RAIS WA BURUNDI ATEMBELEA BANDARI KAVU – KWALA

RAIS WA BURUNDI ATEMBELEA BANDARI KAVU – KWALA

Rais wa Jamhuri ya Burundi Mhe. Evariste Ndayishimiye amewasili leo mchana katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam akitokea Zanzibar na kupokelewa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mhe. Amos Makalla. Mhe. Ndayishime ameambatana na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula (Mb).

Mara baada ya kuwasili jijini Dar es Salaam, Mhe. Ndayishimiye alielekea katika Stesheni ya Pugu na kapata taarifa fupi kuhusu mradi wa Reli ya Kisasa (SGR) inayojengwa kutoka Dar es Salaam – Morogoro, Morogoro – Makutupora na Mwanza – Isaka ikiwa ni jumla ya Kilomita 1063 za njia kuu na njia za kupishania.

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli, Bw. Masanja Kadogosa amemueleza Mhe. Ndayishimiye kuwa hadi sasa ujenzi wa SGR (kipande cha Pugu - Morogoro) umefikia asilimia 94 na kuwa unaendelea vizuri.

Aidha, mara baada ya kupata taarifa fupi kuhusu mradi wa ujenzi wa SGR, Mhe. Rais Ndayishimiye ametembelea bandari kavu eneo la Kwala Mkoani Pwani.

Mhe. Ndayishimiye amesema kuwa eneo la bandari kavu (Kwala) litakuza biashara kati ya Tanzania na Burundi na litatusaidia kupunguza gharama za usafiri na fedha zitakazookolewa zitaenda kwenye miradi mingine.

“Mradi huu pia utapunguza gharama za bidhaa mbalimbali Nchini Burundi, kwetu sisi Burundi, mtu akikupa eneo amekuthamini sawa na kukuunga undugu kwenye familia yake,” amesema Mhe. Ndayishimie.

Awali akitoa taarifa ya eneo hilo, Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Prof. Makame Mbarawa (Mb) amesema eneo hilo lina ukubwa wa hekta 502, kati ya hizo hekta 10 zimetengwa kwa ajili ya Serikali ya Burundi.

“Dhumuni la kutenga eneo hili ni kupunguza msongamano wa mizigo kutoka bandari ya Dar es Salaam,” Amesema Prof. Mbarawa na kuongeza kuwa ujenzi wa miundombinu ya eneo hili utakapokamilika utagharimu kiasi cha shilingi bilioni 37.23

Kwa upande wake Waziri wa Mambo ya NJe na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula (Mb) amesema kuwa kupitia mradi wa ujenzi wa bandari kavu eno la Kwala utasaidia kuimarisha uhusiano wa Tanzania na Burundi pamoja na ukanda wa Afrika Mashariki kwa ujumla.

  • Rais wa Jamhuri ya Burundi Mhe. Evariste Ndayishimiye pamoja na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula (Mb), Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Prof. Makame Mbarawa (Mb) na baadhi ya Mabalozi wakimsikiliza Mkurugenzi wa Shirika la Reli Tanzania Bw. Masanja Kadogosa alipokuwa akitoa taarifa fupi kuhusu maendeleo ya ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR) wakati Mhe. Ndayishimiye alipowasili leo katika Stesheni ya Pugu ikiwa ni muendelezo wa ziara yake ya kikazi ya siku tatu hapa nchini
  • Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula (Mb) akitoa hotuba yake kwa wananchi wa Kwala kabla ya mkaribisha Rais wa Jamhuri ya Burundi kuongea na wananchi wa eneo la Bandari Kavu (Kwala) mkoani Pwani
  • Rais wa Jamhuri ya Burundi Mhe. Evariste Ndayishimiye akihutubia wananchi wa Kwala wakati alipotembelea eneo la Bandari Kavu leo mkoani Pwani
  • Rais wa Jamhuri ya Burundi Mhe. Evariste Ndayishimiye pamoja na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula (Mb), Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Prof. Makame Mbarawa (Mb) na baadhi ya Mabalozi wakimsikiliza Mkurugenzi Mkuu wa Bandari ya Tanzania Bw. Eric Hamissi alipokuwa akitoa taarifa ya eneo la Bandari Kavu (Kwala) mkoani Pwani leo
  • Rais wa Jamhuri ya Burundi Mhe. Evariste Ndayishimiye akipokea nakala ya hati ya eneo lenye ukubwa wa hekta 10 zilizotengwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa ajili ya Serikali ya Burundi kutoka kwa Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Prof. Makame Mbarawa (Mb)