Skip to main content
News and Events

Tanzania na Finland kuimarisha Ushirikiano katika Usimamizi wa Amani na Usuluhishi wa migogoro

Rais wa Jamhuri ya Finland, Mhe. Alexander Stubb amesema Serikali ya Finland itaendelea kuimarisha ushirikiano na Tanzania ili kuhakikisha juhudi za pamoja zinatekelezwa katika usimamizi wa amani na usuluhishi wa migogoro Barani Afrika na duniani kwa ujumla. 

Mhe. Rais Stubb ameyasema hayo Mei 15, 2025 wakati akifungua semina ya kuenzi mchango wa Rais wa zamani wa Jamhuri ya Finland, Hayati Martti Ahtisaari katika kuleta amani na upatanishi duniani, iliyofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam.

Mhe. Rais Stubb amesema kuwa, Hayati Martti Ahtisaari ni hazina na mwongozo kwa dunia ya leo, kwani aliifuindisha Dunia kuwa amani ni kitu kinachowezekana, kama watatuzi wa amani watakuwa tayari kusikilizana na kushirikiana kwa dhati.

“Hayati Ahtisaari, alijulikana kwa juhudi zake za kusuluhisha migogoro katika nchi za Kosovo, Namibia, na jimbo la Aceh nchini Indonesia, ambapo alitumia njia ya mazungumzo na maridhiano, katika kuleta usuluhu endelevu kwenye maeneo yaliyoathirika na migogoro ya muda mrefu” alifafanua Mhe. Rais Stubb.

Awali, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mahmoud Thabit Kombo (Mb.), ameishukuru Finland kwa ushirikiano na mchango wake katika miradi ya maendeleo nchini na ufadhili wa program mbalimbali katika Taasisi ya Uongozi na Kituo cha Uhusiano wa Kimataifa cha Dkt. Salim Ahamed Salim, hatua ambayo imeimarisha utekelezaji wa majukumu ya taasisi hizo katika ngazi ya Kitaifa na Kimataifa.

Kuhusu mchango wa Finland katika kukuza amani na utatuzi wa migogoro Waziri Kombo amesisitiza, Tanzania itaendelea kuwa mstari wa mbele katika juhudi za kutafuta amani, huku ikizingatia falsafa nne ambazo ni, Maridhiano, Ustahimilivu, Mageuzi na Kujenga upya taifa (4R), zilizoanzishwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ili kujenga jamii zenye mshikamano na amani ya kudumu.

“Kwa Tanzania, Hayati Rais Ahtisaari ni mtu wa kipekee kwetu, aliishi nasi na kushiriki nasi katika kumbukumbu nyingi nzuri tangu mwaka 1973, alipochaguliwa kuwa Balozi wa Finland hapa Tanzania. Urafiki wake wa muda mrefu na marehemu Rais Benjamin William Mkapa unakumbusha kuwa alikuwa na uhusiano wa kipekee na Watanzania” Mhe. Kombo alieleza.

Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Shirika la Kutetea Amani la Martti Ahtisaari, Bw. Marko Ahtisaari, amesema kuimarika kwa uhusiano wa kidiplomasia kati ya Tanzania na Jamhuri ya Finland kunatokana na msingi imara uliowekwa na viongozi waasisi wa mataifa hayo, akiwemo Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, Hayati Benjamin Mkapa na Hayati Martti Ahtisaari, ambao wamewezesha nchi hizo kukuza maeneo ya ushirikiano kwa manufaa ya wananchi wa pande zote mbili.