NGORONGORO YAIKUTANASHA SERIKALI NA MABALOZI, WAKUU WA MASHIRIKA YA KIMATAIFA NA WADAU WA MAENDELEO

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula akiongea na Mabalozi, Wakuu wa Mashirika ya Kimataifa na Wadau wa Maendeleo (hawapo pichani) Jijini Dar es Salaam

NGORONGORO YAIKUTANASHA SERIKALI NA MABALOZI, WAKUU WA MASHIRIKA YA KIMATAIFA NA WADAU WA MAENDELEO

*Yasema inazingatia Haki za Binadamu na kuwawezesha wale watakaoondoka kwa hiyari katika maeneo hayo

Serikali imesema haitamzuia mtu yeyote anayetaka kuondoka kwa hiyari katika eneo la Ngorongoro kwenda kuishi popote nchini na kuwataka wadau wengine kutowazuia wanaotaka kuondoka katika eneo hilo.

Waziri wa Maliasili na Utalii Dkt. Damasi Ndumbaro ameyasema hayo Jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na Mabalozi, Wakuu wa Mashirika ya Kimataifa na Wadau wa Maendeleo kuhusu mpango wa serikali wa kutafuta suluhu ya kudumu katika eneo la Ngorongoro na Loliondo na kuongeza kuwa itawawezesha wale wote wanaotaka kuondoka kwa hiyari katika maeneo hayo.

Dkt. Ndumbaro amewaeleza Mabalozi hao kuwa mpaka sasa jumla ya kaya 164 sawa na watu 915 wamejiandikisha kuondoka Ngorongoro kwa hiyari na kwenda kuishi katika maeneo mbadala watakayopewa na Serikali ikiwa ni pamoja na kuwajengea nyumba ama kuwalipa fidia.

Waziri Ndumbaro ameongeza kuwa Serikali imeamua kuchukua hatua hiyo ili kuzipatia ufumbuzi changamoto zilizojitokeza katika eneo la Ngorongoro ikiwa ni kuongeza kwa binadamu kutoka 8000 mwaka 1959 hadi kufikia 110,000 kwa sasa ikiambatana na ongezeko la mifugo kutoka mifugo 200,000 mwaka 1959 hadi kufikia mifugo 1,000,000 kwa sasa jambo linaloathiri ikolojia na uhifadhi, maendeleo ya utalii na maendeleo ya jamii ya wanaoishi Ngorongoro.

Kwa upande wake Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula akiwa ameambatana na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Balozi Fatma Rajabu amesema dhumuni la kuwaita Mabalozi hao pamoja na Wakuu wa Mashirika ya Kimataifa ni katika jitihada zinazofanywa na Serikali kuhakikisha Mabalozi na wadau wa Maendeleo wanapata taarifa sahihi kuhusu suala la Ngorongoro na Loliondo kutokana na kugubikwa na upotoshaji.

Ameongeza kuwa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki imeweka utaratibu wa kuzikutanisha Wizara za kisekta na  Mabalozi, Wakuu wa Masharika ya Kimataifa na Wadau wa Maendeleo mara moja kila baada ya miezi 3 lengo likiwa ni kutoa fursa kwa Serikali kutoa ufafanuzi wa masuala mtambuka ya serikali na kuruhusu majadiliano yanayosaidia wadau hao kuwa na taarifa sahihi pamoja na kuwa na uelewa wa pamoja.

Akichangia mjadala huo, Balozi wa Ujerumani nchini, Mhe. Regina Hess ameunga mkono jitihada za Serikali za kulinda uhifadhi na mazingira katika eneo la Ngorongoro ili kukabiliana na athari zinazotokana na mabadiliko ya tabia nchi.

  • Waziri wa Maliasili na Utalii Dkt. Damasi Ndumbaro akiongea na Mabalozi, Wakuu wa Mashirika ya Kimataifa na Wadau wa Maendeleo (hawapo pichani) Jijini Dar es Salaam
  • Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Fatma Rajab akiongea na Mabalozi, Wakuu wa Mashirika ya Kimataifa na Wadau wa Maendeleo Jijini Dar es Salaam