WIZARA YA MAMBO YA NJE YAJIVUNIA KUIMARIKA KWA DIPLOMASIA, MIAKA 60 YA MUUNGANO
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk (Mb.) ametaja mafanikio ya Wizara katika kipindi cha miaka 60 ya Muungano wa Tanzania.
Mhe. Balozi Mbarouk ametaja mafanikio hayo jijini Dodoma Aprili 18, 2024 alipozungumza na waandishi wa habari kuelezea mafanikio ya Wizara katika kipindi cha miaka 60 ya Muungano wa Tanzania.
Balozi Mbarouk amesema Wizara inajivunia kuendelea kuimarika kwa ushirikiano na uhusiano kati ya Tanzania na nchi mbalimbali duniani na hivyo kupata mafanikio katika sekta mbalimbali kupitia ushirikiano wa uwili na ujirani mwema baina yake na mataifa mengine,
“Mafanikio haya yamepatikana kupitia ushirikiano uliopo ambao unatekelezwa kupitia taratibu maalum ikiwemo mikutano ya Tume za Ushirikiano wa Pamoja. Ushirikiano huu umeleta mafanikio kupitia kusainiwa Mikataba na Hati za Makubaliano (MoUs) ili kutekeleza maeneo mahsusi katika sekta mbalimbali za siasa, kiuchumi na kijamii,” alisema.
Amesema kupitia mikutano hiyo Tanzania imenufaika na kuongezeka kwa biashara na uwekezaji ambapo bidhaa za kilimo, mifugo, matunda na mbogamboga zimepata masoko katika nchi mbalimbali.
Amesema Tanzania imenufaika na fursa za mafunzo ya muda mrefu na mfupi yanayofadhiliwa na nchi mbalimbali ikiwemo Uingereza, Uturuki, Marekani, Misri, India, Indonesia, China, Hungary, Japan, New Zealand, Australia, Urusi, Ujerumani, Cuba, Korea, Yugoslavia, Uholanzi, Ubelgiji, Algeria, Sudan, Saudi Arabia, Thailand na Pakistan.
Amesema Tanzania imefanikiwa kuwa sehemu ya kuanzishwa kwa jumuiya za kikanda kama Umoja wa Afrika; Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), Jumuiya ya Afrika Mashariki na Jumuiya ya Nchi zilizo katika Maziwa Makuu (ICGLR) na kupitia uanachama katika jumuiya hizo Tanzania imetekeleza programu katika sekta mtangamano za siasa, ulinzi na Usalama; Miundombinu; Biashara, Viwanda, Fedha na Uwekezaji.
“Tanzania imekuwa sehemu ya utekelezaji wa dhana ya kutatua changamoto za kidunia kwa pamoja yaani Multilateralism, kuwa mbia anayeaminika na kukubalika katika maamuzi mbalimbali duniani hasa katika mashirika ya kimataifa hususan Umoja wa Mataifa na kuwa mbia kwenye vyombo mbalimbali ikiwemo Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa; Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa; Benki ya Dunia na Shirika la Biashara Duniani (WTO),” alisema.
Ameongeza kuwa Tanzania imekuwa sehemu ya maamuzi katika maeneo ya mazingira na mabadiliko ya tabia nchi; ulinzi na usalama; utatuzi wa migogoro; maendeleo endelevu na utafutaji rasilimali kwa ajili ya maendeleo ambapo kupitia jukwaa hilo imepata fursa ya kutoa misimamo yake kwa masuala muhimu ikiwemo mgogoro wa Isarel na Palestina na suala la Sahara Magharibi na kuwa sehemu ya kuunga mkono Sera ya Kutofungamana na Upande wowote (NAM) na kuunga mkono ajenda ya msimamo wa Kundi la 77 na China katika majukwaa ya Kimataifa kwa maslahi mapana ya Taifa.
Amesema Tanzania inajivunia mchango wake katika juhudi za kulinda Amani Duniani na hivyo kutekeleza malengo ya Sera Mpya ya Mambo ya Nje na moja ya malengo mahsusi ya Umoja wa mataifa.
Amesema pia Tanzania imekuwa ikishiriki kulinda Amani kupitia Misheni za Kikanda ikiwemo Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC); Umoja wa Afrika na Umoja wa Mataifa na baadhi ya maeneo ambayo Tanzania imechangia walinda amani ni pamoja na Lebanon; Darfur; Abyei; Liberia; Sudan Kusini; Sudan; DRC; Msumbiji na Afrika ya Kati na kuongeza kuwa Tanzania imeshiriki kikamilifu katika utatuzi wa migogoro kwa njia ya mazungumzo na diplomasia kwenye nchi na maeneo mbalimbali ikiwemo, Darfur; Cambodia; Sudan Kusini; Burundi na Kenya.
Amesema Tanzania kuwa mwenyeji wa Taasisi za Kimataifa kama ishara ya kuaminika na kukubalika na nchi nyingine. Tanzania imeendelea kufungua Balozi na Ofisi za Uwakilishi katika nchi mbalimbali za kimkakati ikiwa ni sehemu ya kuimarisha utekelezaji wa Sera ya Mambo ya Nje hususan Diplomasia ya Uchumi.
Amesema Serikali ya Awamu ya Sita imefungua Balozi mpya mbili za Vienna, Austria na Jakata, Indonesia na Konseli Kuu mbili za Lugumbashi na Guangzhou, China ambapo ufunguzi wa Balozi hizo unaifanya Tanzania kuwa na Balozi na Ofisi za Uwakilishi 45 na Konseli Kuu TANO huku ikiwa ni mwenyeji wa nchi na mashirika ya kimataifa zaidi ya 90 zikiwemo Konseli Kuu ambazo baadhi yake zipo Zanzibar kama vile China, Oman, India na Umoja wa Falme za Kiarabu.
Amesema Tanzania imefanikiwa kutoa viongozi mahiri kuongoza taasisi za kikanda na kimataifa ikiwa ni ishara ya kuaminiwa na mataifa mengine na kutaja baadhi ya nafasi hizo kuwa ni uteuzi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kuwa Mwenyekiti Mwenza wa Mkutano wa Kilele wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia Barani Afrika utakaofanyika Paris, Ufaransa mwezi Mei 2024.
Amesema Tanzania pia ilitoa Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa ambapo Dkt. Salim Ahmed Salim aliongoza Vikao Vinne vya Baraza hilo mwaka 1979 na 1980 na Dkt. Salim Ahmed Salim alihudumu kama Katibu Mkuu wa Umoja wa Afrika (OAU). Watanzania wengine ni Dkt. Asha-Rose Migiro kuwa Naibu Katibu Mkuu wa kwanza kutoka Afrika; Balozi Getrude Mongela kuwa Rais wa Bunge la Afrika; Dkt. Stergomena Tax kuwa katibu Mtendaji wa SADC; Balozi Juma Mwapachu katibu Mkuu wa EAC; Mhe. Balozi Liberata Mulamula (Mb.), Katibu Mtendaji wa Jumuiya ya Nchi za Ukanda wa Maziwa Makuu (ICGLR); Profesa Anna Tibaijuka kuwa Naibu Katibu Mkuu na Mkuu wa Shirika la Maendeleo ya Makazi la Umoja wa Mataifa (UN-HABITAT) na Mkuu wa Ofisi za Umoja wa Mataifa Nairobi (UNON), Bi. Joyce Msuya, Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP) na Spika wa Bunge la Tanzania Mhe. Dkt. Tulia Ackson (Mb.) kuchaguliwa kuwa Rais wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU). Dkt. Tulia ni mwanamke wa kwanza kutoka barani Afrika kushika wadhifa huo.
Amesema Tanzania imechangia katika juhudi za kubidhaisha Kiswahili ndani na nje ya nchi na kutoa ushawishi wa matumizi yake kama nyenzo ya diplomasia, usuluhishi wa migogoro; ukombozi na uhuru katika nchi za bara la Afrika.
Amesema Viongozi wa Tanzania katika awamu zote na sasa wakiongozwa na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, Makamu wa Rais, Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango; Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt Hussein Ali Mwinyi; Waziri Mkuu, Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa (Mb.), Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba (Mb.) wamekuwa wakifanya ziara za kimkakati katika nchi mbalimbali kwa lengo la kukuza na kuimarisha uhusiano baina ya Tanzania na nchi hizo.
Amesema Wakuu wa Nchi waliotembelea Tanzania katika miaka ya hivi karibun ni pamoja na: Rais wa Uganda, Mhe. Yoweri Kaguta Museveni; Rais wa Rwanda, Mhe. Paul Kagame; Rais wa Burundi, Mhe. Everiste Ndayishimiye; Rais wa DRC, Mhe. Felix Tshisekedi; Rais wa Msumbiji, Mhe. Fillipe Nyusi; Rais wa Zambia, Mhe. Hakainde Hichilema; Rais wa Malawi, Mhe. Lazarous Chakwera; Rais wa Poland, Mhe. Andrzej Duda; Rais wa Ujerumani, Mhe. Frank-Walter Steinmeier; Rais wa Romania, Mhe. Klaus Werner Iohannis; Rais wa Hungary, Mhe. Katalin Novak; Rais wa Indonesia, Mhe. Joko Widodo; Makamu wa Rais wa Marekani, Mhe. Kamala Harris; Makamu wa Rais wa Cuba, Mhe. Salvador Valdes Mesa; Waziri Mkuu wa Ethiopia, Mhe. Abiy Ahmed na Naibu Waziri Mkuu wa China Mhe. Liu Guozhong na Rais wa Kenya, Mhe. William Ruto.
Amesena Serikali imeimarisha ushiriki wa Watanzania waishio Nje ya Nchi na Raia wa Nchi nyingine Wenye Asili ya Tanzania katika maendeleo ya Taifa na kuchukua hatua za Kisera kwa kujumuisha masuala ya Diaspora katika mapitio ya Sera ya Mambo ya Nje ya Mwaka 2001 na imekamilisha mfumo wa kiditali wa kukusanya na kutunza taarifa za Diaspora ambapo mpaka sasa Diaspora wa Tanzania wapatao 1403 wamejiandikisha katika mfumo huo na hivyo kuiwezesha Serikali kupata takwimu sahihi za idadi ya Diaspora, mahali walipo, ujuzi na uzoefu walionao huku mfumo pia ukiwawezesha Diaspora kupata taarifa kuhusu fursa na huduma mbalimbali zinazotolewa na Serikali na sekta binafsi nchini.
Amesema Serikali iko katika hatua za kukamilisha kutoa Hadhi Maalum (Special Status) kwa Raia wa Nchi Nyingine Wenye Asili ya Tanzania ili kuwezesha kuchangia ipasavyo katika maendeleo ya Taifa.