Rais Samia ampongeza Rais wa Comoro, kwa uongozi safi na wenye maono katika kuleta maendeleo ya wananchi
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassa amempongeza Rais wa Umoja wa Visiwa vya Comoro, Mhe. Azali Assoumani kwa uongozi safi na wenye maono katika kuleta maendeleo ya wananchi wake.
Rais Samia ametoa pongezi hizo leo tarehe 06 Julai, 2025 katika Uwanja wa Mlouzini Omnisport, mjini Moroni, wakati akihutubia Wananchi, katika Sherehe za maadhimisho ya miaka 50 ya uhuru wa Comoro.
Amesema tangu Rais Asoumani aingie madarakani amefanya jitihada kubwa za kuimarisha uchumi, miundombinu ya usafiri, kilimo, nishati, umeme, na huduma za kijamii ikiwemo ujenzi wa hospitali, ili kukidhi mahitaji ya wananchi na kuleta Maendeleo.
Aidha, amewasihi wananchi wa Comoro kuheshimu mambo muhimu walioachiwa na mababu na mabibi zao, na kuyatumia maadili hayo katika kujiletea maendeleo kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.
Rais Samia pia amesema sambamba na juhudi za Kimataifa, Tanzania itaendelea kushirikiana kwa karibu na Serikali ya Comoro, katika kukabiliana na changamoto zinazoikabili dunia hususan, athari za mabadiliko ya tabianchi.
Kwa upande wake, Rais wa Comoro, Mheshimiwa Azali Assoumani, amemshukuru Rais Samia, kwa kukubali kuwa mgeni rasmi katika sherehe hizo, pamoja na mchango mkubwa wa Tanzania katika kuimarisha uhusiano wa kindugu na kukuza diplomasia ya uchumi na nchi yake.
Sherehe hizo zilihudhuriwa na Marais kutoka nchi za Tanzania, Ethiopia, Mauritius na Comoro, Wakuu wa vyombo vya Ulinzi na Usalama, Maspika wa Mabunge mbalimbali, Viongozi wa Serikali, wawakilishi wa sekta binafsi, mashirika yasiyo ya kiserikali, na washirika wa maendeleo.