Skip to main content
News and Events

SEKRETARIETI YA AfCFTA YATOA ELIMU KUHUSU MKATABA WA AfCFTA

Sekretarieti ya Mkataba wa Eneo Huru la Biashara barani Afrika (AfCFTA) limeendesha Warsha ya kujenga uelewa wa pamoja kuhusu Mkataba huo kwa Wabunge na Wajumbe wa Baraza Wawakilishi ili kuwa na uelewa wa pamoja na kuutekeleza kwa ufanisi. 

Akifungua warsha hiyo mjini Zanzibar, Waziri wa Biashara na Maendeleo ya Viwanda Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Mhe. Omar Said Shabaan amesema uelewa wa pamoja kuhusu mkataba huo ni  muhimu kwakuwa utaiwezesha nchi kuutekeleza kwa vitendo na hivyo kunufaika na malengo ya kuanzishwa kwake.

"Kutekeleza mkataba huu lazima kuwe na uelewa wa pamoja, hii itawezesha nchi kujipanga na kwenda pamoja kuutekeleza na hivyo kunufaisha nchi kwa ujumla wake," alisema mhe. Omar

Amesema uelewa wa pamoja wa Mkataba huo wa AfCFTA kutawezesha nchi kupata tija iliyokusudiwa wakati nchi ilipoamua kuuridhia na kusaini na hivyo kuwa miongoni mwa watekelezaji wake.

Amesema Serikali zote mbilii za Muungano na ile ya Mapinduzi Zanzibar zimeufanyia tathmini Mkataba huo na kuja na mkakati maalum wa kusaidia utekelezaji wake

Amezitaka taasisi za uratibu wa mkataba huo kuendeleza juhudi za kuwezesha utekelezaji wa Mkataba huo ili kufahamu na kuzikamata fursa zinazopatikana katika soko la Mkataba huo ili kuutekeleza kwa ufanisi na hivyo kunufaika nao.

Amesema kama nchi haina budi kuangalia fursa za soko la AfCFTA ambalo litakuwa mbadala wa masoko mengine ambayo yana ukomo kutegemeana na nchi inavyokua kiuchumi.

Amesema kwa ukubwa wa soko la AfCFTA unaweza kuleta changamoto lna kueleza kuwa Serikali zimejipanga kukabiliana na changamoto za biashara kwa kuboresha mazingira ya kufanya biashara,  kuvutia wawekezaji na kuwafaanya wazalishaji wake wawe na uwezo wa kuzalisha bidhaa zenye viwango ili kufikia mahitaji ya bidhaa katika soko hilo la AfCFTA.

Amesisitiza kuwa utekelezaji wa Mkataba wa AfCFTA utapelekea ukuaji wa biashara, uwekezaji na uzalishaji wa bidhaa bora kwa nchi na hivyo kama nchi lazima itilie mkazo ili kunufaika na soko hilo.

Warsha hiyo inayoendeshwa na Sekretariati ya AfCFTA yenye makao yake makuu mjini Accra ,Ghana ililenga kutoa elimu na mahitaji ya Mkataba wa AfCFTA ambao Tanzania kupitia Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania iliuridhia na kuusaini mwezi Septemba 2021.

Tanzania iliwasilisha Hati ya kuuridhia Mkataba huo kwa Kamisheni ya Afrika jijini Addis Ababa, Ethiopia mwezi Februari ,2022 na hivyo kuwa miongoni mwa mataifa yanayotekeleza mkataba huo.

Mkataba wa AfCFTA ulianzishwa na Wakuu wa Nchi na Serikali za Umoja wa Afrika walipokutana katika kikao kilichofanyika jijiini  Kigali,  Rwanda  mwaka 2018.

  • Mwenyekiti wa Kamati ya Kilimo, Biashara na Utalii katika Baraza la Wawakilishi Zanzibar Mhe. Yussuf Hassan Iddi (katikati) akiwa na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji Dkt. Hashir Abdallah (kulia) Katibu Mkuu Wizara ya Uchumi wa Buluu na Uvuvi Dkt. Aboud S. Jumbe (kushoto) wakifuatilia ufunguzi wa Warsha ya pamoja ya Wabunge na Wajumbe wa Baraza Wawakilishi kuhusu utekelezaji wa Mkataba wa Eneo Huru la Biashara barani Afrika (AfCFTA) iliyofanyika Zanzibar.
  • Waziri wa Biashara na Maendeleo ya Viwanda Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Mhe. Omar Said Shabaan akifungua Warsha ya pamoja ya Wabunge na Wajumbe wa Baraza Wawakilishi ili kuwa na uelewa wa pamoja na kutekeleza kwa ufanisi Mkataba wa Eneo Huru la Biashara barani Afrika (AfCFTA) iliyofanyika Zanzibar.