BUNGE LAPITISHA BAJETI YA WIZARA KWA MWAKA WA FEDHA 2025/2026
Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania limepitisha kwa kishindo makadirio ya bajeti ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026 ya Shilingi 340,538,614,000 ambapo kati ya fedha hizo shilingi 294,998,588,000 ni kwa ajili ya Matumizi ya Kawaida na shilingi 45,540,026,000 ni kwa ajili ya Bajeti ya Maendeleo.
Maombi ya Makadirio ya Bajeti ya Wizara yaliwasilishwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo (Mb.) ambapo Bunge limepitisha na kuipongeza Wizara kwa jinsi ilivvyotekeleza majukumu yake kwa kipindi cha mwaka wa fedha 2024/2025 na ilivyojipanga kutekeleza majukumu yake ikiwemo Sera ya Mambo ya Nje ya Mwaka 2001, Toleo la Mwaka 2024 kwa mwaka wa fedha 2025/2026.
Akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara kwa mwaka wa fedha 2025/2026 Mhe. Balozi Kombo aliwaeleza Wabunge kuwa Wizara, katika kipindi cha mwaka wa fedha 2024/2025 imefanikisha kwa kiasi kikubwa kutekeleza majukumu yake ya msingi ikiwemo kusimamia na kutetea maslahi ya Tanzania nje ya nchi pamoja na kukamilisha mapitio ya Sera ya Mambo ya Nje ya Mwaka 2001, Toleo la Mwaka 2024 iliyozinduliwa rasmi na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan tarehe 19 Mei 2025.
Mhe. Waziri Kombo amesema kuwa, Sera hiyo pamoja na mambo mengine inaweka msisitizo katika utekelezaji wa diplomasia ya uchumi ikiwemo kukuza upatikanaji wa masoko ya bidhaa za Tanzania nje ya nchi, kutangaza na kuvutia fursa za uwekezaji, utalii, uchumi wa buluu, kuhamasisha ushiriki wa Diaspora katika maendeleo ya Taifa na kutumia Kiswahili kama nyenzo ya diplomasia kwa manufaa ya kiuchumi.
Pia amesema Sera hiyo Sera hii imeweka msingi mpya wa kulinda mila, desturi na utamaduni wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambapo pia alitumia nafasi hiyo kutoa rai kwa Wizara, Taasisi, Idara zinazojitegemea, Sekretarieti za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa kujumuisha malengo ya Sera ya Mambo ya Nje, Toleo la Mwaka 2024 katika mipango na programu zao.
“Napenda kutoa rai kwa Wizara, Taasisi, Idara zinazojitegemea, Sekretarieti za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa kujumuisha malengo ya Sera ya Mambo ya Nje, Toleo la Mwaka 2024 katika mipango na programu zao kama ilivyoainishwa katika Mkakati wa utekelezaji ili kuwezesha Taifa letu kunufaika ipasavyo", alisisitiza Mhe. Waziri Kombo.
Aidha, Mhe. Waziri Kombo amesisitiza kuwa Tanzania itaendelea kuwa mstari wa mbele katika utatuzi wa migogoro kwa njia ya amani pamoja na kushiriki katika operesheni za kulinda amani kikanda na kimataifa ambapo amesema hadi kufikia Mei, 2025 Tanzania ilikuwa na jumla ya walinda amani 1,890 ikiwa nafasi ya 11 kati ya nchi 119 zinazochangia walinda amani katika misheni za ulinzi wa amani za Umoja wa Mataifa.
Kuhusu Tume za pamoja, Mhe. Waziri Kombo amebainisha kuwa, takribani mikutano Arobaini na Mbili (42) ya Tume za Pamoja za Kudumu za Ushirikiano (JPC) kati ya Tanzania na nchi mbalimbali , Tume za Pamoja za Ushirikiano (JCC) na mashauriano ya kisiasa kati ya Tanzania na nchi nyingine. Mikutano hiyo imewezesha Serikali yetu kutetea maslahi ya Taifa na nchi hizo katika maeneo mbalimbali ya ushirikiano kwa manufaa ya Taifa letu.
Akizungumzia masuala ya Diaspora, Mhe. Waziri Kombo amesema Wizara imeendelea kuratibu na kuhamasisha ushiriki wa diaspora katika shughuli za kiuchumi, kielimu na kijamii hapa nchini kwa namna mbalimbali ikiwemo kuwaunganisha na taasisi mbalimbali nchini ili waweze kupata huduma na bidhaa zinazorahisisha ushiriki wao katika maendeleo ya Taifa ambapo amesema kwa mwaka 2024 diaspora waliwekeza kiasi cha shilingi 7,500,000,000ikilinganishwa na shilingi 6,400,000,000 mwaka 2023 katika Mfuko wa Uwekezaji wa Pamoja wa UTT-AMIS.
“Takwimu za Benki Kuu ya Tanzania (BoT) zinaonesha kuwa katika kipindi cha kuanzia Julai hadi Desemba 2024 fedha zinazotumwa na Diaspora kuja nyumbani ni shilingi 2,116,188,355,632.06 ukilinganisha na shilingi 2,045,855,200,000 kwa kipindi cha mwaka 2023. Kiasi hicho kina mchango mkubwa katika kuboresha maisha ya familia zao, kusaidia uwekezaji na kuchangia ukuaji wa sekta ya fedha nchini”alieleza Mhe. Waziri Kombo.
Vile vile, hotuba ya Bajeti ya Mhe. Waziri Kombo imeainisha vipaumbele vya Wizara kwa mwaka wa fedha 2025/2025 ikiwemo kuendelea kuimarisha uratibu na ushirikiano wa uwili pamoja na ushiriki wa Tanzania katika jumuiya na mashirika ya kikanda na kimataifa ili kulinda maslahi ya taifa; pamoja na kustawisha diplomasia ya kisiasa na kujenga mahusiano ya karibu na nchi washirika.