Skip to main content
News and Events

Waziri wa Mambo ya Nje China Awasili Nchini

Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama cha Kikomunisti cha China na Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Watu wa China, Mheshimiwa Wang Yi, amewasili Dar es Salaam, Tanzania, kwa ziara ya kikazi ya siku mbili kuanzia tarehe 9 hadi 10 Januari 2026.

Katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam Mheshimiwa Wang Yi amelakiwa na mwenyeji wake Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mheshimiwa Balozi Mahmoud Thabit Kombo (Mb), aliyeambatana na Naibu Mawaziri wake Mhe. Dkt. Ngwaru Maghembe na Mhe. James Milya, pamoja na Katibu Mkuu Balozi Dkt. Samwel Shelukindo na viongozi wengine wa Serikali

Ziara hiyo inalenga kuimarisha zaidi uhusiano na ushirikiano wa kimkakati kati ya Tanzania na China.

Vilevile, inalenga kukuza ushirikiano kwa kuendeleza uhusiano wa kiuchumi na kuangazia fursa mpya za ushirikiano katika maeneo yenye maslahi ya pamoja.

Akiwa nchini Mheshimiwa Wang Yi atakuwa na mazungumzo na mwenyeji wake Mheshiniwa Balozi Mahmoud Thabit Kombo yatakayolenga kuendeleza na kuimarisha uhusiano wa kimkakati kati ya Tanzania na China

Mheshimiwa Wang Yi pia atakutana na Rais wa Jamhuri  ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan Ikulu jijini Dar es Salaaam ambako pia atawasilisha salamu maalum kutoka kwa Rais wa China Mheshimiwa Xi Jinping

Tanzania na China zimekuwa zikishirikiana katika maeneo mbalimbali ikiwemo biashara na uwekezaji, ambapo kwa mwaka 2024 thamani ya biashara kati ya Tanzania na China ilifikia takriban dola za Marekani bilioni 5.2. Kampuni za China pia zimeendelea kuwekeza nchini katika sekta za viwanda, kilimo, huduma, usafirishaji, mawasiliano na utalii. Kwa mwaka 2025, Mamlaka ya Uwekezaji na Maeneo Maalum ya Kiuchumi Tanzania (TISEZA) ilisajili miradi ya China 343 yenye thamani ya dola za Marekani bilioni 3.1 na kuzalisha ajira 82,404.