Skip to main content
News and Events

WAZIRI MULAMULA AZINDUA MASHINDANO YA KIMATAIFA YA BAISKELI TANZANIA JIJINI DAR

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula (Mb) leo Septemba 28, 2021 amezindua Mashindano ya Kimataifa ya Baiskeli Tanzania (Tanzania International Cycle Tour) jijini Dar es Salaam. Mashindano haya ambayo yatafanyika sambamba na Maadhimisho ya miaka 60 ya Uhuru wa Tanzania yanalenga kutambua mchango wa Tanzania katika kupigania Ukombozi wa Nchi za Kusini mwa Afrika na kusherekea mafanikio yaliyofikiwa na Tanzania katika demokrasia, amani na utulivu wakisiasa tokea kupata Uhuru kiasi cha kuwa mfano wa kuigwa katika Bara la Afrika.

Akizungumza katika ufunguzi wa mashindano hayo Waziri Mulamula ameeleza imani yake kuwa kupitia mashindano hayo yakipekee ujumbe wa Mshikamano na Umoja ambao unabeba dhana nzima ya Maadhimisho ya miaka 60 ya Uhuru utawafikia watu wengi zaidi. Aidha ametumia nafasi hiyo kutoa Wito kwa Taasisi zingine kutoka Nchi Wanachama wa Afrika Mashariki kuiga jambo lililofanywa na waandaaji wa Shindano hili ambao ni Taasisi ya Afrika Mashariki Fest na Taasisi ya Utalii wa Utamaduni Butiama. 

“Tunaamini pia baada ya mashindano haya mtakuwa mabalozi wazuri wa Tanzania kwa kuwa mkiwa huko njiani wakati wa mashindano mnaenda kujionea mabaliko makubwa  ya maendeleo kijamii na kiuchumi na mafanikio makubwa yaliyofikiwa na Nchi yetu katika nyanja mbalimbali” alieleza Waziri Mulamula

Mheshimiwa Tabia Maulid Mwita Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar akizungumza katika ufunguzi huo amesema, amefarijika sana namna vijana kutoka nchini, Jumuiya Afrika Mashariki na nchi nyingine nje ya Jumuiya walivyohamasika kushiriki katika Mashindano haya. Aliendelea kueleza hiki ni kielelezo tosha kuwa vijana wanatambua na kudhamini uhuru wao sambamba na kudhamini jitihada zinazofanywa na Serikali yao katika kuleta maendeleo. 

Kwa upande wake Mkurugenzi na Mwanzilishi wa Taasisi ya Utalii wa Utamaduni Butiama Bw. Godfrey Madaraka Nyerere ameeleza kuwa pamoja na mambo mengine mashindano haya yanaenda kuionesha dunia hatua kubwa ya maendeleo iliyofikiwa nchini katika ujenzi wa miundiumbinu ya uchukuzi hivyo kuleta mchango mkubwa katika kutangaza Utalii sambamba na kuvutia Uwekezaji kutoka Nje. 

Katika hafla hiyo ya ufunguzi wa Mashindano pamoja na washiriki wengine yalihudhuriwa na Mhe. Tabia Maulid Mwita Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Mabalozi na Wanadiplomasia kutoka Nchi Wanachama wa Afrika Mashariki wanaoziwakilisha Nchi zao hapa nchini, Bw. Kisembo Ronex Tendo Mtendaji Mkuu wa Afrika Mashariki Fest kutoka nchini Uganda na Bw. Godfrey Madaraka Nyerere Mkurugenzi na Mwanzilishi wa Taasisi ya Utalii wa Utamaduni Butiama.

  • Mtendaji Mkuu wa Afrika Mashariki Fest kutoka nchini Uganda Bw. Kisembo Ronex Tendo akizungumza kwenye ufunguzi wa Mashindano ya Kimataifa ya Baiskeli Tanzania uliofanyika katika Ukumbi wa JNICC jijini Dar es Salaam
  • Wimbo wa Taifa ukipigwa kabla ya ufunguzi wa Mashindano ya Kimataifa ya Baiskeli Tanzania uliofanyika katika Ukumbi wa JNICC jijini Dar es Salaam
  • Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mheshimiwa Balozi Liberata Mulamula (Mb) akiwa kwenye ufunguzi wa Mashindano ya Kimataifa ya Baiskeli Tanzania uliofanyika katika Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam
  • Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mheshimiwa Balozi Liberata Mulamula (Mb) akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya waandaaji wa Mashindano ya Kimataifa ya Baiskeli Tanzania.