Skip to main content
News and Events

UN Yawaenzi Walinzi Wake wa Amani

Umoja wa Mataifa,  jana Mei 19 umefanya  hafla  maalumu ya  siku ya Kimataifa ya  Walinzi wa Amani  wanaohudumu  katika Misheni mbalimbali za Kulinda Amani chini  ya kofia ya  Umoja wa Mataifa.

Katika hafla hiyo  jumla ya walinzi 129  wanajeshi na  polisi waliopoteza maisha  mwaka  jana  kwa kushambuliwa na  makundi ya wapiganaji wenye silaha, matukio ya kigaidi, ajali na kuumwa walikumbukwa  na kuenziwa kwa mchango wao.

Miongoni mwa Mashujaa hao 129 kutoka  nchi  50, wapo mashujaa watatu kutoka Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Mashujaa hao ni  Sgt. Musa Abdrahamani Yusuf, Cpl. John Leornad Mkude na Pte. Juma Ally Khamis. 

Hafla  hiyo maalum ya kutambua mchango wa walinzi  hao  wa Amani na ambao wamejitolea maisha  yao kwaajili ya kuwalinda na kuokoka maisha ya wananchi wasiokuwa na hatia   katika  nchi zinazokabiliwa na vita na  migogoro ya wenyewenye  kwa wenyewewe iliongozwa na Katibu Mkuu wa  Umoja wa Mataifa,  Ban Ki  Moon.

Mwakilishi wa Kudumu wa  Tanzania katika Umoja wa Mataifa,  Balozi Tuvako Manongi,  ndiye aliyepokea medali maalum za mashuja hao watatu kwa niaba ya familia zao.  Medali waliyotunukiwa  mashujaa hao na  wengine inatambuliwa kama medali ya Dag Hammarskjold.

Hafla ya mwaka huu,   pamoja na  kutambua mchango wa mashujaa hao 129,  pia  ilitambua kwa namna ya pekee  na kwa mara ya kwanza,  mchango  na kujitolea wa hali ya juu  ulikofanywa na Kapteni  Mbaye Diagne raia ya  Senegal, aliyepoteza maisha mwaka 1994 wakati  akiokoa maisha ya  wanyarwada wakati wa  mauaji ya kimbali.

Kapteni Mbaye Diagne ameeziwa rasmi katika maadhimisho ya mwaka  huu kwa kupewa medali maalum iliyopewa  jina  la Medali ya  Mbaye Diagne, medali ambayo alikabidhiwa mjane wa Mbaye  Bibi Yacine Mar Diop  huku akishuhudiwa na watoto wake wawili.

Kapten Mbaye Diagne alikuwa mwangalizi wa Amani nchini Rwanda, kwa ushujaa mkubwa na bila ya kujali  hatari iliyokuwa ikimkabili  alitumia lori kuwaficha na kuwapeleka  mahali  salama mamia ya wanyarwada wakati wa mauaji ya kimbali ya Rwanda.

Kwa kutambua ushujaa na uthubutu wake huo, Baraza la Usalama lilibuni   mwaka 2014 medali ya  Kapten Mbaye Diagne ambayo  watakuwa  wanatunukiwa wanajeshi,  polisi na raia ambao wameonyesha uthubutu na ushupavu wa hali ya juu kiasi cha kupoteza maisha yao wakati wakitekeleza majukumu yao.

Akizungumza wakati wa halfa  hiyo ambayo  ilibeba majonzi ya  aina yake,  Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki Moon, alieleza kwamba,  hadi kufikia mwezi   wa nne mwaka huu, jumla ya walinzi wa Amani  3,400 wakiwamo  wanajeshi, polisi na raia walikuwa wamepoteza maisha  tangu kuanzishwa wa  shughuli za ulinzi wa Amani kwa  kofia ya Umoja wa Mataifa miaka 70 iliyopita.

“Wakati leo tunawaenzi na  kuwakumbuka mashujaa hawa 129 kutoka mataifa 50 waliopoteza maisha  yao mwaka jana  wakati wakitekeleza  jukumu la kuwalinda  wananchi wengine,  jana ( Mei 18) walinzi wengine watano wanaohudumu huko   Mali  wamepoteza maisha baada ya kushambuliwa”. Akasema Ban  Ki Moon kwa huzuni.

  • Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa Balozi Tuvako Manongi akiwa ameshika medali ya Dag Hammarskjold waliyotunukiwa mashujaa watatu watanzania ambao wamepoteza maisha mwaka jana wakati wakihudumu katika Misheni za kulinda Amani za Umoja wa Mataifa.