RAIS SAMIA, DKT. ADESINA WATEMBELEA BARABARA YA MZUNGUKO NA UWANJA WA NDEGE MSALATO
RAIS SAMIA, DKT. ADESINA WATEMBELEA BARABARA YA MZUNGUKO NA UWANJA WA NDEGE MSALATO
• Amshukuru Dkt. Adesina kwa kuwa Mbia wa Maendeleo wa Tanzania
• Barabara ya Mzunguko ya Dodoma kuitwa Adesina
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan akiambatana na Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) Dkt. Akinwumi Adesina wametembelea na kujionea maendeleo ya ujenzi wa Barabara ya Mzunguko wa nje wa Dodoma (outer ring roads) yenye urefu wa Km 112 na Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Msalato unaoendelea jijini Dodoma.
Katika ziara hiyo, Mheshimiwa Rais Dkt. Samia aliambatana na viongozi mbalimbali wa Serikali wakiongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule, Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne Mhe. Jakaya Kikwete, Waziri wa Ujenzi Mhe. Abdallah Ulega, Waziri wa Fedha Mhe. Mwigulu Nchemba na viongozi wengine waandamizi wa Serikali.
Ziara hiyo ilianzia katika eneo la Mtumba na kupita hadi Veyula na kuingia eneo la Msalato ambako ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Msalato ambao ni wa pili kwa ukubwa nchini baada ya Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA).
Ujenzi wa Uwanja wa Msalato utagharimu Shilingi Bilioni 370 na unatarajiwa kuwa wa Daraja F ambalo ni la juu linalotambulika Kimataifa ambapo kwa sasa wanakamilisha ujenzi wa daraja la NNE ambalo litahudumia abiria wapatao million moja na nusu
Akizungumza na wananchi katika eneo la Nala baada ya kumaliza kutembelea barabara na Uwanja wa Msalato, Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan alitumia fursa hiyo kumshukuru Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AFDB) anayemaliza muda wake Dkt. Adesina kwa kuwa mbia mkubwa wa Maendeleo ya Tanzania
“Ndugu zangu wana Dodoma, tumekutana hapa Leo hii kwa ajili ya Kutoa shukurani na kumuaga Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika anayemaliza muda wa utumishi katika benki hiyo,” alisema Rais Samia
Alisema anamshukuru Dkt. Adesina kwa Utumishi wake na upendo wake kwa Tanzania, ambapo Benki ya AFDB imekuwa mbia mkubwa katika safari ya maendeleo ya Tanzania kwa kutipatia fedha za mikopo nafuu, ambazo zimesaidia utekelezaji wa miradi ya ujenzi wa miundombinu nchini.
Alisema Utumishi wa Dkt. Adesina umeleta manufaa sio tu Tanzania bali kwa Afrika Nzima.
Rais Samia ameongeza kuwa ujenzi wa miundombinu ya barabara inalenga kuondoa msongamano katika jiji la Dodoma na kuleta urahisi wa kutoka eneo moja hadi lingine na kuongeza kuwa barabara ya mzunguko ya jijini Dodoma ni muhimu kwa Dodoma na Tanzania nzima huku wakilenga kuifungua zaidi Dodoma kwa njia za reli anga na barabara.
Amesema ujenzi wa Uwanja Msalato utaimarisha mitandao wa usafiri wa anga ndani na nje na hivyo kukuza utalii nchini Aliongeza kuwa asilimia 85 ya fedha za miradi wa Uwanja wa Msalato zinatoka benki ya AFDB na asilimia 15 inatolewa na Serikali ya Tanzania.