MHE. ANNE MAKINDA ARIDHISHWA NA UCHAGUZI MKUU WA NAMIBIA ASEMA ULIKUWA WA AMANI NA UTULIVU
Spika wa Zamani wa Bunge la Jamhuri ya Muungano la Tanzania na Mkuu wa Misheni ya Uangalizi wa Uchaguzi Mkuu wa Namibia; ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC-SEOM), Mhe. Anne Semamba Makinda, ameelezea kuridhishwa na uchaguzi mkuu wa Namibia uliofanyika tarehe 27 Novemba, 2024 na kukamilika mapema leo tarehe 28 Novemba 2024, ambapo ulikuwa wa amani na utulivu.
Mhe. Makinda ameyasema hayo katika ufunguzi wa vituo vya kupigia kura, ambapo alishuhudia zoezi la upigaji kura katika kituo cha A-Shipena Sekondari kilichopo katika jimbo la John A. Pandemi lililopo katika mkoa wa Khomas nchini Namibia.
Mhe. Makinda amesema kwa vituo kadhaa alivyovitembelea mkoani Khomas hadi usiku wa kuamkia leo, vimeonesha mazingira ya utulivu, amani na usalama kwa wapigakura wote kwani walikuwa wamejipanga mistari pasipo na fujo, wakisubiri kuitwa kwa zamu, ili wakapige kura.
“Nimefurahishwa kuona utulivu wa namna hii na uvumilivu walionao wapiga kura wa rika zote, hususani vijana, kwani hatua hiyo imewawezesha kutekeleza wajibu wao wa kikatiba na kidemorasia.” Alifafanua Dkt. Makinda.
Mhe. Makinda aliambatana na Timu ya SADC-SEOM, Sekrekatariati ti ya SADC na wajumbe wa SADC Troika inayomsaidia Mkuu wa SEOM Mhe. Anne Makinda, kutekeleza majukumu yake.
Vituo vilivyotembelewa ni pamoja na Single Quarter Police Station (Katutura Center), Shule ya Msingi ya Suiderhof (Vanduk East), Mix Settlement A (Windhoek Rural) na Windhoek Municipality (Windhoek East).
Vituo vingine vya uchaguzi ambavyo Mhe. Makinda na ujumbe wake walitembelea ni Omeya Golf Estate (Windhoek Rural), Shule ya Msingi ya Groot Aub A na Goot Aub B pamoja na Luiyo Parii Valley, katika jimbo la Windhoek.
Mhe, Makinda pia alishiriki katika zoezi la ufungaji vituo vya uchaguzi ambalo lilitakiwa kukamilika saa tatu jana, badala yake kwa idhini ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi ya Namibia (ECN) kutokana na wingi wa wapigakura kwa baadhi ya vituo, wapigakura waliruhusiwa kuendelea na zoezi hilo mpaka wapigakura wote watakapokamilika na hivyo kusababisha zoezi hili kukamilika leo.
Tume ya Uchaguzi nchini Namibia inatarajia kutangaza matokeo ya uchaguzi Mkuu wa Rais na Wabunge mara baada ya kazi inayoendelea ya kuhesabu kura kukamilika na kuthibitishwa.
Kwa sasa Vituo mbalimbali vya Uchaguzi nchini Namibia vinaendelea na kazi ya kuhesabu kura na kubandika matokeo ya awali katika mbao za matangazo za vituo hivyo kwa manufaa ya wapiga kura na wanachi kwa ujumla.