MKURUGENZI MTEULE WA SHIRIKA LA AFYA DUNIANI KANDA YA AFRIKA
Mkurugenzi Mteule wa Shirika la Afya Duniani Kanda ya Afrika, Dkt. Faustine Ndugulile; afanya kikao na Waziri-Afya, Wabunge na Mabalozi, Atoa neno la Shukrani
Brazzaville, Congo
29 Agosti 2024
Mkurugenzi mteule wa Shirika la Afya Duniani (WHO) Kanda ya Afrika, Dkt. Faustine Ndugulile, amekutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Afya, Mhe. Jenista Mhagama pembezoni mwa Mkutano wa 74 wa Shirika la Afya Duniani Kanda ya Afrika, unaoendelea Jijini Brazaville, Congo.
Kwenye Mkutano huo uliohudhuriwa pia na Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mabalozi na Maafisa Waandamizi wa Wizara za Afya na Mambo ya Nje, Dkt. Ndugulile ametoa shukrani za dhati kwa kuhitimiisha salama Kampeni za Uchaguzi na kupata ushindi mnono kwa Tanzania. Aidha kupitia mkutano huo amewaahidi watanzania kuto kuwaangusha.
Kwa upande wake, Waziri wa Afya ambaye ndiye aliyepiga kura ya Tanzania kwenye uchaguzi huo uliofanyika tarehe 27 Agosti 2024, amempongeza tena na kumsihi kujipanga vizuri na timu mahiri kwa kazi kubwa iliyopo mbele yake ya kuhudumia Bara la Afrika. Aliongeza kuwa nchi ipo nyuma yake ili kuhakikisha malengo na maono yake kwa taasisi hiyo kubwa ya kimataifa yanafikiwa.
Wakati huo huo, Dkt. Ndugulile alifanya pia mazungumzo na Balozi anayeiwakilisha Tanzania nchini Congo, mwenye makazi yake Kinshasa, DRC, Mhe. Balozi Saidi Mshana, aliyeongozana na Balozi Mindi Kasiga, Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, katika ofisi zake za muda kwa lengo la kutoa shukrani za dhati kwa Jumuiya ya Wanadiplomasia.
Kwenye mazungumzo yake na Balozi Mshana, ambaye ndiye atakayekua mwenyeji wake kwa kipindi cha miaka mitano au kumi cha uongozi wake kwenye taasisi hiyo yenye Makao yake makuu Jijini Brazaville, Dkt Ndugulile alimshukuru yeye binafsi kwa ushirikiano na utayari wake muda wote wa kampeni kwa kuweza kuratibu uwasilishwaji wa nyaraka mbalimbali muhimu kwenye taasisi hiyo.
Aidha Dkt. Ndugulile aliongeza Shukran nyingi kwa msaada na uungwaji mkono alioupata kutoka kwa Jumuiya ya Wanadiplomasia, hususan wa Kanda ya Afrika waliopo kwenye eneo la uwakilishi la Balozi Mshana, ambao walimsaidia kufanikisha ushindi wake kama Mkurugenzi wa WHO Kanda ya Afrika.
Aidha, aliwaomba Balozi Mshana na Balozi Kasiga wafikishe salamu zake za shukrani kwa mabalozi wote wanaoiwakilisha Tanzania duniani, kwa ushiriki wao katika kampeni hiyo muhimu na ya kihistoria kwake yeye, kwa Tanzania na Afrika Mashariki, kwani kwa kipindi cha miaka sabini cha taasisi hiyo, nafasi hiyo haijawahi kushikwa na Mtanzania wala na Mwananchi kutoka nchi yoyote ya Ukanda wa Afrika Mashariki.
Mwanzoni mwa mwezi Mei, 2024, Dkt. Faustine Ndugulile alijitosa kwenye kinya’ang’anyiro hicho baada ya Mhe. Rais Dkt. Samia kuridhia na kumpendekeza kama mgombea wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwenye nafasi hiyo nyeti kushinda zote kwenye sekta ya Afya.
Kwenye mchuano mkali uliohusisha nchi tatu nyingine za Senegal, Niger na Rwanda, Tanzania iliibuka mshindi kwa kupata kura 25 na kuwaacha mbali Senegal (14) na Niger (6) katı ya kura 45 zilizopigwa na Mawaziri wa Afya wa nchi wanachama wa Shirika la Afya Duniani.
Licha ya hiatoria iliyoandikwa na Tamzania kupitia kampeni za uchaguzi wa Dkt. Ndugulile, yeye amekua mgombea pekee aliyenadi maono yake kwa kujumuisha changamoto za kiafya za pamoja zinazoikumba Afrika
Mkurugenzi Mteule Dkt. Faustine Ndugulile, anatarajiwa kuanza kazi rasmi Frebruari 2025, baada ya kuthibitishwa na Baraza Kuu la Shirika la Afya Duniani Januari 2025.
Mwisho