TANZANIA KUIMARISHA UFANISI WA MFUMO WA KODI ILI KUKUZA UWEKEZAJI NCHINI
TANZANIA KUIMARISHA UFANISI WA MFUMO WA KODI ILI KUKUZA UWEKEZAJI NCHINI
Tanzania imechukua hatua stahiki za kuimarisha ufanisi wa mfumo wake wa kodi, ili kukuza uwekezaji na biashara na mataifa mbalimbali duniani.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Mahamoud Thabit Kombo, amesema hayo tarehe 13 Novemba, 2024 jijini Dar es Salaam alipozungumza na Jumuiya ya Wanadiplomasia wanaowakilisha nchi na Mashirika ya Kimataifa nchini.
Mhe. Kombo amesema Serikali inatambua malalamiko yanayohusiana na mfumo wa ulipaji kodi kwa wafanyabiashara wa ndani na wa kigeni na katika kukabiliana na changamoto hiyo imeunda Tume ya Rais kwa ajili ya kupitia na kutathimini mfumo uliopo, ambapo pia itapitia upya Sera ya kodi. Ameingeza kuwa Serikali itashirikisha wadau mbalimbali ili kutoa maoni yao yatakayochangia kuleta matokeo chanya kwa walipa kodi na tija kwa Taifa.
Mhe. Kombo ameongeza kuwa, katika kuimarisha Diplomasia ya kijamii na kiuchumi na kuendana na Siasa za kImataifa, Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imefanya mapitio ya Sera ya Mambo ya Nje ya mwaka 2001.
Amewaambia Mabalozi kuwa mchakato wa mapitio ulijumuisha mashauriano ya kina na wadau mbalimbali ndani ya nchi na nje ya nchi.
“Ni furaha yangu kuwaarifu kuwa Sera ya Mambo ya Nje ya mwaka 2001 sasa itajulikana kama Toleo la 2024 baada ya kuridhiwa na Baraza la Mawaziri tarehe 25 Oktoba, 2024, Kuanzia sasa, Sera ya Mambo ya Nje Toleo la mwaka 2024 ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania itapatikana kwenu nyote na kwa wadau wengine itakapochapishwa na kusambazwa rasmi”, alisisitiza Balozi Kombo.
Amesema kuwa Sera ya Mambo ya Nje itaendelea kuzingatia Diplomasia ya Uchumi, na misingi iliyopo ya kulinda maadili ya kijamii na ya kitamaduni ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kama kitambulisho muhimu cha Taifa ikilenga kukuza amani, utulivu, usalama, Utawala Bora na Udugu; huku ikiheshimu misingi ya kutofungamana na upande wowote (Non-Alignment); a uhusiano wa Kidiplomasia ya uwili, Kikanda na Kimataifa.
Aliongeza kuwa Sera hiyo ya Mambo ya Nje pia itazingatia masuala mbalimbali ya kisasa ikiwemo matumizi ya Lugha ya Kiswahili yatakayoimarisha diplomasia, kuendeleza ajenda ya Uchumi wa Buluu (Blue Economy); ushirikiano na Diaspora na kuibua mikakati ya hifadhi bora ya Mazingira na udhibiti wa Mabadiliko ya Tabianchi, ambayo hayakuwepo hapo awali.
Masuala mengine katika Sera hiyo yanahusu Jinsia na Vijana; Kukuza Haki za Binadamu kulingana na Katiba ya nchi, na maadili ya kijamii na kitamaduni ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na watu wake.