Skip to main content
News and Events

’SERIKALI YA KENYA IMEJIFUNZA KUTUMIA TAASISI KAMA NSSF KUFANYA UWEKEZAJI’ - WAZIRI MKUU WA KENYA.

’SERIKALI YA KENYA IMEJIFUNZA KUTUMIA TAASISI KAMA NSSF KUFANYA UWEKEZAJI' - WAZIRI MKUU WA KENYA.

SERIKALI ya Tanzania Juni 18 2024 imezindua rasmi ujenzi wa majengo pacha jijini Nairobi, Kenya yatakayotumika na ofisi za Ubalozi wa Tanzania nchini humo na kama kitega uchumi.

Ujenzi huo ambao ni uwekezaji Baina ya Serikali na Mfuko wa Hifadhi ya Jamii wa NSSF na utajengwa katika eneo la kibiashara katikati ya jiji la Nairobi kwenye eneo ambalo Serikali ya Kenya iliipa Tanzania kwa ajili ya kujenga ofisi zake za ubalozi.

Mgeni rasmi katika tukio hilo, Waziri Mkuu na Waziri wa Mambo ya Nje wa Kenya, Mhe. Musalia Mudavadi, ameipongeza Serikali ya Tanzania kujenga jengo hilo akisema litakuwa mojawapo ya alama za kudumu za uhusiano wa kirafiki baina ya nchi hizo mbili.

Mudavadi ambaye amewahi kuwa Waziri wa Fedha wa Kenya, amesema serikali yao pia imejifunza kitu kuhusu namna ya kutumia fedha za mifuko ya hifadhi za jamii kama NSSF kwa kufanya uwekezaji ili zizalishe zaidi na kuwa muda si mrefu, Kenya itafuata nyayo za Tanzania kwenye utaratibu huo.

Akizungumza katika tukio la uzinduzi huo, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, January Makamba, amesema mradi huo ni sehemu ya mkakati mpya wa serikali kuhakikisha inatumia maeneo na majengo yake yaliyopo ughaibuni kuingiza fedha za kigeni badala ya kutumia fedha za serikali kuendesha ofisi hizo.

Waziri Makamba amesema mkakati wa serikali unataka kuiondoa Tanzania kutoka kutumia kiasi cha shilingi bilioni 29 kwa mwaka kulipa kodi za pango kwenye balozi zake ughaibuni na badala yake kuingiza kiasi cha shilingi bilioni 36 kwa mwaka kama mapato ya uwekezaji kama huo wa unaofanyika Kenya.

Kwa upande wake, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira na Walemavu), Deo Ndejembi, amesema mradi huo umefanyika baada ya upembuzi yakinifu wa kina uliofanywa na kubainisha faida itakayopatikana baada ya kukamilika kwa ujenzi huo.

Tukio hili lilihudhuriwa na Waziri Mkuu wa Kenya ambaye pia ni Waziri wa Mambo ya Nje, Mhe. Musalia Mudavadi, Waziri wa Afrika Mashariki wa Kenya Mhe. Peninah Malonza, Waziri wa Uwekezaji, Biashara na Viwanda wa Kenya Mhe. Rebecca Maino, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. January Makamba na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi na Ajira), Deo Ndejembi, Wafanyakazi wa Wizara ya Mambo ya Nje na Wafanyakazi wa NSSF.