WIZARA YA MAMBO YA NJE YASHIRIKI MAONESHO YA WIKI YA UTUMISHI WA UMMA
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki imeungana na Wizara na Taasisi mbalimbali za serikali kushiriki katika maonesho ya Wiki ya Utumishi wa Umma yanayofanyika katika Viwanja vya Chinangali jijini Dodoma.
Maonesho hayo yaliyofunguliwa rasmi leo Juni 17, 2025 na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Goerge Simbachawene (Mb) yatafanyika kwa siku 7 kuanzia tarehe 16 – 23 Juni 2025 huku yakiongozwa na kauli mbiu isemayo “Himiza matumizi ya mifumo ya kidigiti ili kuongeza upatikanaji wa taarifa na kuchagiza uwajibikaji”.
Akifungua maonesho hayo Waziri Simbachawene ametoa wito kwa Wizara na Taasisi zote za Serikali kuhakikisha zinatumia mifumo ya TEHAMA ili kurahisisha upatikanaji wa huduma, vilevile kuwapunguzia wananchi mzigo wa gharama za kupata huduma kutoka serikalini.
Mbali na hayo Waziri Simbachawene alitoa wito kwa watumishi na wananchi kwa ujumla kuwa na mwamko wa kutumia mifumo ya TEHAMA inayoanzishwa na taasisi za umma, huku akihimiza kuwa mifumo hiyo kwasasa kwa kiasi kubwa inasomana.
“Kunafaida nyingi kwa wananchi kutembelea katika maonesho haya, licha ya kupata ufafanuzi wa shughuli za Wizara na Taasisi wanaweza kupata huduma mbalimbali kutokea mahali hapa (Chinangali Park), mfano, nimetembelea banda la Wizara ya Ardhi nimeelezwa kuwa zaidi ya hati 5 za viwanja tayari zimetolewa kwa wananchi katika siku hizi mbili” alisema Waziri Simbachawene.
Waziri Simbachawene alihitimisha hotuba yake kwa kuwataka wananchi wa Dodoma na maeneo ya jirani kujitokeza kwa wingi katika maonesho hayo ambayo yatafungwa tarehe 23 Juni 2025 ili waweze kupata huduma za papo kwa papo na taasisi zinazoshiriki ikiwa ni pamoja na kupata hati za viwanja, vitambulisho vya taifa na kupima afya.
Wizara inashiriki maonesho hayo pamoja na Taasisi zilizopo chini yake za AICC, Kituo cha Uhusiano wa Kimataifa cha Dkt. Salim Ahmed Salim na Mpango wa Afrika Kujitathimini Kiutawala Bora (APRM-Tanzania).