Skip to main content
News and Events

AKATIBU WAKUU WANAOSIMAMIA SEKTA YA NISHATI WA AFRIKA MASHARIKI WAKUTANA JIJINI ARUSHA

Makatibu Wakuu wanaosimamia Sekta ya Nishati katika Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) wamekutana jijini Arusha katika mkutano wa 16 wa Baraza la Mawaziri la Kisekta la Nishati la EAC unaoendelea jijini humo.

Mkutano huo ambao ulitanguliwa na mkutano wa Wataalam uliyofanyika tarehe 12 Februari 2024, umepitia na kujadili utekelezaji wa maamuzi na maelekezo ya Baraza la Mawaziri la Jumuiya. Vilevile umepokea na kujadili taarifa za maendeleo ya sekta ya nishati katika maeneo ya umeme, mafuta na nishati jadidifu. 

Katika hotuba yake ya ufunguzi, Mwenyekiti wa Mkutano huo ambaye pia ni Katibu Mkuu anayesimamia masuala ya Afrika Mashariki katika Jamhuri ya Kenya Bw. Abdi Dubati ameeleza kuwa mkutano huo ni mwendelezo wa jitihada za Wakuu wa Nchi wanachana wa Jumuiya, za kuhahikisha sekta ya nishati inaimarika ili kuchagiza maendeleo ya Jumuiya kutokana na mchango wake mkubwa katika kuvutia wawekezaji, kukuza biashara na uzalisha wa bidhaa viwandani.

“Nitoe rai kwetu sote tuliopata nafasi na kuaminiwa kusimamia maendeleo ya sekta hii muhimu kuwa tujidhatiti katika kutoa michango na kushirikishana uzoefu wetu ili kwa pamoja kama Jumuiya tupige hatua katika upatikanaji wa nishati ya kutosha, endelevu na salama kwa maendeleo ya Jumuiya yetu”. Alisema Dubati. 

Kwa upande wake kiongozi wa ujumbe wa Tanzania kwenye mkutano huo ambaye pia ni Katibu Mkuu Wizara ya Nishati Mhandisi Felchesmi Mramba akizungumza kwenye ufunguzi wa mkutano huo ameleeza kuwa kikao hicho kinatoa fursa ya kuunganisha nguvu na kuweka mikakati ya pamoja katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya nishati ikiwemo umeme. 

Vilevile alitoa wito kwa washiriki wa mkutano huo kutumia fursa ya kuwepo jijini humo kutembelea vivutio mbalimbali vya utalii. 

Makatibu Wakuu wengine kutoka Tanzania walioshiriki katika mkutano huo wa 16 wa Baraza la Mawaziri la Kisekta la Nishati wa Jumuiya ya Afrika Mashariki ni Balozi Stephen P. Mbundi wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki na Bw. Joseph Kilangi Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Nishati na Madini, Zanzibar.

  • Katibu Mkuu Wizara ya Nishati Mhandisi Felchesmi Mramba akichangia hoja kwenye Mkutano wa 16 wa Baraza la Mawaziri la Kisekta la Nishati wa Jumuiya ya Afrika Mashariki ngazi ya Makatibu wakuu uliofanyika jijini Arusha.
  • Sehemu ya washiriki kutoka nchi wanachama wakifuatilia mkutano wa Mkutano wa 16 wa Baraza la Mawaziri la Kisekta la Nishati wa Jumuiya ya Afrika Mashariki ngazi ya Makatibu wakuu uliofanyika jijini Arusha.
  • Meza Kuu wakiongoza mkutano wa 16 wa Baraza la Mawaziri la Kisekta la Nishati wa Jumuiya ya Afrika Mashariki ngazi ya Makatibu wakuu uliokuwa ukiendelea katika Makao Mkuu ya Jumuiya jijini Arusha.
  • Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki anayesimamia masuala ya Afrika Mashariki Balozi Stephen P. Mbundi akijadili jambo na Mkurugenzi wa Idara ya Miundombinu ya Uchumi na Huduma za Jamii katika Wizara ya Mambo ya Nje Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhandisi Abdillah Mataka.
  • Sehemu ya ujumbe wa Tanzania wakifuatilia mkutano wa Mkutano wa 16 wa Baraza la Mawaziri la Kisekta la Nishati wa Jumuiya ya Afrika Mashariki ngazi ya Makatibu wakuu uliofanyika jijini Arusha.
  • Mkutano ukiendea