Skip to main content
News and Events

WAKAZI WA MARA WANUFAIKA NA MAADHIMISHO YA “SIKU YA MARA”

WAKAZI WA MARA WAJIVUNIA MAFANIKIO YA MAADHIMISHO YA SIKU YA MARA

Septemba 15 kila mwaka Tanzania na Kenya hufanya maadhimisho ya Siku ya Mara (Mara Day), ambayo pia huusisha maonesho ya bidhaa mbalimbali sambamba na utoaji elimu inayolenga kuhimiza umuhimu wa kuhifadhi mazingira ya Bonde la Mto Mara.   

Sherehe za maadhimisho haya ambayo hufanyika kwa zamu baina ya Tanzania na Kenya, mwaka huu 2021, Maadhimisho ya 10 ya Siku ya Mara yanafanyika katika Wilaya ya Tarime, mkoani Mara. Kama ilivyo ada ya maadhimisho haya kuendeshwa kwa ushirikiano baina ya pande mbili (Tanzania na Kenya) mwaka huu pia kumekuwa na ushiriki wa pande zote mbili. 

Madhimisho ya Kumi ya Siku ya Mara mwaka huu 2021 yanaongozwa na Kauli Mbiu isemayo “Tuhifadhi Mto Mara kwa Utalii na Uchumi Endelevu”  

Akizungungumza kwenye maadhimisho hayo Waziri wa Maji Mhe. Jumaa Aweso ametoa wito kwa Mkuu wa Mkoa, Wakuu wa Wilaya, Wenyeviti wa Halmashauri pamoja na Wenyeviti wa Vijiji kuhakikisha wanashughulikia kwa mtazamo chanya suala la utunzaji wa mazingira na vyanzo vya maji katika maeneo yetu.

“Suala la kuhifadhi ya mazingira ya Bonde la Mto Mara ikiwa ni pamoja na vyanzo vya maji limekua likitiliwa mkazo na Serikali ili kuhakikisha kuwa maji yaliyopo yanahifadhiwa na kutunzwa kwa mujibu wa sheria. Wito wangu kwenu ni kwamba tuendeleze ushirikiano katika uhifadhi wa mazingira ili pawepo na vyanzo vya maji vya uhakika, vyenye maji ya kutosha na yenye ubora wakati wote kwa ajili ya maendeleo” alisema Mhe. Aweso

Akizungumza kwenye ufunguzi wa maadhimisho hayo Mkuu wa Wilaya ya Tarime ambaye pia ni Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Mara Mheshimiwa Lt. Col. Michael Mangwela Mtenjela amebainisha baadhi ya mafanikio yaliyofikiwa tokea kuanza kwa Maadhimisho haya mwaka 2012 kuwa ni pamoja na; ongezeko la upandaji miti, ongezeko la watalii, kuongezeka kwa ushirikiano baina ya jamii za pande zote mbili zinazozunguka Bonde la Mto Mara na uwekwaji wa mawe ya kuonesha mipaka (bikoni) katika eneo la Bonde.  

“Mwaka huu Idadi ya miti na vigingi imeongezeka ikilinganishwa na mwaka 2020 ambapo miti 2600 ilipandwa pamoja na vigingi 20 katika Wilaya ya Butiama. Ongezeko hili linatokana na juhudi za makusudi zinazochukuliwa na Mkoa wa Mara katika kuhifadhi ikolojia ya Bonde la Mto Mara na Mkoa mzima wa Mara” alieleza Mheshimiwa Lt.Col. Mtenjela.

Kwa upande wake Balozi wa Tanzania nchini Kenya Mhe. Dkt. John Simbachawene ameeleza kuwa Mara Day ni jukwaa linatoa fursa nzuri ya utetezi na ushirikiano kati ya watendaji wa serikali, asasi za kiraia, sekta binafsi, washirika wa maendeleo na mashirika yasiyo ya kiserikali katika mashirikiano ya kuimarisha usimamizi na maendeleo ya rasilimali za maji katika Bonde la Mto Mara. 

Katika kuadhimisha Siku ya Mto Mara mwaka 2021, sambamba na shughuli zingine zilizokuwa zikiendelea Mkoa wa Mara umepanda miti 13,000 na kuweka vigingi 70 katika vijiji vya Mrito na Kerende vilivyopo wilayani ya Tarime.

Akizungumza katika hafla ya ufunguzi wa madhimisho hayo Bi. Bhoke Mwita amkazi wa Tarime ameelezea kuridhishwa kwake na mafanikio aliyoyaona tokea kuanzishwa kwa maadhimisho ya Siku ya Mara. Ambapo ameeleza kuwa hapo awali pamoja na kunufaika na Mto Mara hawakutambua umuhimu wa kutunza mazingira yanayo uzunguka hivyo kusababisha uharibifu wa Ikolojia ya Bonde, tofauti na ilivyo sasa ambapo kupitia Maadhimisho haya wamejifunza na kuhamasika kutunza mazingira ya Bonde la Mto Mara. 

Tunazishukuru sana Serikali zetu ya Tanzania na Kenya kwa kuridhia kufanyika kwa Maadhimisho haya, licha kupata fursa ya kushiriki maonesho tunapata elimu kubwa kuhusu umuhimu wa kulinda Bonde la Mto Mara, sasa tumefikia mahali ambapo sisi wenyewe tunakuwa mlinzi dhidi ya kila mmoja kuzuia uharibifu katika mazingira ya Bonde la Mto. Kwa mafanikio tuanayoendelea kuyaona na kunufaika nayo hatuna budi kuendelea kuhifadhi mazingira kwa ajili ya mandeleo yetu wenyewe. Alisema Bi. Bhoke Mwita

Mto Mara ambao ni eneo muhimu kwa maendeleo ya kiuchumi pamoja na baioanuai zilizopo unaanzia katika chemchem ya Enapuyapui iliyopo kwenye misitu ya Milima ya Mau nchini Kenya, ambapo maji ya Mto huo hutiririka kupitia pori la akiba la Hifadhi ya Taifa ya Maasai-Mara kwa upande wa Kenya na hatimaye katika Hifadhi ya Taifa ya Serengeti (SENAPA) kwa upande wa Tanzania, kabla ya kumwaga maji yake katika Ziwa Victoria. Mto huu unapita katika Wilaya nne kwa upande wa Tanzania ambazo ni Serengeti, Tarime, Rorya na Butiama.

Maadhimisho haya yanatokana na Mkutano wa 10 wa Baraza la Mawaziri la Kisekta la Bonde la Ziwa Victoria lililoamua kuwe na Maadhimisho ya Siku ya Mara kila mwaka ifikapo tarehe 15 Septemba katika Mkutano uliofanyika Mei 4,2021 jijini Kigali, Rwanda ili kuhamasisha na kutoa elimu kwa wadau juu ya utunzaji wa mazingira na rasilimali maji katika Bonde la Mto Mara. 

 • Meza Kuu wakifuatilia matukio mbalimbali yaliyokuwa yakiendela kwenye Maadhimisho ya 10 ya Siku ya Mara yaliyofanyika katika viwanja vya Chuo cha Uwalimu cha Tarime, Musoma
 • Waziri mwenye Dhamana ya Usimamizi wa Rasilimali Maji Mhe. Job Kiyiapi kutoka Kenya akizungumza na wananchi (hawapo pichani) waliojitokeza kushiriki kilele cha Maadhimisho ya 10 ya Siku ya Mara yaliyofanyika katika viwaja vya Chuo cha Uwalimu cha Tarime, Musoma.
 • Mkuu wa Wilaya ya Tarime Mhe. Lt. Col. Michael Mangwela Mtenjela akizungumza na wananchi waliojitokeza kwenye ufunguzi wa Maadhimisho ya 10 ya Siku ya Mara yaliyofanyika katika viwaja vya Chuo cha Uwalimu cha Tarime, Musoma.
 • Kaimu Mkurugenzi wa Miundombinu ya Uchumi na Huduma za Kijamii Bw. Eliabi Chodota (wakwanza) katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki akifuatilia matukio mbalimbali yaliyokuwa yakiendela kwenye kilele cha Maadhimisho ya 10 ya Siku ya Mara yaliyofanyika katika viwanja vya Chuo cha Uwalimu cha Tarime, Musoma
 • Waziri wa Maji Mhe. Jumaa Aweso (wapili kulia) akiwa ameambatana na viongozi na watendaji mbalimbali wa Serikali wakati akielekea kuona bidhaa mbalimbali za wafanyabiashara walioshiriki maonesho ya Maadhimisho ya Siku ya Mara
 • Waziri wa Maji Mhe. Jumaa Aweso (Mb) akifuatilia maelezo kuhusu huduma mbalimbali za Mamlaka ya Kodi Tanzania (TRA) alipotembelea banda la Mamlaka hiyo kwenye kilele cha Maadhimisho ya 10 ya Siku ya Mara
 • Balozi wa Tanzania nchini Kenya Mhe. Dkt. John Simbachawene (wakwanza kulia) akifuatilia Maadhimisho ya 10 ya Siku ya Mara yaliyokuwa yakiendelea katika viwaja vya Chuo cha Uwalimu cha Tarime, Musoma
 • Balozi wa Tanzania nchini Kenya Mhe. Dkt. John Simbachawene akizungumza na wananchi waliojitokeza kushiriki kilele cha Maadhimisho ya 10 ya Siku ya Mara yaliyofanyika katika viwaja vya Chuo cha Uwalimu cha Tarime, Musoma.
 • Waziri wa Maji Mhe. Jumaa Aweso (Mb) akisisitiza jambo wakati akizungumza na Wananchi wa Tarime (hawapo pichani) kwenye kilele cha Maadhimisho ya 10 ya Siku ya Mara
 • Waziri wa Maji Mhe. Jumaa Aweso (Mb) akisaini kitabu cha wageni kwenye Maadhimisho ya 10 ya Siku ya Mara yaliyofanyika Wilayani Tarime, Musoma
 • Waziri wa Maji Mhe. Jumaa Aweso (Mb) akisalimiana na Bw. Eliabi Chodota Kaimu Mkurugenzi wa Miundombinu ya Uchumi na Huduma za Kijamii katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, wakati alipowasili katika viwaja vya Chuo cha Uwalimu cha Tarime kwenye Maadhimisho ya 10 ya Siku ya Mara