Skip to main content
News and Events

TANZANIA YAONESHA NJIA MISSION 300

Tanzania imetajwa kama nchi iliyoonesha njia katika kufikia azma ya kufikisha umeme kwa watu milioni 300 barani Afrika ifikapo mwaka 2030.

Hayo yamejiri wakati wa Mkutano wa Wakuu wa Nchi za Afrika kuhusu Nishati unaofanyika kwenye Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere jijini Dar Es Salaam Januari 28,2025.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan alitajwa katika mkutano huo kama kiongozi mwanamke, wa mfano kwa kuwaunganisha viongozi wenzake barani Afrika na wadau wengine kujadili kwa pamoja mikakati itakayopelekea Bara la Afrika kuwa na nishati ya umeme ya uhakika, endelevu na nafuu.

Rais Samia alisema Bara la Afrika lina jukumu la kuwaondolea umasikini watu wake kwa kufanya uwekezaji na kujenga viwanda vitakavyozalisha ajira na kukuza uchumi. Amesema hayo yatawezekana ikiwa tu, bara la Afrika litakuwa na umeme wa uhakika, endelevu na nafuu.

Kuboresha upatikanaji wa umeme wa uhakika nchini, Rais Samia alisema Tanzania ni moja ya nchi 12 zitakazosaini Mpango Mahsusi wa Kitaifa wa Nishati ambapo Dola za Marekani bilioni 13 zinahitajika katika kipindi cha miaka mitano ijayo ili kutekeza mpango huo. Kati ya fedha hizo bilioni tano zitatoka sekta binafsi ili kufanya uwekezaji utakaosaidia upatikanaji wa umeme kufikia asilimia 72 ifikapo mwaka 2030.

Rais Samia alisema Serikali yake itatekeleza mpango huo kwa kuongeza uzalishaji wa umeme kupitia vyanzo mchanganyiko na lengo ni kuongeza uzalishaji wa Megawati 2463 kupitia nishati ya jua, gesi asilia, joto-ardhi, upepo na vyanzo vingine ifikapo mwaka 2030.

Aidha, Serikali itaendelea na ujenzi wa njia za kusafirisha umeme kuunganisha na nchi za Mashariki na Kusini mwa Afrika kwa ajili ya kufanya biashara na nchi hizo. Hadi sasa nchi za Burundi, Rwanda na Kenya zimeunganishwa na Serikali inaendelea na ujenzi wa miundombinu ya kuunganisha umeme na nchi za Zambia na Uganda.

Rais Samia aliongeza kuwa mahitaji ya umeme ya Tanzania kwa sasa ni megawati 1888 na uzalishaji ni megawati 3431, hivyo kuna ziada ya kufanya biashara na nchi nyingine.

Mikakati mingine  ni kufikisha umeme kwenye vitongoji baada ya zoezi la kufikisha umeme vijiji vyote vya Tanzania kukamilika na kusambaza nishati safi ya kupikia ambapo malengo ni kuongeza kiwango cha matumizi ya nishati hiyo kutoka asilimia 10 za sasa hadi 80 ifikapo mwaka 2034.

Naye, Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), Dkt. Akinwumi Adesina ametangaza msaada wa Dola za Marekani bilioni 46 kutoka taasisi mbalimbali kwa ajili ya utekelezaji wa Mission300. Fedha hizo zitatolewa na Benki ya Dunia bilioni 22; AfDB bilioni 18; Benki ya Maendeleo ya Kiislam bilioni 2.5; Benki ya Maendeleo ya Uwekezaji wa Miundombinu ya Asia bilioni 1.5; na Mfuko wa OPEC bilioni 2.

Alisema wadau wengine wataendelea kutoa ahadi ya fedha kwa ajili ya kufanikisha mpango huu adhimu kwa maendeleo ya Bara la Afrika.