KAMALA AWASILI NCHINI
Makamu wa Rais wa Marekani, Mhe. Kamala Harris amewasili nchini tarehe 29 Machi, 2023 kuanza ziara yake ya kikazi ya siku tatu kuanzia tarehe 29 hadi 31 Machi, 2023.
Mara baada ya kuwasili kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijiji Dar es Salaam Mhe. Kamala amepokelewa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Mpango.
Mhe. Kamala atapokelewa rasmi na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan atampokea Ikulu jijini Dar es Salaam tarehe 30 Machi 2023 ambapo mapokezi hayo yatafuatiwa na mazungumzo ya kuimarisha ushirikiano wa pande mbili baina ya viongozi hao.
Vilevile, akiwa nchini, Mhe. Kamala ataweka shada la maua katika Makumbusho ya Taifa Jijini Dar es Salaam kama ishara ya kuwakumbuka wahanga wa mabamu yaliyolipuliwa kwenye Ubalozi wa Marekani, Dar es Salaam mwaka 1998.
Pia atatembelea Taasisi ya Tanzania Startup Association ya Jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kukutana na Wajasiriamali Vijana pamoja nakushiriki Futari iliyoandaliwa kwa heshima yake na Mwenyeji wake Mhe. Dkt. Rais Samia.
Katika ziara hii Mhe. Kamala amefuatana na mwenza wake Mhe. Doug Emhoff pamoja na Viongozi mbalimbali wa Serikali ya Marekani.
Mapokezi ya Mhe. Kamala yameongozwa na Mhe. Dkt. Mpango na kumshirikisha Mama Mbonipa Mpango pamoja na viongozi mbalimbali wa Serikali akiwemo Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax, Waziri wan chi, Ofisi ya Rais-Zanzibar, Mhe. Jamal Kassim Ali, Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara, Mhe. Ashatu Kijaji, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Fedha na Mipango, Dkt. Saada Mkuya na Mkoa wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mhe. Amos Makalla