RAIS NYUSI AWEKA JIWE LA MSINGI HOSPITALI YA RUFAA YA KANDA - CHATO

Rais wa Msumbiji, Mhe. Filipe Jacinto Nyusi amewasili nchini leo kwa ziara ya kikazi na kupokelewa na mwenyeji wake Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli katika uwanja wa ndege wa Geita - Chato na kisha kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa hospitali ya Rufaa ya Kanda- Chato.

Akizungunza katika hafla hiyo ya uwekaji wa jiwe la msingi la ujenzi wa hospitali ya Rufaa ya Kanda-Chato, Rais Magufuli alimshukuru Rais Mhe. Filipe Nyusi kwa kumtembelea  Chato na kuongeza  kuwa  Msumbiji ni rafiki wa muda mrefu wa Tanzania na nchi hizo  zina makubaliano ya kushirikiana katika mambo mbalimbali ikiwemo biashara na uwekezaji.

"Biashara kati ya Tanzania na Msumbiji imeongezeka, hadi kufikia mwaka 2020 ilifikia shilingi bilioni 93.6, kuna makampuni ya Msumbiji yanafanya kazi hapa na baadhi ya makampuni ya Tanzania yanafanya kazi kule." Amesema Rais Magufuli.

Rais Magufuli ameongeza kuwa Januari 9, 1967 Hayati Mwalimu Julius Nyerere alitembelea Wilaya ya Chato na kufungua kiwanda cha pamba kilichojengwa kwa shilingi milioni 2 ambacho kilikuwa na uwezo wa kuchakata marobota 20,000. 

Aidha, Rais Magufuli amesema kuwa Mwalimu Nyerere alichangisha fedha na yeye binafsi kuchangia shilingi 2,000 kwa ajili ya kujenga bandari ya Nyamirembe ili iweze kusafirisha pamba kwenda Mwanza na Dar es Salaam kwa hiyo wa Rais Nyusi amefika eneo ambalo alifika Mwalimu Nyerere.

"Kwetu sisi tunaona hii ni zawadi kubwa kwa wewe kuja kuzindua hospitali hii ambayo ni kubwa na itahudumia pia nchi za jirani.Nawashukuru Wizara ya Afya na Wakandarasi, nitawabana Wizara ya Afya  ili hospitali hii ikamilike mara moja." Alisema Rais Magufuli

Kwa upande wake Rais Nyusi amempongeza Rais Magufuli kwa juhudim kubwa za kushughulikia maisha ya wananchi wa Tanzania kwa kuendelea kuboresha sekta pamoja na huduma za afya nchini.

"Nashukuru kwa Rais Magufuli kunipa nafasi ya kuweka jiwe la msingi kwa sababu Serikali inayoaangalia afya za wananchi hiyo ni Serikali inayopenda wananchi wake. Rais Magufuli anashughulikia sana maisha ya wananchi wa watanzania kwa kuangalia nyumba bora za kuishi, huduma za maji, chakula  na afya bora" amesema Rais Nyusi.

"Kwa hiyo hii ni zawadi kwetu  kwa kutupa nafasi ya kuweka jiwe la msingi katika hospitali hii kubwa, kule Msumbiji tumeanza (Program ya  presidential initiatives) ya kujenga hospitali kila wilaya hii ni zawadi kubwa kwetu ya  kutupa nafasi ya kuweka jiwe la msingi  katika afya ya wananchi," Ameongeza Rais Nyusi

Aidha, Rais Nyusi amesema kuwa mkoa wa Geita  ni tajiri kwa kuwa kuna kilimo cha mpunga,  madini ya dhahabu na uvuvi wa  samaki, hivyo kuwataka wananchi wa mkoa huo kufanyakazi kwa bidii.

Naye, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dkt. Dorothy Gwajima amesema kuwa awamu ya kwanza ya ujenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda - Chato ilikadiriwa kutumia sh. bil.16, Serikali imeshatoa sh. bil.14 ambapo ujenzi umekamilika kwa asilimia 90 na makabidhiano yanatarajiwa kufanyika mwezi Machi, 2021.

Ameongeza kuwa awamu ya pili ya ujenzi  imeshaanza kwa jumla ya gharama ya shilingi bilioni 14 ambapo mpaka sasa Serikali imetoa shilingi bilioni 4.1 na utekelezaji wake umefikia asilimia 37.

"Hospitali ya Rufaa ya Kanda - Chato itakapokamilika itakuwa na uwezo wa kuhudumia wananchi zaidi ya milioni 14 ambapo kwa siku itakuwa na uwezo wa kuhudumia wagonjwa kati ya 700 - 1000." Amesema Dkt. Gwajima

Rais wa Msumbiji, Filipe Jacinto Nyusi yupo nchini kwa ziara ya siku moja ambapo atafanya mazungumzo na Rais Magufuli kuhusu namna ya kuboresha maisha  wananchi wetu  pamoja na usalama.

  • Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Pombe Joseph Magufuli akiteta jambo na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb) muda mfupi kabla ya Rais wa Msumbiji, Mhe. Filipe Nyusi kuwasili katika uwanjRais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Pombe Joseph Magufuli akiteta jambo na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb) muda mfupi kabla ya Rais wa Msumbiji, Mhe. Filipe Nyusi kuwasili katika uwanj