NAIBU WAZIRI MHE. COSATO CHUMI APOKEA NAKALA ZA HATI ZA UTAMBULISHO KUTOKA KWA MABALOZI WATEULE WA IRELAND, JAMAICA, MALI, MEXICO, GUINEA NA ROMANIA
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. David Cosato Chumi (MB.) amepokea nakala za Hati za Utambulisho kutoka kwa Mabalozi Wateule wa Matifa Sita katika tukio lililofanyika kwenye ofisi ndogo zaWizara jijini Dar Es Salaam Agosti 11, 2024. Mabalozi hao ni Balozi wa Ireland, Mhe. Nicola Brennan; Balozi Mteule wa Jamaica, Mhe. Joan Thomas Edwards; Balozi Mteule wa Mexico, Mhe. Enrique Ochoa Martίnez; Balozi Mteule wa Guinea, Mhe. Nounke Kaba; Balozi Mteule wa Romania, Mhe. Gentiana Serbu na Balozi Mteule wa Mali, Mhe. Dkt. Madou Diallo.
Akipokea nakala za Hati hizo za Utambulisho, Mhe. Chumi amewapongeza Mabalozi hao Wateule kwa kuaminiwa na kupewa jukumu la kuziwakilisha nchi zao hapa nchini Tanzania. Mhe. Chumi amewakaribisha Mabalozi hao Wateule na kuahidi kuwa Serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki itatoa ushirikiano wa karibu katika kipindi chote watakachokuwa nchini ili waweze kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi.
Aidha, amewaarifu kuwa Mabalozi hao wamepangiwa kuwasilisha hati zao kwa Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambapo Balozi wa Ireland atawasilisha tarehe 12 Agosti 2024 wakati Balozi wa Jamaica, Mexico, Guinea, Romania, na Mali watawasilisha tarehe 13 Agosti 2024.
Akiongea na Balozi wa Ireland, Mhe. Chumi ameishukuru Serikali ya Ireland kwa kuendelea kuwa mdau muhimu wa maendeleo kwa nchi yetu kwa kuisaidia Tanzania kutekeleza miradi mbalimbali katika sekta ya Afya, Kilimo, Elimu, Uzalishaji na Jinsia. Ireland imekuwa ikitoa msaada mkubwa pia kwa Tanzania kwa kuipatia misaada ya kifedha na kuchangia katika bajeti kuu ya Serikali yetu. Balozi huyo ameahidi kuwa ataendeleza yale mazuri yote yaliyopo na kuibua masuala mapya kwa maslahi ya pande zote. Nae, Balozi wa Romania ameahidi kuwa watashirikiana kwa karibu na Serikali ya Tanzania katika kutekeleza miradi ya elimu na usalama wa mitandao.