Skip to main content
News and Events

TANZANIA KUENDELEA KUIMARISHA USHIRIKIANO NA SEKRETARIET YA EAC

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mheshimiwa January Makamba (Mb.) amekutana na Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) Mhe. Dkt. Peter Mathuki kuzungumzia masuala muhimu yanayohusu kuimarisha na kuboresha ushirikiano baina ya Sekretarieti ya Jumuiya hiyo na nchi wanachama kwa maslahi mapana ya Jumuiya. Viongozi hao wawili ambao wamekutana leo tarehe 07 Februari 2024 jijini Dar es Salaam, wamezungumzia pamoja na mambo mengine, masuala ya kulinda amani na usalama kwa nchi wanachama na kuimarisha ushirikiano wa kibiashara baina ya nchi wanachama ili kukuza na kuimarisha uchumi wa wananchi wa nchi wanachama. Akizungumza, Mhe. Waziri Makamba amesisitiza umuhimu wa Baraza la Mawaziri wa EAC kukutana mara kwa mara hata kidijitali ili kuweza kujadili masuala muhimu kwa wakati na kutoa suluhu kwa wakati kwa migogoro mbalimbali inayojitokeza hususan ile ya kibiashara. Kwa upande wake, Dkt. Mathuki amesema kwa migogoro ya kibiashara inayojitokeza baina ya nchi na nchi isichukuliwe kama udhaifu bali ichukuliwe kama chachu kwa nchi hizo ya kutafuta suluhu za kudumu kwa migogoro hiyo. “Wakati wowote migogoro inapotokea, isichukuliwe kama udhaifu. Tunaweza kuwa na migogoro yenye afya inayolenga kutatua tatizo,” amesema Dkt. Mathuki. Katika mazungumzo yao, Viongozi hao wamejadili pia juu ya namna bora ya kuliendeleza eneo la Ardhi ya EAC lililopo Kisongo mkoani Arusha kwa ajili ya shughuli za Jumuiya.

  • Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mheshimiwa January Makamba (Mb.) akisisitiza jambo wakati wa mazungumzo na Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) Mhe. Dkt. Peter Mathuki yaliyofanyika jijini Dar es Salaam
  • Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) Mhe. Dkt. Peter Mathuki akifafanua jambo wakati wa mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mheshimiwa January Makamba (Mb.) jijini Dar es Salaam