Rais Samia Azindua Sera ya Mambo ya Nje
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amezindua Sera ya Mambo ya Mje ya Mwaka 2001, Toleo la Mwaka 2024 katika hafla iliyofanyika jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa Sera hiyo, Mhe. Dkt Samia amesema maboresho ya Sera ya Mambo ya Nje, yamefanywa ili kuiwezesha Tanzania kuendana na mahitaji na kasi ya mabadiliko yanayoendelea duniani katika nyanja zote za kisiasa, kiuchumi na kijamii.
Amesema kuwa ili kunufaika na kwenda sambamba na mabadiliko haya zinaihitajika mbinu, mikakati na maarifa mapya na kwamba kuzinduliwa kwa sera hiyo ni mkakati mmoja wapo wa kuhakikisha Tanzania inafikia malengo yake kupitia jukwaa la ushirikiano na nchi mbalimbali pamoja na mashirika ya kikanda na Kimataifa.
Mhe. Rais Samia amesisitiza kuwa pamoja na kuzinduliwa kwa Sera hiyo, misingi ya Sera ya Mambo ya Nje iliyowekwa na waasisi wa Taifa hili haijabadilika ikiwemo uhuru wa nchi kujiamulia yenyewe, ujirani mwema, na kutofungamana na upande wowote katika masuala ya kimataifa. Aidha, amekumbusha umuhimu wa kuendeleza umoja wa Afrika na kuunga mkono Umoja wa Mataifa katika jitihada za maendeleo ya kiuchumi, kulinda amani, na usalama duniani.
Aliongeza kusema kuwa toleo hili la sera linalenga kuendelea kulinda na kukuza maslahi ya Tanzania katika nyanja za kisiasa, kiuchumi, na kijamii kupitia dhana ya Diplomasia ya Uchumi; Kukuza ushirikiano wa kiuchumi na mataifa mbalimbali na mashirika ya kikanda na kimataifa na kuhamasisha uwekezaji na biashara; kuwashirikisha Watanzania waishio nje ya nchi (Diaspora) katika kuchangia maendeleo ya Taifa; Kukuza matumizi ya Kiswahili duniani; kutilia mkazo masuala Uchumi wa Buluu kwa kujumuisha masuala ya mazingira katika mikakati ya diplomasia na kuimarisha usimamizi na uratibu wa mikataba ya kimataifa ili kulinda masilahi ya Taifa.
Amesema Sera iliyoboreshwa ni sera yenye mwelekeo na matwaka ya Watanzania kwa kuwa wameshiriki kikamilifu hadi kukamilika kwake.
Kadhalika ameitaka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kuhakikisha wanatoa elimu kuhusu maudhui ya sera husika ili ieleweke na kutekelezwa kwa ufanisi
Akiongea kuhusu kulinda uhuru na amani ya nchi, Mheshimiwa Rais Samia amesema kuwa ni vyema kwa Wizara na Vyombo vya dola vikachukua hatua za haraka kufafanua, kukanusha au kukubaliana na hoja kujipanga.
Amesema kama nchi hatupaswi kuruhusu wanahaakati na watovu wa nidhamu kutoka nchi nyingine kuja na kuvuruga amani na usalama ambao umekuwepo nchini mwetu kwa miaka mingi.