Tanzania China za kubaliana kuendeleza Ushirikiano wa Kimkakati
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo, amekutana na kufanya mazungumzo ya pande mbili na mgeni wake, Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Watu wa China, Mhe. Wang Yi, na kukubaliana kuendelea kuimarisha ushirikiano wa kimkakati, katika kikao kilichofanyika jijini Dar es Salaam.
Katika kikao hicho, viongozi hao wawili walijadili kwa kina masuala mbalimbali ya ushirikiano wa kihistoria na kimkakati kati ya Tanzania na China, hususan katika nyanja za kisiasa, kiuchumi na kijamii na kusisitiza umuhimu wa kuendelea kuimarisha uhusiano wa kindugu uliojengwa katika misingi ya kuheshimiana na kuaminiana kwa manufaa ya pamoja kama ulivyo asisiwa na waasisi wa mataifa hayo.
Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo aliishukuru Serikali ya China kwa mchango wake mkubwa katika maendeleo ya Tanzania, hususan katika utekelezaji wa miradi ya kimkakati ya miundombinu, afya, elimu, nishati na viwanda. Ameeleza dhamira ya Serikali ya Tanzania ya kuendelea kushirikiana na Serikali ya China katika kuvutia uwekezaji, biashara na teknolojia kwa lengo la kukuza uchumi na kuboresha maisha ya wananchi.
Kwa upande wake, Mhe. Wang Yi ameeleza utayari wa China wa kuendelea kuiunga mkono Tanzania katika juhudi zake za maendeleo, na kusisitiza kuwa China itaendelea kuwa mshirika wa kuaminika wa Tanzania na Afrika nzima katika kutekeleza ajenda za maendeleo ya pamoja, ikiwemo kupitia Mpango wa Ukanda wa njia (Belt and Road Initiative) na Jukwaa la Ushirikiano wa Afrika na China (FOCAC).
Mbali na hayo viongozi hao walijadili kuhusu masuala ya kikanda na kimataifa, na kusisitiza umuhimu wa kuimarisha mshikamano wa nchi zinazoendelea, kudumisha amani na usalama, pamoja na kukuza mfumo wa kimataifa unaozingatia usawa na haki.
Ziara ya Mhe. Wang Yi nchini inaendelea kudhihirisha dhamira ya Tanzania na China ya kuimarisha zaidi ushirikiano uliodumu kwa muda mrefu kwa manufaa ya wananchi wa pande zote mbili.