TANZANIA NA FINLAND ZAKUBALIANA KUONGEZA WIGO WA USHIRIKIANO
TANZANIA NA FINLAND ZAKUBALIANA KUONGEZA WIGO WA USHIRIKIANO
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Jamhuri ya Finland zimekubaliana kuanzisha maeneo mapya ya ushirikiano huku kipaombele kikiwekwa zaidi kwenye masuala ya maendeleo ya kiuchumi na kijamii.
Hayo yameelezwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan na Rais wa Jamhuri ya Finland Mheshimiwa Alexander Stubb kwenye mkutano wao wa pamoja na waandishi wa habari uliofanyika Ikulu jijini Dar es Salaam Mei 14, 2025.
Rais Samia ameyataja maeneo hayo ya ushirikiano kuwa ni uchumi wa buluu, madini, elimu, utalii, biashara na uwekezaji, misitu, uhifadhi wa mazingira, nishati, mafunzo ya kidigitali, ufundi stadi na nishati safi ya kupikia.
Vilevile, Rais Samia ameeleza kuwa pande zote mbili zimekubaliana kuanzisha ushirikiano kupitia Taasisi ya Uongozi ambao utajikita katika kutoa mafunzo ya kuwajengea uwezo wa uongozi wanawake ikiwa ni moja ya jitihada za kuleta usawa wa kijinsia nchini.
Mbali na hayo Rais Samia ameizungumzia ziara hiyo kuwa imefungua zama mpya za ushirikiano katika Nchi hizo mbili rafiki, huku akiahidi kuwa Tanzania itaendelea kushirikiana na Finland katika kutetea agenda mbalimbali za uwili na kimataifa ikiwemo ustawi wa uchumi wa watu, kulinda amani na usalama na utunzaji wa mazingira.
Kwa upande wake Rais wa Finland Mheshimiwa Stubb, ambaye ameambatana na ujumbe wa wafanyabiashara kutoka makampuni 10 ya nchini humo, ameeleza kuwa pamoja na masuala mengine ziara yake hapa nchini itasaidia kukuza ushirikiano wa sekta binafsi kupitia biashara na uwekezaji.
Tanzania na Finland tumekuwa washirika kwa muda mrefu na daima tumekuwa na mitazamo inayofanana kuhusu musuala mbalimbali ya kimataifa ikiwemo kupigania mageuzi katika mfumo wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ili liweze kuendana na mabaliko ya nyakati tunazoishi.
“Finland inaitazama Tanzania kama mshirika wa kipekee katika bara la Afrika, daima tumekuwa na mitazamo inayofanana ya kutaka misingi ya sheria za kimataifa ziheshimiwe na kutekelezwa kwa usawa, kupigania usawa wa kijinsia, na amani na usalama. Hivyo ni imani yangu kuwa katika siku za usoni Finland na Tanzania tutakuwa wajumbe wa Baraza la Amani na Usalama la Umoja wa Mataifa”. Alisema Mheshimiwa Rais Alexander Stubb.
Finland kwa sasa barani Afrika inaushirikiano na Mataifa mawili pekee ambayo ni Tanzania na Ethiopia.
Mheshimiwa Alexander Stubb amewasili nchini kwa ziara ya kitaifa ya siku tatu kuanzia tarehe 14 hadi 16 Mei, 2025 na kupokelewa na mwenyeji wake Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan katika hafla iliyofanyika Ikulu jijini Dar es Salaam.
Pamoja na masuala mengine Rais Stubb anatarajiwa kushiriki katika sherehe ya maadhimisho ya miaka 60 ya uhusiano wa kidiplomasia kati ya Tanzania na Finland itakayo fanyika kesho Mei 15, 2025 jijini Dar es Salaam.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan akizungumza na waandishi wa habari (hapo pichani) kuelezea yaliyojili kwenye mazungumzo na mgeni wake Rais wa Jamhuri ya Finland Mheshimiwa Alexander Stubb yaliyofanyika Ikulu jijini Dar es Salaam.
Rais wa Jamhuri ya Finland Mheshimiwa Alexander Stubb akizungumza na waandishi wa habari (hapo pichani) kuelezea yaliyojili kwenye mazungumzo na mwenyeji wake Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan yaliyofanyika Ikulu jijini Dar es Salaam