Skip to main content
News and Events

UGANDA YAZINDUA UJENZI WA OFISI YA UBALOZI JIJINI DODOMA

Serikali ya Jamhuri ya Uganda imezindua mradi wa ujenzi wa jengo la Ofisi ya Ubalozi wake ambao utekelezaji wake umeshaanza kufanyika katika mjini wa Serikali Mtumba, jijini Dodoma. 

Akizungumza kwenye hafla ya uzinduzi wa mradi wa ujenzi huo uliofanyika leo Mei 9,2025, Balozi wa Uganda nchini Tanzania Mhe. Kanali Fred Mwesigye ameeleza kuwa ujenzi huo haumaanishi tu kuwa na jengo la kuhudumia wananchi bali ni kituo muhimu cha kuimarisha na kukuza zaidi uhusiano wa kiuchumi na kidiplomasia baina ya Tanzania na Uganda.

Aliendelea kueleza kuwa Tanzania na Uganda ni ndugu na daima zimeendelea kushirikiana katika masuala mbalimbali ya uwili na kimataifa. Hivyo Uganda inaona fahari kutumia fursa hiyo kuwa nchi ya kwanza kuanzisha ujenzi wa Ofisi ya Ubalozi ikiwa ni sehemu ya kutoa shukrani zake kwa Serikali ya Tanzania kwa mchango mkubwa iliyotoa katika ujenzi wa Taifa la Uganda, na mkono maamuzi ya Serikali ya Tanzania ya kuhamia jijini Dodoma. 

Balozi Mwesigye ametoa rai kwa Balozi zingine zinazowakilisha nchini zao hapa nchini kuiga mfano huo, huku akiitaka Kampuni iliyopewa kandarasi ya kutekeleza mradi huo kumaliza kwa wakati, viwango na gharama zilizokubaliwa. 

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki anaye shughulikia masuala ya Afrika Mashariki Mhe. Dennis Londo ambaye alikuwa mgeni rasmi katika hafla ya ufunguzi wa mradi ujenzi huo akimwakilisha Waziri Mhe. Balozi Mahmoud Thabiti Kombo ametoa pongezi kwa Serikali ya Uganda kwa kuweka historia ya kuwa nchi ya kwanza kuanzisha ujenzi wa Ofisi ya Ubalozi katika Mji Mkuu wa Serikali jijini Dodoma. 

Naibu Waziri Londo alieleza kuwa uzinduzi wa ujenzi huo ambao unatarajiwa kukamilia ni kielelezo cha ushirikiano na uhusiano mzuri uliopo baina ya Uganda na Tanzania uliojikita sio tu katika misingi na historia ujirani mwema bali undugu. 

Kadhalika Naibu Waziri Londo, ametumia fursa hiyo kuzihimiza Balozi zingine zilipo nchini kuhamishia Ofisi zao jijini Dodoma, kwa kuwa Serikali tayari imeshaweka mazingira rafiki na wezeshi ya kuwawezesha kutekeleza majukumu yao vyema wakiwa jijini hapo. Ametaja baadhi ya hatua zilizochukuliwa na Serikali katika kuboresha mazingira hayo ikiwa ni pamoja upatikanaji wa huduma bora na muhimu za kijamii, kama vile afya na shule, na ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Msalato unaotarajiwa kukamilika hivi karibuni. 

Naye Mkuu wa Mkoa wa jijini la Dodoma ambaye pia alihudhuria hafla hiyo Mhe. Rosemary Senyamule amewahakikishia jumuiya ya wanadiplomasia nchini kuwa Jiji hilo lipo tayari kuwapokea na miundombinu muhimu za kijamii ikwemo maji, elimu, afya na usafirishaji, inaendelea kujengwa na kuboreshwa zaidi. 

Viongozi wengine waliohudhuria hafla hiyo ni pamoja na Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu)Mhe. Ummy Nderiananga; Mkuu wa Itifaki wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Uganda Balozi Charles Ssentongo, Mkurugenzi Idara ya Utawala na Usimamizi Raslimali Watu katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Bi. Chiku Kiguhe na viongozi wengine Waandamizi wa Serikali. 

  • Naibu Waziri wa Mambo yan Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki anayeshughulikia masuala ya Afrika Mashariki Mhe. Dennis Londo akifungua hafla Ujenzi wa Ofisi za Ubalozi wa Uganda, katika Mji wa Serikali Mtumba jijini Dodoma
Downloads File:
  • 3 [6 MB]