NAIBU WAZIRI CHUMI AIPONGEZA NJE SPORTS KWA KUSHIKA NAFASI YA TATU SHIMIWI
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Cosato Chumi (Mb.) amewapongeza wanamichezo wa timu ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki (Nje - Sports), kwa kufanya vizuri na kushika nafasi ya tatu katika michezo ya SHIMIWI iliyomalizika Mkoani Morogoro tarehe 5 Octoba, 2024.
Mhe. Chumi pia alimpongeza Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt. Samweli Shelukindo kwa kuwa hamasa na mstari wa Mbele kwenye michezo Wizarani .
Waziri Chumi ametoa pongezi hizo alipopokea Kombe la Mshindi wa Tatu katika hafla fupi iliyofanyika katika Ofisi ndogo za Wizara jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki anayeshughulikia masuala ya Afrika Mashariki Mhe. Dennis Londo.1
“Nitumie nafasi hii kukupongeza Katibu Mkuu kwasababu nyie wote mnaona eeh kwakuwa michezo za kazi inategemeana na kiongozi ana hamasa kiasi gani na michezo, kama hana hamasa, michezo utaisikia tuu, lakini kwa kweli Katibu Mkuu kwenye hili tokea nimefika hapa nimefarijika sana, mimi mwenyewe ni mwanamichezo na Mhe. Londo nae ni mtu wa Michezo na wewe mwenyewe mtu wa michezo kwakweli imetupa faraja,” amesema Mhe. Chumi.
Naye Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki anayeshughulikia masuala ya Afrika Mashariki Mhe. Denis Londo (Mb.) alitoa salamu za pongezi kwa wanamichezo wa Wizara kutoka kwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe, Thabiti Kombo (Mb.).
Mhe. Londo pia alimpongeza Katibu Mkuu Dkt. Shelukindo kwa namna anavyokuwa karibu na wanamichezo Wizarani na hata wanavyoenda kwenye mashindano ameendelea kuwapa hamasa ili wafanye vizuri.
“Katibu Mkuu Balozi Shelukindo nikupe pongezi kwa kuwalea vijana hawa, umekuwa mtu muhimu sana kwao, nimepata mrejesho huo nilipoenda watembelea wakiwa kwenye mashindano, umekuwa ukiwapigia simu kila siku kuwajulia maendeleo yao na kwakweli ukaribu wako kwao umekuwa chanzo cha wao kufanya vizuri kwenye Michezo ya SHIMIWI, naomba Uendelee hivyo,” alisema Mhe. Londo
Mhe. Londo alitoa rai kwa viongozi wa Wizara kuendelea kuona umuhimu wa michezo kwa wafanyakazi kwa kuwa michezo inasaidia kujikinga na magonjwa yasiyoambukiza na ndio sehemu ambayo Mtumishi anapata kujuana na watumishi wenzie.
Kwa upande wa Katibu Mkuu Balozi Dkt. Shelukindo hakusita kuonesha furaha yake kwa namna Manaibu Waziri walivyoweza kutenga muda wao na kuja kujumuika pamoja na Wachezaji ambao walikuja kukabidhi Kombe la Mshindi wa Tatu kwenye mchezo wa Mpira wa Miguu SHIMIWI.
Nje – Sports ilishika nafasi ya Tatu baada ya kuichapa Timu ya Ikulu kwa Mikwaju ya penati.
Katibu wa Michezo Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bi. Pili Sukwa ameushukuru uongozi na Menejimenti ya Wizara kwa namna walivyofanikisha Wanamichezo hao kushiriki Michezo ya SHIMIWI Mkoani Morogoro.