CHINA YATOA USD 50 BILIONI KUSAIDIA MAENDELEO AFRIKA
• Asisitiza kutoingilia masuala ya ndani ya nchi • Ahaidi hakuna Taifa likakalosalia nyuma katika safari ya maendeleo • Ataja vipaumbele 10 vya ushirikiano wa kimkakati na Afrika Rais wa Jamhuri ya Watu wa China Mheshimiwa Xi Jinping ametangaza kutoa kiasi cha dola za Marekani bilioni 50 zitakazo elekezwa kusaidia masuala mbalimbali ya maendeleo ya kijamii na kiuchumi kwa mataifa ya barani Afrika. Ahadi hiyo imetolewa leo tarehe 5 Septemba 2024 alipokuwa akitoa hotuba ya ufunguzi wa Mkutano wa Kilele wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jukwaa la Ushirikiano kati ya China na Afrika (FOCAC) jijini Beijing. Akifungua mkutano huo Rais Xi Jinping ameeleza kuwa kiasi hicho kitaelekezwa katika sekta mbalimbali kwa lengo la kuchagiza maendeleo ya pande zote mbili bila kuathiri misingi na taratibu za Taifa husika. Aidha, aliongeza kusema kwamba kiasi hicho cha fedha kitaelekezwa katika maeneo kumi (10) ya kipaumbele ya ushirikiano wa kimkakati na Afrika. Aliendelea kwa kuhimiza umuhimu wake katika kuleta mageuzi ya kiuchumi na usasa huku akisisitiza kuwa hakuna Taifa litakalo baki nyumba katika maendeleo hayo. Rais Xi Jinping ameyataja maeneo hayo ya ushirikiano wa kimkakati kuwa ni ubia katika ushirikiano wa maendeleo (partnership action for development cooperation), Afya (partnership action for health), kilimo na ustawi (partnership action for agriculture and livelihood), mwingiliano wa watu na watu (partnership action for people to people exchanges), maendeleo ya kijani (partnership action for green development) na masuala ya ulinzi na usalama (partnership action for common security). Maeneo mengine yaliyoainishwa ni ushirikiano katika viwanda (partnership action for industrial chain cooperation), mawasiliano (partnership action for connectivity), ubia katika kukuza biashara (partnership action for trade prosperity) na ubia katika mafunzo (Partnership Action for Mutual Learning among Civilizations). Aidha Rais Xi Jinping amefafanua kuhusu mgawanyo wa dola za Marekani bilioni 50 zitakazotolewa kama ifuatavyo, bilioni 29 zitaelekezwa katika mikopo, bilioni 11 zitaelekezwa kwenye misaada ya aina mbalimbali na bilioni 10 zitaelekezwa katika uwekezaji kupitia makampuni ya China yatakayoenda kuwekeza katika Nchi mbalimbali barani Afrika. Ni zama mpya za ushirikiano na usasa kati ya China na Afrika, ushirikiano na urafiki wetu uliodumu katika miongo mingi na kuleta aina mpya ya ubia na ushirikiano katika jumuiya ya mataifa sasa tumefanikiwa kufika katika hatua ya juu ya ushikiano wa kimkakati. Nawahakikishia ninyi wote ndugu na marafiki zangu tuliokusanyika hapa kuwa hakuna Taifa lolote litakalo salia nyuma katika safari hii ya usasa (modernization). Ameeleza Rais Xi Jinping. Mbali na hayo Rais Xi Jinping ametaja hatua kadhaa zinazotarajiwa kuchukuliwa na Serikali yake katika kipindi cha miaka 3 ijayo (2025-2027) katika kufikia adhima yake ya kusaidia kuleta mageuzi ya maendeleo na usasa barani Afrika ikiwemo utekelezaji wa miradi 30 ya nishati safi, miradi 30 ya mawasiliano, programu 500 za kilimo cha kisasa na kutoa fursa 60,000 za mafunzo hasa kwa vijana na wanawake. Katika hatua nyingine, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan amehutubia mkutano huo ambao ulipata mwitikio mkubwa kutoka kwa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Afrika, viongozi na watendaji kutoka Taasisi na Mashirika mbalimbali ya Kikanda na Kimataifa, huku ukifuatiliwa na mamilioni ya watu kote duniani. Rais Samia amehutubia mkutano huo akiwakilisha kanda ya Afrika Mashariki. Katika hotuba yake Rais Samia ameeleza kuhusu umuhimu wa ushikirikiano wa kimkakati katika kuchagiza maendeleo na kutoa wito kwa pande zote mbili kuendelea kuunganisha nguvu ili kuongeza kasi ya ukuaji wa uchumi kwa manufaa ya wananchi wa pande zote mbili. Marais wengine kutoka Afrika waliohutubia mkutano huo ni pamoja na Mheshimiwa Matamela Cyril Ramaphosa wa Afrika Kusini, Mheshimiwa Bassirou Diomaye Faye wa Senegal, Mheshimwa Mohamed Ould Ghazouani wa Mauritania, Mheshimiwa Denis Sassou Nguesso wa Jamhuri ya Congo na Mheshimiwa Bola Ahmed Adekunle Tinubu wa Nigeria.