Skip to main content
News and Events

TANZANIA, CUBA KUIMARISHA SEKTA ZA KIPAUMBELE

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Jamhuri ya Cuba zimekubaliana kuimarisha ushirikiano wa maendeleo katika sekta za kipaumbele ambazo ni elimu, afya, kilimo na utalii.

Makubaliano hayo yameafikiwa wakati Makamu wa Rais wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Mpango alipokutana kwa mazungumzo na Makamu wa Rais wa Cuba, Mhe. Salvador Mesa, Ikulu Jijini Dar es Salaam.

Taarifa ya makubaliano hayo ilielezwa na viongozi hao wawili wakati wa mkutano na waandishi wa Habari uliofanyika Ikulu Jijini Dar es Salaam tarehe 24 Januari 2024.

Awali, viongozi hao walishuhudia utiaji saini wa Hati mbili za Makubaliano ya Ushirikiano (MoUs) ambazo ni makubaliano kati ya Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA) na Chuo Kikuu cha Artimesa Diaz Gonzalez cha Cuba. 

Hati ya pili ya Makubaliano ni kati ya Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba Tanzania(TMDA) na Kituo cha Afya cha Taifa cha Udhibiti na Vifaa Tiba (CECMED) cha Serikali ya Cuba kwa lengo la kupanua wigo na kuongeza matumizi ya teknolojia katika masuala ya dawa na vifaa tiba.

Kadhalika, Dkt. Mpango aliongeza kuwa, Serikali ya Cuba imekubali kuendelea kuimarisha kiwanda cha Viuatilifu cha Biotech, Kibaha, Pwani ambapo kwa sasa kitaanza kutengeneza dawa za binadamu na kilimo na kuwa kiwanda cha kipekee barani Afrika. 

“katika mazungumzo yetu tumekubaliana Cuba waje kuimarisha kiwanda cha Viatilifu cha Biotech cha Kibaha na kwa sasa kiwanda hicho kitaanza kutengeneza dawa za binadamu za aina zaidi ya 10 sambamba na kuongeza wigo wa masoko ukanda wa Afrika Mashariki,”alisema Dkt. Mpango.

Pamoja na mambo mengine, viongozi hao wamekubaliana kuendelea kuimarisha ushirikiano wa kihistoria baina ya mataifa hayo uliodumu kwa muda mrefu. 

Kwa upande wa Makamu wa Rais wa Cuba, Salvador Mesa ameisifu Tanzania kwa kuitetea Cuba kimataifa na kusimama kupinga vikwazo wanavyowekewa vya kiuchumi na kusema imekuwa Nchi hizo ni ndugu na rafiki wa kweli.

“Tunaishukuru Tanzania kwa kutuunga mkono dhidi ya vikwazo tulivyowekewa vya kiuchumi, mmetutetea kupinga na kutaka vikwazo hivyo viondolewe ili kutuwezesha kutumia rasilimali zetu na kukuza uchumi,” alisema Mhe. Mesa.

Mhe. Mesa aliongeza kuwa lengo la ziara yake nchini ni kuimarisha na kuendeleza ushirikiano na Tanzania katika sekta ya elimu, afya, kilimo, siasa na utalii na kuwa Cuba itaendelea kukitangaza Kiswahili nchini humo na Ukanda wa Amerika ya Kusini.

Wakati huohuo, Mhe. Mesa amekutana kwa mazungumzo na Spika wa Bunge la Tanzania, Dkt. Tulia Ackson ambapo pamoja na mambo mengine wamejadili masuala ya ushirikiano kati ya Tanzania na Cuba. 

  • Mkuu wa Chuo Kikuu cha Kilimo (SUA) Prof. Raphael Chibunda na Mkuu wa Chuo Kikuu cha Cuba, Prof. Adianez Fernandez wakionesha (MoUs) walizosaini Jijini Dar es Salaam
  • Makamu wa Rais wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Mpango na Makamu wa Rais wa Cuba, Mhe. Salvador Mesa wakishuhudia utiaji saini wa Hati za Makubaliano ya Ushikiano kati ya Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba Tanzania(TMDA) na Kituo cha Afya cha Taifa cha Udhibiti na Vifaa Tiba (CECMED) cha Serikali ya Cuba, Ikulu Jijini Dar es Salaam. Hati hizo zimesainiwa na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba Tanzania (TMDA) Bw. Adam Fimbo na Naibu Waziri wa Afya wa Cuba, Mhe. Reinol Garcia Mareno
  • Makamu wa Rais wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Mpango na Makamu wa Rais wa Cuba, Mhe. Salvador Mesa wakiongea na waandishi wa habari Ikulu Jijini Dar es Salaam.