Skip to main content
News and Events

RAIS DKT. SAMIA AWAHAKIKISHIA MABALOZI USHIRIKIANO

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amewahakikishia Mabalozi wanaoziwakilisha nchi zao hapa nchini na Wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa kuwa Serikali itaendelea kushirikiana nao wakati wote wa utekelezaji wa majukumu yao hapa nchini.

Mhe. Rais Dkt. Samia alitoa ahadi hiyo tarehe 13 Januari, 2023 katika Sherehe za Mwaka Mpya 2023 kwa Mabalozi (Diplomatic Sherry Party) iliyofanyika Ikulu jijini Dar es Salaam.

Pamoja na mambo mengine, katika sherehe hizo Mhe. Dkt. Samia alisema licha ya changamoto za uviko 19 zilizoikumba Dunia kwa ujmla, uchumi wa Tanzania umeendelea kuwa himilivu. “mfano kwa mwaka 2022 pato la taifa limekua kwa asilimia 4.7 ukilinganisha na asilimia 4.3 mwaka 2021, na kwa mwaka 2023 tunategemewa utaongezeka na kufikia asilimia 5,” alisema Dkt. Samia

Rais pia aliwaeleza Mabalozi kuhusu utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa na Serikali ambapo alisema kuwa kuanzia Julai mpaka Novemba 2022 Miradi imeongezeka na kufika 132 yenye thamani ya dola bilioni 3.16 za Marekani ambayo ni ongezeko la asilimia 22.2 ikilinganishwa na idadi ya miradi iliyosajiliwa kwa kipindi kama hicho kwa mwaka 2021.

“Mfano mzuri waheshimiwa mabalozi, Serikali inatarajia kukamilisha ujenzi wa Bwawa la Nyerere mwezi Juni mwaka 2024 likiambatana na miradi mingine mikubwa” Dkt. Samia alibainisha

Kadhalika, Rais Dkt. Samia akatoa wito kwa mabalozi wanazowakilisha nchi zao kuungana na Serikali kuhamisha ofisi zao katika Makao Makuu ya Serikali Jijini Dodoma.

“Mnafahamu kwamba Dodoma ndiyo makao makuu rasmi ya nchi yetu na Serikali imehamia huko na tunachukua kila hatua kuhakikisha linakuwa Jiji la kisasa lenye huduma zote muhimu. Tunawaomba mfanye mipango ya kuhamia Dodoma ili muweze kunufaika na fursa mbalimbali ambazo Serikali inatoa kabla ya kumaliza wakati wake,” aliongeza Rais Dkt. Samia.

Awali, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax aliwaeleza Mabalozi na Wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa kuwa Tanzania itaendelea kuimarisha uhusiano wake na nchi zao kila wakati kwa maslahi mapana ya pande zote mbili.

“Napenda kuwahakikishia kuwa Serikali ya awamu ya Sita chini ya Uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan itaendelea kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia na nchi na Mashirika mnayoyasimamia kila wakati kwa maslahi mapana ya pande zote mbili,” alisema Dkt. Tax 

Kwa upande wake kiongozi wa Mabalozi nchini ambaye pia ni Balozi wa Visiwa vya Comoro nchini, Mhe. Dkt. Ahmada El Badaoui Mohamed aliahidi kuwa wataendelea kushirikiana na Serikali katika kuhakikisha inafikia malengo yake iliyojiwekea kwa mwaka 2023.

 

  • Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akiongea na Mabalozi wanaoziwakilisha nchi zao hapa nchini pamoja na Wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa (hawapo pichani) katika Sherehe za Mwaka Mpya 2023 kwa Mabalozi (Diplomatic Sherry Party) iliyofanyika Ikulu tarehe 13 Januari 2023 Jijini Dar es Salaam
  • Sehemu ya Mabalozi na Wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa pamoja na Menejimenti ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki wakiwa katika Sherehe za Mwaka Mpya 2023 kwa Mabalozi (Diplomatic Sherry Party) iliyofanyika Ikulu tarehe 13 Januari 2023 Jijini Dar es Salaam
  • Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akiongea na Mabalozi wanaoziwakilisha nchi zao hapa nchini pamoja na Wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa katika Sherehe za Mwaka Mpya 2023 kwa Mabalozi (Diplomatic Sherry Party) iliyofanyika Ikulu tarehe 13 Januari 2023 Jijini Dar es Salaam
  • Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax akiongea na Mabalozi pamoja na Wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa (hawapo pichani) katika Sherehe za Mwaka Mpya 2023 kwa Mabalozi (Diplomatic Sherry Party) iliyofanyika Ikulu tarehe 13 Januari 2023 Jijini Dar es Salaam