Skip to main content
News and Events

BALOZI SIRRO AWASILISHA HATI ZA UTAMBULISHO KWA RAIS WA JAMHURI YA MAURITIUS

Balozi wa Tanzania nchini Mauritius mwenye makazi yake nchini Zimbabwe, Mhe. Simon Nyakoro  Sirro amewasilisha Hati za Utambulisho kwa Rais wa Jamhuri ya Mauritius Mhe. Prithvirajsing  ROOPUN, G.C.S.K katika Ikulu ya nchi hiyo jijini Port Louis, Mauritius tarehe 16 Oktoba, 2024.

Aidha, Mhe. Balozi Sirro alipata wasaa wa kufanya mazungumzo na  Mheshimiwa Rais Prithvirajsing  ROOPUN, G.C.S.K ambapo aliwasilisha  salaam za  Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,  Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Mazungumzo hayo pamoja na masuala mengine pia, yalilenga kuimarisha ushirikiano kati ya Tanzania na Mauritius hususan katika utekelezaji wa Sera ya  Diplomasia ya Uchumi, ukamilishaji wa mikataba mbalimbali  ikiwemo  Mkataba wa Kutotoza Kodi Mara Mbili na Mkataba wa Kubadilishana Wafungwa .

Naye, Mhe. Rais Prithvirajsing  ROOPUN, G.C.S.K alimhakikishia Mhe. Sirro Ushirikiano katika utekelezaji wa majukumu yake pamoja na kuelezea kuwa ni wakati wa nchi hizi mbili kufungua milango zaidi ya ushirikiano hususan katika sekta ya uchumi, biashara, uwekezaji na usafiri.