TANZANIA NA DRC ZAKUTANA DAR KUJADILI BIASHARA NA UWEKEZAJI
Katibu Mkuu, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Joseph Sokoine ameelezea matumaini yake kuwa Mkutano wa Tatu wa Tume ya Kudumu ya Pamoja ya Ushirikiano (JPC) kati ya Tanzania na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) utajadili na kukubaliana maeneo ya ushirikiano ambayo yatakuwa na tija ya moja kwa moja kwa nchi hizo na watu wake.
Balozi Sokoine amesema hayo leo tarehe 12 Septemba 2022 jijini Dar Es Salaam wakati akisoma hotuba ya ufunguzi ya Mkutano huo wa siku tatu ulioanza katika ngazi ya wataalamu na utahitimishwa kwa ngazi ya Mawaziri tarehe 14 Septemba 2022.
DRC ambaye ni mwanachama mpya wa Jumuiya ya Afrika Mashariki imekuwa ikishirikiana na Tanzania katika kuendeleza sekta mbalimbali kama vile; miundombinu, nishati, utalii, elimu, afya, huduma za kifedha, biashara, uwekezaji, kilimo, maliasili na ufugaji. Nchi hizo pia zinashirikiana na kuungana mkono kwenye masuala ya kikanda na kimataifa yenye maslahi kwa pande zote mbili.
Katibu Mkuu amewataka wajumbe wa pande zote mbili kuhakikisha kuwa wanatumia mkutano huo kuweka mikakati na mazingira mazuri yatakayofanya mataifa hayo mawili yenye rasilimali lukuki, yanakuwa kitovu cha biashara, utalii na uwekezaji kwa wafanyabiashara na wananchi kwa ujumla.
“Wajumbe tumieni mkutano huu wa JPC kujadili namna ya kuondoa changamoto zinazokwamisha utekelezaji wa maeneo tunayokubaliana na kuweka mazingira wezeshi ili sekta za umma na binafsi ziweze kuwekeza kwa ajili ya kujiletea maendeleo endelevu na kuinua pato la nchi zote mbili”, Balozi Sokoine alisisitiza.
Naye, Katibu Mkuu wa Wizara ya Mtangamano wa Kikanda na Nchi zinazongumza Kifaransa wa DRC, Mhe. Zacharie Tshimbinda Bilolo amesisitiza umuhimu wa wajumbe wa pande zote mbili kuja na mikakati inayotekelezeka itakayoiwezesha nchi hizi mbili kupiga hatua za maendeleo.
Mkutano huu wa JPC kati ya Tanzania na DRC ni watatu na unafanyika baada ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan kufanya ziara ya kitaifa nchini DRC mwezi Agosti 2022. Mkutano wa mwisho wa JPC baina ya nchi hizi mbili ulifanyika mwaka 2002.
Mkurugenzi wa Afrika katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Naimi Aziz akiwakaribisha Makatibu Wakuu wa Tanzania na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Balozi Joseph Sokoine na Mhe. Zacharie Tshimbinda Bilolo kusoma hotuba za ufunguzi za Mkutano wa Tatu wa Tume ya Kudumu ya Pamoja ya Ushirikiano kati ya Tanzania na DRC.
Sehemu ya Ujumbe wa DRC unaoshiriki Mkutano wa Tatu wa Tume ya Kudumu ya Pamoja ya Ushirikiano kati ya Tanzania na DRC.
Mkurugenzi wa Afrika katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Naimi Aziz akifafanua jambo kwa viongozi kuhusu Mkutano wa Tatu wa Tume ya Kudumu ya Pamoja ya Ushirikiano kati ya Tanzania na DRC.
Katibu Mkuu, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Joseph Sokoine na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mtangamano wa Kikanda na Nchi zinazongumza Kifaransa wa DRC, Mhe. Zacharie Tshimbinda Bilolo wakiwa katika picha ya pamoja na wajumbe wa Tanzania na DRC wanaoshiriki Mkutano wa Tatu wa Tume ya Kudumu ya Pamoja ya Ushirikiano kati ya Tanzania na DRC
Mkutano wa Tatu wa Tume ya Kudumu ya Pamoja ya Ushirikiano kati ya Tanzania na DRC ngazi ya wataalam unaendelea jijini Dar Es Salaam