Skip to main content
News and Events

WAZIRI MAHIGA AHITIMISHA ZIARA YAKE NCHINI NORWAY ASISITIZA UWEKEZAJI WENYE TIJA

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

WAZIRI MAHIGA AHITIMISHA ZIARA YAKE NCHINI NORWAY ASISITIZA UWEKEZAJI WENYE TIJA

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Augustine Mahiga amehitimisha ziara yake ya kikazi nchini Norway kwa mazungumzo na wafanyabiashara huku akiwapa ujumbe mkuu wa kuwekeza Tanzania ambapo tayari kuna mazingira mazuri ya uwekezaji.

Kwenye hotuba yake kwa wanachama wa Umoja wa Wafanyabiashara wa Norway na Afrika (NABA), Mhe. Mahiga ameelezea ushirikiano uliopo kati ya Serikali za Norway na Afrika kwa ujumla hususan Tanzania, ambapo Norway inasaidiana na nchi nyingi za kiafrika  ikiwemo Tanzania katika kutekeleza miradi ya maendeleo. Hii ni ishara nzuri kwa ukuaji wa biashara na mahusiano.

Akitolea mfano wa Tanzania, Mhe. Mahiga alisema kuwa miaka ya hivi karibuni Serikali ya Norway imebadilisha ushirikiano wake na Tanzania kutoka kwenye kutoa misaada kwenda kwenye udhamini wa pamoja wa miradi mbalimbali ya maendeleo yenye lengo la kuinua uchumi.

“Ushiriki wa Serikali ya Norway nchini kwetu ni wa kipekee, kwani unazingatia vipaumbele na sera za Tanzania na pale wanaongeza nguvu kwa kudhamini mafunzo na hatimaye ujenzi wa mifumo sahihi ya utekelezaji wa sera hizo” Waziri Mahiga alisema.

Waziri Mahiga aliongeza kuwa, kwenye awamu ya tano ya uongozi nchini Tanzania, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli pamoja na mambo mengine, amejenga mifumo bora ya ukusanyaji kodi, usimamizi wa rasilimali za umma pamoja na uendelezwaji wa rasilimali ya mafuta kwa maendeleo. “Serikali ya Norway inadhamini maeneo yote hayo na mengine mengi, kama mdau wa maendeleo ya Watanzania. Hivyo ni vyema na nyie wafanyabiashara muwekeze pale ambapo Serikali yenu ipo. Kwa sababu hapo ndio mahali salama kwa uwekezaji wenye tija” alihimiza Mhe. Mahiga.

Mkutano huo uliojumuisha taasisi takriban 25, ulifanyika chini ya mwamvuli wa Norfund, Taasisi inayojenga uwezo kwa wafanyabiashara kuendesha biashara kwenye nchi zinazoendelea.

Akielezea mikakati ya taasisi hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wake, Bw. Kjell Roland alisema Norfund inajikita zaidi kwenye nchi ambazo upatikanaji wa mitaji ni mgumu kutokana na uchanga wa sekta binafsi.

Kwa upande wake, Mratibu wa umoja huo wa Wafanyabiashara wa NABA, amesema kuwa wapo kwenye maandalizi ya ziara ya biashara Tanzania kabla ya mwisho wa mwaka huu.

Waziri Mahiga alitumia fursa ya mkutano huo kumtambulisha Balozi wa Tanzania nchini Norway mwenye makazi yake nchini Sweden, Mhe. Dkt. Wilbroad Slaa ambaye anatarajiwa kukabidhi hati zake  za utambulisho tarehe 21 Juni, 2018.

 

Imetolewa na:

Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,

Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,

Dar es Salaam, 21 Juni, 2018

 

Downloads File: