Skip to main content
Press Release

Taarifa kuhusu ziara ya Rais wa Zimbabwe nchini

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Taarifa kuhusu ziara ya Rais wa Zimbabwe nchini Mheshimiwa Emmerson Dambudzo Mnangagwa, Rais wa Jamhuri ya Zimbabwe atafanya ziara ya kitaifa nchini Tanzania tarehe 28 hadi 29 Juni, 2018. Hii itakuwa ziara ya kwanza ya Mheshimiwa Rais Mnangagwa nchini Tanzania tangu aingie madarakani mwezi Novemba, 2017.

Lengo la ziara hii ya Rais wa Zimbabwe ni kujitambulisha kwa Rais na wananchi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Tangu aingie madarakani, Mheshimiwa Rais Mnangagwa ameshafanya ziara katika nchi za Namibia, Zambia, Msumbiji, Angola, Afrika Kusini, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Botswana.

Ziara hii ni muhimu kwa Tanzania kwani itatoa fursa ya kuimarisha na kukuza zaidi mahusiano mazuri yaliyopo ya kidiplomasia, kihistoria, kiuchumi na kijamii kati ya nchi hizi mbili. Ziara hii pia itatoa fursa kwa viongozi wetu kujadili masuala mbalimbali yanayohusu nchi hizi mbili ya kikanda na kimataifa.

Wakati wa ziara hiyo, Mhe. Rais Mnangagwa atafanya mazungumzo rasmi na mwenyeji wake Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli. Rais Mnangagwa anatarajiwa pia kutembelea Chuo cha Sanaa cha Kaole Bagamoyo ambacho awali kilitumika kutoa mafunzo kwa wapigania uhuru kutoka nchi za Kusini mwa Bara la Afrika na Mhe. Rais Mnangagwa ni miongoni mwa waliopata mafunzo katika chuo hicho. Mhe. Rais Mnangagwa anatarajiwa kuondoka tarehe 29 Juni 2018 kurejea chini Zimbabwe.

-Mwisho-

Imetolewa na:

Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,

Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,

Dar es Salaam, 27 Juni, 2018

Downloads File: