Skip to main content
News and Events

TANZANIA NA JAPAN ZAAHIDI KUENDELEA KUDUMISHA USHIRIKIANO

Tanzania na Japan zimeahidi kuendelea kushirikiana na kudumisha ushirikiano uliopo kati ya nchi hizo mbili.

Ahadi hiyo imetolewa wakati wa kikao kati ya Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Cosato Chumi (Mb.) na Balozi wa Japan nchini Mhe. Yusushi Misawa kilichofanyika katika Ofisi Ndogo za Wizara jijiji Dar es Salaam tarehe 07 Agosti 2024.

Akizungumza kwenye kikao hicho, Mhe. Chumi ameishukuru serikali ya Japan kwa kuwa mstari wa mbele katika kuchangia maendeleo ya Tanzania na nchi nyingine za Afrika kwa ujumla.

Ameongeza kuwa, Tanzania itashiriki kikamilifu kwenye Mkutano wa Tisa wa Ngazi ya Mawaziri wa Ushirikiano kati ya Japan na Afrika (TICAD 9) unaotarajiwa kufanyika jijini Tokyo, Japan kuanzia tarehe 22 hadi 25 Agosti 2024.

Naye Balozi wa Japan nchini Mhe. Misawa ameishukuru Serikali ya Tanzania kwa kuwa mshirika wa karibu wa Japan kwa manufaa ya pande zote.

Kadhalika, ameishukuru Serikali ya Tanzania kwa kukubali kushiriki Mkutano wa Tisa wa TICAD ambao utakutanisha Mawaziri kutoka nchi 47 za Bara la Afrika.

Viongozi hao hao pia wamejadili masuala mbalimbali ya ushirikiano uliopo kati ya mataifa hayo rafiki kwa kipindi cha miongo sita iliyopita.

Serikali ya Japan imekuwa mdau muhimu wa kuchangia maendeleo ya Tanzania kupitia sekta mbalimbali kama vile miundombinu, afya, maji, biashara na uwekezaji.

Ushirikiano wa Tanzania na Japan ulianza tangu mwaka 1961.