Skip to main content
News and Events

WIZARA KUSHIRIKIANA NA SMZ KUTEKELEZA AGENDA ZA KIKANDA, KIMATAIFA

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax amesema Wizara anayoiongoza itaendelea kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar katika kuhakikisha agenda mbalimbali za kikanda na kimataifa zinawanufaisha wananchi wa Tanzania Bara na Zanzibar.

Mhe. Dkt. Tax ametoa kauli hiyo leo tarehe 17 Novemba, 2022 wakati alipokutana kwa mazungumzo na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais -Ikulu, Mhe. Jamal Kassim Ali, Ikulu Zanzibar.

Mhe. Waziri Tax amemtembelea Mhe. Jamal, Ofisini kwake Ikulu Zanzibar kwa lengo la kumsalimia na kubadilishana naye mawazo ya namna ya kuimarisha ushirkikiano kati ya Wizara na Ofisi yake.

Pamoja na mambo mengine, Dkt. Tax amemwahidi ushirikiano Waziri Jamal na kumshukuru kwa kupata fursa hiyo muhimu ambayo inalenga kuendelea kuboresha utekelezaji wa majukumu ya Wizara hususan katika masuala ya kikanda na kimataifa kwa kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.

Waziri Tax ameongeza kuwa Wizara anayoiongoza inaendelea kutekeleza kikamilifu maelekezo yote yaliyotolewa kwao na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan pamoja na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi kuhusu kuzipa kipaumbele hoja za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwenye majukwa ya kikanda na kimataifa pamoja na kuwashirikisha Diaspora katika kuchangia maendeleo ya Taifa.

“Mhe. Waziri leo nimekuja kwa ajili ya kukusalimia kwa vile nipo hapa Zanzibar na Mabalozi wa Tanzania wote tukiendelea na Mkutano. Nakuahidi kufanya kazi kwa pamoja kwa nguvu mpya ili kuhakikisha hoja zote za kipaumbele za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania zinakuwa na tija katika majukwaa ya kikanda na kimataifa kwa manufaa ya pande zote na bila kuwasahau Diaspora wetu” amesema Dkt. Tax.

Kwa upande wake, Mhe. Jamal ambaye Ofisi yake pamoja na mambo mengine, ina jukumu la kusimamia masuala ya kikanda na kimataifa amemshukuru Dkt. Tax kwa kutenga muda na kumtembelea na kwa namna ya pekee alishukuru ushirikiano anaoupata kutoka Ofisi ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki ya Zanzibar.

Pia alieleza kuwa, ipo haja ya kuimarisha zaidi ushirikiano ulipo ili kupeleka maazimio ya pamoja kwenye majukwaa ya kikanda na kimataifa na kwamba Ofisi yake ipo tayari kutoa ushirikiano wote utakaohitajika.

Kuhusu Diaspora alisema tayari Ofisi yake imeandaa Sheria na sasa wanaendelea na zoezi la kuwatambua. Hivyo aliomba kuendeleza ushirikiano wa pamoja ili kuendelea kuwatambua, kuwasimamia na kuwaratibu ili kuwawezesha kuchangia kikamilifu maendeleo ya Taifa.

“Naomba tuendelee na ushirikiano huu ili tuweze kuwaunganisha pamoja Diaspora wetu pamoja na kuwatambua kwa usahihi ili kuweza kuwasimamia na kuwaratibu katika kuchangia maendeleo ya taifa letu,” amesema Mhe. Jamal

Dkt. Tax yupo Zanzibar kwa ajili ya kushiriki Mkutano wa Sita wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan na Mabalozi wa Tanzania unaofanyika Kisiwani humo kuanzia tarehe 14 hadi 21 Novemba 2022.

  • Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Ikulu - Zanzibar, Mhe. Jamal Kassim Ali akimsindikiza Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax baada ya kumaliza kikao chao Ikulu, Zanzibar
  • Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Ikulu - Zanzibar, Mhe. Jamal Kassim Ali akiagana na mwenyeji wake Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax baada ya kumaliza kikao chao Ikulu, Zanzibar
  • Kikao baina ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais -Ikulu, Mhe. Jamal Kassim Ali na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax kikiendelea
  • Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais -Ikulu, Mhe. Jamal Kassim Ali akieleza jambo wakati wa kikao chake na mgeni wake Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax Ofisini kwake Ikulu Zanzibar
  • Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax akieleza jambo wakati wa kikao chake na mwenyeji wake Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Ikulu, Mhe. Jamal Kassim Ali, Ikulu - Zanzibar
  • Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax akieleza jambo wakati wa kikao chake na mwenyeji wake Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Ikulu - Zanzibar, Mhe. Jamal Kassim Ali