HATI TATU ZA MAKUBALIANO ZASAINIWA KUHITIMISHA MKUTANO WA NNE WA TUME YA PAMOJA

Waziri Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Liberata Mulamula (Mb) na Waziri wa Mambo ya Nje wa Kenya Mhe. Balozi Raychelle Omamo wakifuatilia Mkutano wa Nne wa Tume ya Pamoja ya Ushirikiano Ngazi ya Mawaziri uliofanyika jijini Nairobi, Kenya.

Mkutano wa Nne wa Tume ya Pamoja ya Ushirikiano kati ya Tanzania na Kenya  umehitimishwa leo  tarehe 24 Agosti 2021 kwa kusainiwa Hati tatu za Makubaliano ya ushirikiano kwenye masuala ya Diplomasia na Siasa, Elimu na Uhakiki wa Mpaka.

Mkutano huo ambao umeongozwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Liberata Mulamula kwa pamoja na Waziri wa Mambo ya Nje wa Kenya, Mhe. Raychelle Omamo umefanyika katika Hoteli ya Movenpick jijini Nairobi na kuwashirikisha Mawaziri, Makatibu Wakuu na Maafisa Waandamizi kutoka Tanzania na Kenya.

Akizungumza wakati wa Mkutano huo, Mhe. Balozi Mulamula amesema kuwa, amefarijika sana kwa Mkutano huo kufanyika kwa mafanikio na kueleza kuwa hiyo ni hatua muhimu kwenye mahusiano kati ya nchi na nchi na kwamba ana imani kubwa yale yote yaliyokubalika yatatekelezwa kwa ufanisi ili kufikia malengo tarajiwa ya nchi hizi mbili na Serikali kwa ujumla.

Alieleza kuwa, miongoni mwa mafanikio ya mkutano huo ni kusainiwa kwa hati tatu muhimu za makubaliano ambazo zitawezesha utekelezaji wa makubaliano kufanyika kwa ufanisi na kwa wakati kama ilivyokubalika. Hati zilizosainiwa ni ile ya Makubaliano ya Mashauriano ya Kisiasa na Kidiplomasia; Uhakiki wa Mpaka kati ya Tanzania na Kenya na Hati ya Makubaliano ya Ushirikiano katika Elimu ya Juu, Sayansi na Teknolojia.

Akielezea umuhimu wa kusainiwa kwa Hati ya Makubaliano kuhusu Uhakiki wa Mpaka Mhe. Balozi Mulamula alisema pamoja na mambo mengine kutazipa Nchi zote mbili msingi wa kisheria wa kuhakiki mpaka uliowekwa na wakoloni kwa kuuimarisha na kuweka alama zinazoonekana ili kuondoa mwingiliano wa jamii za mpakani na hivyo kupunguza migogoro ya mara kwa mara. 

Kadhalika alifafanua kuwa, Hati ya ushirikiano kwenye masuala ya elimu inalenga kuanzisha ushirikiano kati ya taasisi za pande zote katika maeneo ya Elimu ya Juu, Sayansi na Teknolojia ili kuleta manufaa kwa nchi zote katika kubadilishana uzoefu, kujenga uwezo wa masuala ya elimu ya juu, Sayansi na teknolojia kwa pande zote.

Kuhusu Hati ya Mashauriano ya Kisiasa na Kidiplomasia, Balozi Mulamula alisema ina umuhimu katikakuendeleza na kuimarisha mahusiano mazuri ya kisiasa na kidiplomasia yaliyopo kati ya Tanzania na Kenya na katika ngazi za kikanda na kimataifa. 

Kwa upande wake, Mhe. Balozi Omamo aliipongeza na kuishukuru Tanzania kwa kushiriki kikamilifu na kwa kuupa uzito wa hali ya juu Mkutano wa Nne wa Tume ya Pamoja ya Ushirikiano ambapo alisema kuwa hiyo ni dalili njema inayoonesha nia iliyopo ya kukuza ushirikiano wa kihistoria na kindugu uliopo kati ya Kenya na Tanzania.

Aliongeza kuwa, mbali na kusainiwa kwa Hati za makubaliano, Mkutano huo umepokea taarifa njema kuhusu utatuzi wa changamoto 30 kati ya 64 zilizokuwa zinaikabili sekta ya biashara baada ya kufanyika kwa Mkutano wa Mawaziri mwezi Julai 2021. Alisema, Mkutano wa Nne umeelekeza vikwazo 34 vya biashara visivyo vya kiforodha vilivyosalia kuondolewa kabla ya mwisho wa mwezi Desemba 2021 ili kuwezesha ufanyaji biashara kati ya nchi hizi mbili kuendelea kwa ufanisi.

Kadhalika alieleza kuwa, Mkutano huo pia umepokea taarifa kuhusu makubaliano ya ushirikiano katika Sekta ya Afya yaliyofikiwa wakati wa mkutano wa pamoja wa Mawaziri wa Afya uliofanyika jijini Nairobi hivi karibuni. Pamoja na mambo mengine ilikubalika nchi hizi mbili kuandaa utaratibu wa kushirikiana kwenye mapambano dhidi ya ugonjwa wa UVIKO-19  ikiwa ni pamoja na kushirikiana kwenye masuala ya upimaji na chanjo pamoja na kubadilishana Wataalam wa Afya.

Tume ya Pamoja ya Ushirikiano kati ya Tanzania na Kenya ilianzishwa rasmi mwezi Septemba 2009 jijini Arusha, Tanzania na kufuatiwa na Mkutano wa Kwanza wa Tume hiyo uliofanyika jijini hapo mwaka 2009. Mkutano wa Pili wa Tume hiyo ulifanyika jijini Nairobi, Kenya mwezi Septemba 2012 na Mkutano wa Tatu ulifanyika jijini Dar es Salaam mwezi Desemba 2016.

Mkutano wa Nne wa Tume ya Pamoja ya Ushirikiano kati ya Tanzania na Kenya umefanyika ikiwa ni utekelezaji wa maagizo yaliyotolewa na Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mhe. Uhuru Kenyatta, Rais wa Jamhuri ya Kenya walipokutana wakati wa ziara ya Mhe. Rais Samia iliyofanyika nchini Kenya mwezi Mei 2021.

Mbali na Mhe. Balozi Mulamula, Mkutano wa Nne wa Tume ya Pamoja ya Ushirikiano kati ya Tanzania na Keya umehudhuriwa na Mawaziri kadhaa kutoka Tanzania akiwemo, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. William Lukuvi, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mhe. Prof. Joyce Ndalichako, Waziri wa Madini, Mhe. Dotto Biteko, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar, Mhe. Khalid Salum Mohammed na Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki. Wengine ni Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhe. Khamis Chilo na Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Exaud Kigahe.

  • Waziri Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Liberata Mulamula (Mb) akisaini Hati ya Makubaliano kati ya Tanzania na Kenya katika Siasa na Diplomasia kwenye Mkutano wa Nne wa Tume ya Pamoja ya Ushirikiano Ngazi ya Mawaziri uliofanyika jijini Nairobi, Kenya.
  • Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe. Prof. Joyce Ndalichako (Mb) akisaini Hati ya Makubaliano kati ya Tanzania na Kenya katika Elimu, Sayansi na Teknolojia kwenye Mkutano wa Nne wa Tume ya Pamoja ya Ushirikiano Ngazi ya Mawaziri uliofanyika jijini Nairobi, Kenya.
  • Waziri Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Liberata Mulamula (Mb) akizungumza kwenye ufunguzi wa Mkutano wa Nne wa Tume ya Pamoja ya Ushirikiano Ngazi ya Mawaziri uliofanyika jijini Nairobi, Kenya.
Downloads File: