ubunifu na teknolojia vinaweza kutumika kama njia mbadala ya kutangaza vivutio vya utalii na kuwavutia watanzania waweze kutembelea vivutio hivyo. 

Aidha, kupitia Kongamano la Wiki ya Ubunifu Tanzania 2022, teknolojia ya ‘Safari Wallet’ imezinduliwa na kijana wa Kitanzania ambapo inapatikana katika tovuti ya ‘Safari Wallet’ na inatumika kuwasaidia wadau wa utalii kuchagua sehemu za kutembelea kwa urahisi na haraka zaidi vivutio vya utalii nchini

Balozi Kasiga ameeleza kuwa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki itajitahidi kuiwasilisha teknolojia ya ‘safari wallet’ katika nyanja za kimataifa ikiwemo ukanda wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Ukanda wa Nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) na mataifa mengine ili kuweza kutangaza zaidi vivutio vya utalii nchini.

Naye Naibu Balozi wa Uholanzi nchini, Mhe. Job Runhaar amesema teknolojia ni nyenzo muhimu katika kutangaza sekta ya utalii nchini.

Sisi kama wadau wa teknolojia tumefurahishwa sana na uzinduzi wa teknolojia ya Safari Wallet. Teknolojia hii ikitumika vizuri  kutangaza vivutio vya utalii itasaidia  kuchangia ongezeko la mapato ya serikali na maendeleo ya wabunifu kwa ujumla,” amesema Mhe. Runhaar  

Kongamano la ubunifu limeandaliwa na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kupitia Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) linaloendelea katika wiki ya Ubunifu lililozinduliwa Mei 10, 2022 Jijini Dar es Salaam ambapo wadau wa ubunifu walipata nafasi ya kujadili masuala yanayohusu ubunifu na hatua wanazochukua kuendeleza sekta ya ubunifu ili kuwa na tija kwa Watanzania.

  • Naibu Balozi wa Uholanzi nchini, Mhe. Job Runhaar akiongea na washiriki wa Kongamano la Wiki ya Ubunifu Tanzania 2022 (hawapo pichani) Jijini Dar es Salaam
  • Mkurugenzi wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mindi Kasiga akiongea na waandishi wa Habari katika Kongamano la Wiki ya Ubunifu Tanzania 2022
  • Baadhi ya wanajopo walioshiriki Kongamano la Wiki ya Ubunifu Tanzania 2022