Skip to main content
News and Events

SERIKALI YAELEZEA MAFANIKIO ZIARA ZA RAIS MAREKANI, UGANDA NA ROYAL TOUR

Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu, Zuhura Yunus, amefafanua mafanikio ya ziara ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan, nchini Marekani iliyojumuisha uzinduzi wa Filamu ya “Tanzania; The Royal Tour." Pamoja na ziara ya Rais nchini Uganda. 

Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika Ikulu jijini Dar es salaam, Bi. Yunus amesema ziara ya Rais nchini Marekani imekuwa na faida ya kusainiwa kwa mikataba saba kati ya kampuni za Marekani na Tanzania zenye lengo la kufanya biashara na uwekezaji nchini yenye gharama za zaidi ya shilingi Trilioni 11. 

Naye Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula (Mb) ameelezea ziara ya Rais nchini Uganda ambayo iliwezesha  kufanyika kwa mkutano maalum na wadau wa sekta za mafuta na gesi kuhusiana na ujenzi wa bomba la mafuta.

"Tulikuwa na mkutano maalum juu ya ujenzi wa bomba la mafuta kutoka Uganda hadi Tanzania, tayari hatua ya ulipaji fidia kwa wananchi imekamilika na  ujenzi wa bomba hilo utaanza hivi karibuni", alisema Balozi Mulamula.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya Rais ya kuitangaza Tanzania, Dkt. Hassan Abbasi, amesema Filamu ya Royal Tour imeonesha mafanikio makubwa sana na kwa sasa filamu hiyo imeendelea kusambazwa katika vituo vya televisheni karibu 300 kati ya 350 nchini Marekani na kwa hapa nchini tayari filamu hiyo imesambazwa katika vituo vyote vya televisheni.

Naye Katibu Mkuu  Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara Prof. Godius Kahyarara amesema filamu ya Royal Tour ina manufaa ya moja kwa moja kwa Taifana  inatarajiwa kuleta wawekezaji, watalii na wafanyabiashara na kuongeza kuwa wao kama Wizara wameandaa mkutano na wadau ili kupanga mikakati ya kuwekeza katika sekta ya utalii.

Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Utalii (TTB), Bw. Amos Nko amesema TTB inatangaza kwa kasi vivutio vya utalii ili kuvutia watalii wengi kuja nchini. 

  • Katibu Mkuu Wizara ya Sanaa, Utamaduni, na Michezo, Dkt. Hassan Abbas akiwaelezea Waandishi wa Habari (hawapo pichani) mafanikio ya ziara ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan nchini Marekani na Uganda katika Mkutano uliofanyika Ikulu Jijini Dar es Salaam
  • Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu Bibi Zuhura Yunus akizungumza na Waandishi wa Habari (hawapo pichani) kuhusu ziara ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan nchini Marekani na Uganda katika Mkutano uliofanyika Ikulu Jijini Dar es Salaam