BALOZI SHAIBU AKUTANA KWA MAZUNGUMZO NA MWAKILISHI WA HESHIMA WA TANZANIA NCHINI SINGAPORE
Mhe. Balozi Said Shaib Mussa, Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki amekutana na kufanya mazungumzo na Bw. Teo Siong Seng, Mwakilishi wa Heshima wa Tanzania nchini Singapore jijini Dar es Salaam tarehe 14 Novemba,2024. Bw. Teo pia ni Mwenyekiti wa Kampuni ya Usafirishaji Pacific International Lines (PIL) iliyopo Singapore.
Katika mazungumzo hayo, mbali na kupongeza kazi nzuri inayofanywa na Bw. Teo Siong Seng katika kuchochea na kuimarisha ushirikiano kati ya Tanzania na Singapore, vilevile, Mhe. Naibu Katibu Mkuu Balozi Shaibu amemtaka mwakilishi huyo wa heshima kutumia umashuhuri wake nchini Singapore kuimarisha uhusiano na ushirikiano kati ya Tanzania na Singapore katika Sekta mbalimbali na kuchochea utekelezaji wa Diplomasia ya Uchumi.
Amemtaka Bw. Teo kuendelea kuhamasisha wawekezaji kutoka Singapore kuja nchini Tanzania pamoja na kutafuta fursa za masoko, mafunzo na kujenga uwezo kwa watanzania.