PROF. MKENDA AFUNGA MKUTANO WA ELIMU WA EAC JIJINI ARUSHA.
Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia Mhe. Prof. Adolf Mkenda amefunga rasmi Mkutano wa kwanza wa Elimu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na Maadhimisho ya mwaka wa elimu wa Umoja Afrika uliofanyika jijini Arusha.
Akizungumza katika hafla hiyo Prof. Mkenda amezitaka nchi wanachama kuandaa mpango kazi utakaoonesha namna bora ya kutekeleza maazimio yaliyotokana na mkutano huo ili kuhakikisha yanafanyiwa kazi kwa ukamilifu.
Pia ametaka kuhakikisha mafanikio yote yaliyopatikana katika maadhimisho ya mwaka wa elimu wa AU yanasherehekewa na kutafakari jinsi ya kuwa na mifumo bora zaidi ya utoaji elimu kwa vijana na hivyo baada ya miaka miwili mkutano ujao uone matunda ya mkutano huo.
Naye Mwenyekiti wa Baraza la Kisekta na Waziri wa Elimu na Mafunzo wa Sudan Kusini Mhe. Awut Deng Achuil alıtoa wito wa kuchukua hatua na kujitoa zaidi ili kuhakikisha malengo na maazimio ya mkutano yanatekelezwa kwa vitendo na ameipongeza Tanzania kwa kuwa mwenyeji pamoja na Sekretarieti ya EAC na nchi wanachama kwa kuandaa mkutano huo kwa mafanikio makubwa.
Mkutano huo wa kwanza na wa aina yake kufanyika katika ukanda wa Afrika Mashariki ulijumuisha wadau mbalimbali wa elimu kutoka Serikalini na sekta binafsi umejadili na kuweka mikakati mipya ya kukabiliana na fursa na changamoto zilizopo katika sekta ya elimu katika Jumuiya ya Afrika Mashariki na Bara la Afrika kwa ujumla. Kufanyika kwa mkutano huo ni utekekezaji wa maamuzi ya Mkutano wa 15 wa Baraza la Kisekta la Jumuiya ya Afrika Mashariki la Elimu, Sayansi na Teknolojia, Utamaduni na Michezo; na Umoja wa Afrika.