Skip to main content
News and Events

TANZANIA YACHAGULIWA MJUMBE WA BARAZA LA ITU

Tanzania imefanikiwa kushinda kwa kishindo katika uchaguzi wa wajumbe wa Baraza la Shirika la Mawasiliano Duniani (ITU) katika uchaguzi uliofanyika wakati wa mkutano mkuu wa ITU jijini Bucharest, Romania leo, tarehe 3 Oktoba 2022. Tanzania imepata kura 141 kati ya kura 180 zilizopigwa na nchi wanachama wa Shirika hilo.  Baraza la ITU husimamia shughuli za Shirika katika kipindi cha kati ya mikutano mikuu ambayo hufanyika kila baada ya miaka 4. Ujumbe wa Tanzania katika mkutano huu uliongozwa na Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhe. Nape Moses Mnauye (Mb) na kujumuisha maofisa waandamizi wengine kutoka Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki na Mashirika na Taasisi za Mawasiliano nchini. Kwa kuchaguliwa kwake, Tanzania sasa itakuwa mjumbe wa Baraza la ITU kwa kipindi cha miaka 4 ijayo. Ushindi huu ni mafanikio makubwa kwa Tanzania na ni kielelezo cha kazi nzuri anayoifanya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe Samia Suluhu Hassan katika medani ya kimataifa na hivyo kuifanya nchi iweze kukubalika na kuaminiwa.  Ushindi huu pia ni matokeo ya kampeni ya kimkakati iliyoendeshwa na Tanzania kupitia Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki na Ubalozi wa Kudumu wa Tanzania, Umoja wa Mataifa - Geneva. Aidha, Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari na Taasisi zilizopo chini yake zilizifanya kazi kubwa ya kampeni na kutoa raslimali muhimu kwa ajili hii.  Itakumbukwa kuwa Tanzania iliwahi kuwa mjumbe wa Baraza hili kabla ya kushindwa katika uchaguzi uliofanyika mwaka 2018, Dubai UAE. Miongoni mwa faida za kuwa mjumbe wa Baraza la ITU ni pamoja na: • Kuwa katika nafasi nzuri ya kutambua fursa zilizopo na hatimaye kunufaika na misaada na huduma zinazotolewa na Mashirika na pia kupata taarifa muhimu za miradi na shughuli za ITU kwa urahisi na haraka • Kujua na kuratibu mwenendo wa teknolojia mpya ili kuandaa njia za utatuzi wa changamoto zake. • Kukuza uwezo wa kiutendaji wa wataalamu nchini wanaoshiriki katika shughuli za Baraza ikiwa ni pamoja na kubadilishana ujuzi na uzoefu na nchi nyingine katika masuala mbalimbali. • Kupata fursa ya kupokea na kuchambua taarifa mbalimbali za utendaji wa ITU, kutoa mapendekezo na kuboresha mwenendo wa Umoja.  • Kuwasilisha mapendekezo ya nchi juu ya uendeshaji wa ITU. • Kushawishi maamuzi yatolewayo na Baraza yasiwe na matokeo hasi kwa sekta ya mawasiliano. • Kuitangaza nchi na kuchangia maendeleo ya sekta ya mawasiliano barani Afrika na duniani kwa ujumla.
  • jumbe wa Tanzania ukiongozwa na Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Nape Mnauye (wa pili kutoka kulia) ukisubiri kutangazwa kwa matokeo ya kura ya uchaguzi wa Baraza la Shirika la Mawasiliano (ITU). Wengine katika picha, wa kwanza kulia ni Mkurugenzi wa Ushirikiano wa Kimataifa katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Robert Kahendaguza na kushoto kwa Mhe. Waziri Nape ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari
  • Ujumbe wa Tanzania ukishangilia ushindi baada ya kutangazwa kwa matokeo