Skip to main content
News and Events

Tanzania na Uganda zaongeza wigo wa ushirikiano wa kiuchumi

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Jamhuri ya Uganda zimekubaliana kuongeza wigo wa ushirikiano wa kimkakati katika sekta muhimu za kiuchumi kwa lengo la kukuza uchumi wa mataifa hayo jirani na rafiki ya Afrika Mashariki pamoja na ustawi wa watu wake. 

Makubaliano hayo yamefikiwa leo Februari 7, 2026, katika mazungumzo yaliyofanyika jijini Dar es Salaam kati ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, na mgeni wake Rais wa Jamhuri ya Uganda, Mheshimiwa Yoweri Kaguta Museveni, aliyekuwa nchini kwa ziara ya kikazi ya siku moja.

Rais Mheshimiwa Dkt. Samia akizungumza na waandishi wa habari muda mfupi baada ya kuhitimisha mazungumzo hayo, mbali na kuelezea mafanikio yaliyofikiwa katika ujenzi wa Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (EACOP), amebainisha kuwa wamekubaliana kuendelea kufanya kazi kwa pamoja sambamba na kuongeza ushirikiano katika sekta muhimu za kiuchumi kwa manufaa ya pande zote mbili. 

Akizungumzia kuhusu sekta mpya za ushirikiano, alizitaja kuwa ni pamoja na ujenzi wa bomba la kusafirisha gesi kutoka Tanzania hadi Uganda, ujenzi wa bomba la mafuta safi kutoka Uganda hadi Tanzania, ujenzi wa reli ya Tanga–Mara itakayounganishwa na reli itakayojengwa upande wa Uganda, uzalishaji wa nishati ya umeme, upanuzi wa huduma za bandari kwa mizigo ya Uganda, pamoja na kuimarisha usafirishaji kwa njia ya maji. Aliendelea kubainisha kuwa meli mpya ya MV Mwanza, inayofanya shughuli zake katika Ziwa Victoria, itasaidia kuboresha huduma za usafiri na usafirishaji kwa upande wa Uganda.

Aidha, Rais Dkt. Samia aliongeza kuwa pande zote mbili zimekubaliana kuendelea kushirikiana katika ngazi ya kimataifa kwenye masuala mbalimbali yenye maslahi ya pamoja, huku akimhakikishia Rais Museveni kuwa Tanzania iko tayari kushirikiana na Uganda katika juhudi zake za kuanzisha mazungumzo ya kuleta amani katika Ukanda wa Maziwa Makuu.

Vilevile, pande zote mbili zimekubaliana kuendelea kuondoa vikwazo vya kibiashara ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Itifaki ya Soko la Pamoja la Jumuiya ya Afrika Mshariki. 

Kwa upande wake, Rais Mheshimiwa Museveni ameeleza kuwa makubaliano ya ushirikiano wa kimkakati yaliyofikiwa katika sekta mpya yatachochea kasi ya ukuaji wa uchumi na maendeleo ya wananchi wa pande zote mbili, pamoja na kukuza sekta nyingine zikiwemo viwanda na ajira.

Mbali na hayo, Rais Museveni amekumbusha na kusisitiza umuhimu wa pande zote mbili, na Afrika kwa ujumla, kusimamia maendeleo ya nchi na ustawi wa wananchi, ikiwa ni mojawapo ya njia za kuenzi malengo ya uhuru wa Afrika na kutimiza maono ya waasisi wake. Alisisitiza kuwa ushirikiano huu wa kimkakati kati ya Tanzania na Uganda ni hatua muhimu kuelekea ukuaji endelevu wa uchumi na kuimarisha umoja wa Afrika.

Rais wa Jamhuri ya Uganda Mheshimiwa Yoweri Kaguta Museveni amehitimisha ziara yake ya kikazi ya siku moja hapa nchini na kurejea nchini Uganda.